Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akijadiliana jambo na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Bw. Gishuli Charles (wa nne kushoto), wakati alipoanza ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu katika Mkoa wa Singida. Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu, na wa tatu kushoto ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo akimuonesha Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa uharibifu wa barabara unaotokana na ajali za barabarani katika barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilometa 89.3 mkoani Singida.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo (wa tano kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa nne kushoto) kuhusu mradi wa ujenzi wa mzani katika barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya ambao ujenzi utakamilika hivi karibuni.
Muonekano wa ujenzi wa kituo cha Mzani Itigi, kinachojengwa katika barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, mkoani Singida.
Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akionesha moja ya picha ya uharibifu wa alama za barabarani uliofanywa na wananchi katika ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilomita 89.3. Kwa picha zaidi BOFYA HAPA
--------------------------------------------------------------------------------------
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amewaagiza viongozi wa Serikali kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi mkoani Singida kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaohujumu miundombinu ya barabara na kuisababishia hasara Serikali.Profesa Mbarara ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilomita 89.3 kwa kiwango cha lami na kubaini kuwa baaadhi ya wananchi wameanza kuhujumu barabara hiyo.
“Tumepanga kujenga barabara ya Mkiwa-Itigi-Makongolosi kwa kiwango cha lami, sasa kitendo cha kuanza kuhujumu barabara iliyokwisha kamilika ni kitendo kisichokubalika na hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa kila mwananchi wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kuilinda miundombinu ya barabara, reli na mawasiliano ambayo inajengwa kwa fedha nyingi ili idumu kwa muda mrefu.
“Tutaimarisha stesheni ya Itigi na kuimarisha mawasiliano ya simu ili kuwezesha eneo hili kuwa na mawasiliano ya uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa mzani wa kupima magari katika eneo la Bumbuwa katika ya barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya na kumtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo kuhakikisha ujenzi wa mzani huo unakamilika kwa wakati na magari yote yanayostahili yanapimwa.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa kilomita 89.3 umekamilika kwa asilimia 98 na umehusisha makalvati makubwa 48 madogo 118.
Zaidi ya shilingi bilioni 109.6 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya iliyojengwa katika mfumo wa usanifu na ujenzi ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Manyoni-Itigi-Chaya-Nyahua hadi Tabora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...