Tayari dunia imeshuhudia maendeleo ya teknolojia yanayowezesha matumizi ya seti kubwa za data zinazoweza kuchambuliwa ili kuonyesha mwelekeo, hasa kuhusiana na vitendo vya binadamu (big data), mifumo ya kompyuta inayoweza kufanya kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili na utashi wa binadamu (Artificial intelligence).
Mipango iliyotangazwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu matumizi ya masafa kwa ajili ya kuendeleza teknolojia ya uzao wa tano wa mawasiliano ya kasi, yaani 5G na mwongozo wa vitu vinavyounganishwa na kuwasiliana kwenye mtandao wa intaneti (machine to machine communication) itaharakisha utekelezaji wa mikakati hii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA,Dr. Jabiri Kuwe Bakari, masafa yaliyobainishwa kutumika kwa teknolojia ya 5G yatatolewa kwa mfumo wa mnada, na tayari TCRA imetoa waraka wa mashauriano kwa umma kuhusu utaratibu utakaofuatwa.
Utaratibu wa TCRA wa kutoa kwa muda, bila malipo, raslimali za mawasiliano kwa wavumbuzi katika TEHAMA/dijitali kwa ajili ya majaribio ya huduma mpya pia utachangia mafanikio haya. Chini ya utaratibu huu, mvumbuzi anapewa namba na misimbo ya mawasiliano, kikoa cha dot tz (.tz) na masafa ya mawasiliano. Kikoa kinawezesha huduma zzinazotumia mtandao wa intaneti.
Sensa ya mwaka huu imekuja wakati Tanzania inatekeleza mpango kabambe wa kuifanya nchi iwe ya kidijitali, kuanzia kwenye matumizi ya huduma za mawasiliano ya mtu mmoja binafsi na taasisi za umma na binafsi kupata na kutoa huduma. Imekuja miaka mitatu kabla ya mwaka 2025, ambao uko kwenye mikakati yote ya kuendeleza TEHAMA nchini.
Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mradi wa Tanzania ya Kidijitali na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) vina malengo yanayotakiwa kutekelezwa ifikapo 2025. Hayo ni pamoja na kufikisha huduma za intaneti kwa asilimia 80 ya Watanzania na kuinua kiwango ch uelewa wa masuala ya TEHAMA miongoni mwa wananchi.
Utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali unatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya mawasiliano kwa pato la taifa kutoka asilimia 1.5 hadi tatu (3) ifikapo 2025.
Mikakati mingine hadi 2025 na kuanza kutumika kwa mawasiliano ya uzao wa tano; yenye kasi kubwa na fursa nyingi, kupanua mkongo wa taifa wa mawasiliano na kutumia teknolojia mpya kwenye maeneo mbalimbali na kujenga vituo vitano (5) vya kusajihisha uvumbuzi wa kidijitali na ujasiriamali.
Kwa ujumla, majibu ya maswali kuhusu simu na vifaa vya mkononi vya mawasiliano, hali za kipato, mahali walipo wanaohojiwa na shughuli zao za kujikimu, viwango vya elimu pamoja na mfumo wa anwani na postikodi vitafanikisha mawasiliano na huduma zinakazojitokeza kama sehemu ya utekelezaji wa mipango na mikakati hiyo.
Hivi sasa asilimia 95 ya Watanzania wapo kwenye maeneo yenye mtandao wenye uwezo wa kutoa huduma za simu za sauti na jumbe fupi, kupitia minara 12,228. Aidha, asilimia 68 ya Watanzania wako kwenye maeneo yenye mtandao wenye uwezo wa kutoa huduma za intaneti ya kasi ya uzao wa tatu (3G) kupitia minara 11,753 na asilimia 45 wapo kwenye maeneo yenye mtandao wa 4G kupitia minara 6,656.
Majibu ya maswali kuhusu milki na aina ya matumizi ya simu zenye uwezo mkubwa (simu janja – zinazowezesha matumizi ya intaneti), simu za kawaida, kompyuta za mezani na mpakato yamelengwa kupata taarifa kuhusiana na kuenea kwa TEHAMA.
Ingawaje asilimia 68 ya Watanzania wako kwenye maeneo yenye huduma ya intaneti, ni asilimia 27 tu ya watumiaji wa huduma za mawasiliano wenye simu janja au vifaa vingine vya mawasiliano vyenye uwezo wa kutumia intaneti.
Kuenea kwa matumizi ya simu za mkononi kumewezesha utoaji, upatikanaji na matumizi ya huduma nyingi za mawasiliano. Pamoja na kufanikisha mawasiliano ya sauti zimewesha matumizi kwa huduma za kifedha, intaneti na shughuli mbalimbali.
Kwa mfano, hadi Juni 2022 kulikuwa na laini za simu zilizosajiliwa milioni 56.3. Idadi hii ni zaidi ya watumiaji mmoja mmoja kwani kuna watu wenye zaidi ya laini moja kwa sababu mbalimbali zikiwemo aina ya matumizi na upatikanaji wa huduma pale walipo.
Watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu waliongezeka kwa asilimia 31 ndani ya mwaka mmoja, kutoka 27,326,938 mwezi Aprili, 2021 hadi kufikia 35,749,298 mwezi Aprili, 2022.
Pamoja na kuongoza kwenye uwiano wa watumiaji wa intaneti na wananchi wake, Tanzania iko juu kwenye usalama kwenye matumizi ya intaneti. Ni ya pili Afrika kwa usalama mtandaoni, ikiwa imependa kutoka nafasi ya 11 mwaka 2015, kwa mujibu wa Fahirisi ya Dunia ya Usalama mtandaoni (Global Cybersecurity Tanzania. Mauritius ni ya kwanza, Kenya ya tano, Rwanda ya saba na Uganda ni ya tisa. Fahirisi hiyo inatolewa na ITU, Shirika la Umoja wa Mataifa linalisimamia TEHAMA.
Kipengele kingine muhimu cha sensa ya 2022 ni matumizi ya mfumo wa anwani za makazi, ambamo umewezesha nyumba kuwa na namba na mitaa na barabara kupewa majina na kuwekewa vibao vya utambulisho. Lengo ni kuwezesha watoa huduma kufikia kaya husika kwa urahisi. Unawezesha mtu kutambuliwa kipekee kutokana na eneo analoishi au kufanyia shughuli zake.
Faida nyingine ni pamoja na kufanikisha shughuli za taasisi za dola zinazotaka kuwasiliana na wananchi kwa sababu mbalimbali kama vile kodi, huduma za afya, huduma za zimamoto na dharura nyingine. Mfumo unainua ubora wa huduma za kusambaza barua, vifurushi na vipeto nchini na kimataifa kati ya Tanzania na nchi nyingine na ni muhimu kwenye kufikisha vitu vitakanunuliwa mtandaoni chini ya huduma za biashara mtandao.
Aidha umewezesha kuanzishwa kanzidata ambayo inaweza kutumiwa na wafanyabiashara kama nyenzo muhimu ya kutangaza biashara zao na kwa tafiti za takwimu. Vile vile unatarajiwa kuboresha makazi ya watu Tanzania, na ni nyenzo inayoendana na mkakati wa serikali wa kutokomeza umaskini na kuboresha mipango vijijini.
Utafiti uliofanywa na TCRA kuhusu matumizi ya mfumo huu katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Zanzibar and maeneo ya Pemba ulionyesha kwamba asilimia 66 ya watu, ikiwa ni pamoja na asilimia 93 ya madereva wa teksi, bodaboda na pikipiki za miguu mitatu, yaani bajaj walikuwa wanatumia mfumo huu kwenye shughuli zao za kila siku.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...