Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa ,Abdulrahman Kinana ameeleza Hayat Mwalimu Nyerere alikuwa sio kiongozi wa matukio ,Wala kujikweza Ila alikuwa kiongozi aliyeamini anachokifanya na hakuwahi kutetereka.
Aidha ameeleza ,Baba wa Taifa alikuwa kiongozi wa kimkakati ,muafilifu na mfano wa kuigwa Duniani .
Akifungua mdahalo wa kumbukizi ya miaka 23 ya Mwalimu Julius Nyerere,ulioandaliwa na Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwamfipa Kibaha Mkoani Pwani,Kinana alisema kiongozi lazima uwe na maono na ushawishi kwa mambo unayoyaamini na sio kuwa kiongozi wa matukio .
"Baba wa Taifa alikuwa na misingi imara kwa mambo aliyoyaamini, kiongozi hatakiwi kujikweza ,kujiona ,"Kiongozi haendi kwa hali ya hewa kwa kusukumwa kwa kufurahisha watu,aliamini kwenye umoja usiojali ukabila,udini ,alijenga msingi huo na hadi leo tukauamini"
Kinana alieleza ,Uongozi bora ni kufuata misingi aliyoiacha Hayat Nyerere kwa kufanya mambo unayoyaamini badala ya kusukumwa na hali ya hewa ili kufurahisha watu.
Aidha alieleza kwamba ,Baba wa Taifa aliamini kwenye Umoja usiojali Ukabila,Urangi,Udini ,Uasili pamoja na kujenga Umoja ,Mshikamano na kuwa kiongozi mwenye maono.
Hata hivyo Kinana alieleza, kiongozi awe mwenye kuacha alama kwa nafasi anayoiongoza .
"Kwa hili tutakumbuka baba wa Taifa licha ya kustaafu Lakini aliwahi kualikwa Kama kiongozi wa kipekee kutoka Afrika kushuhudia usuluhishi katika kisiwa cha Hongkong kukirudisha kutoka katika mikono ya waingereza, Hapa tutaona namna alivyoaminika Duniani,"
"Mkipewa nafasi lazima ujiulize katika nafasi unayoiongoza unataka ufanikiwe nini,uweke ushawishi gani na utaacha alama gani eneo unaloliongoza,sio kuwaswaga watu kama ng'ombe "alifafanua Kinana.
Kinana alieleza wapo Marais wengi Duniani wakiwemo kwenye bara la Afrika ambao hawakumbukwi ,ila yeye alikuwa mtu wa kipekee Duniani ambae anaendelea kukumbukwa kwa Kuwa kiongozi wa kisiasa na kimkakati.
"Ni vigumu kumzungumzia uongozi wake muasisi wetu, nikamaliza yote ila iweze kutosha kusema kwa niliyoongea leo yamekidhi"Na kila siku tunaendelea kujifunza kutokana na uongozi na maisha yake "alieleza Kinana.
Nae Mkuu wa shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Marcelina Chijoriga alielezea ,kuanzishwa kwa shule hiyo ya uongozi kutawezesha viongozi na vijana kukwiva kwenye masuala ya uongozi uliobora.
Alisema hadi sasa wameshaendesha kozi nne na mkakati ni kuendesha kozi nyingine.
Marcelina alieleza, shule hiyo sio ya CCM pekee,ni shule inayoendeshwa na vyama vyote sita vya Ukombozi SWAPO -Namibia,MPLA-Angola,ANC -Afrika ya Kusini,FRELIMO-Msumbiji ,CCM -Tanzania na ZANUPF Cha Zimbabwe.
Aliwaasa vijana kuja kujitokeza kutumia fursa hiyo ,ili kuongeza uwezo wa kujifunza kwa kina na kuwa wabobezi wa masuala ya uongozi na siasa.
"Tunategemea washiriki kuwashirikisha mlete mabadiliko katika maisha ya watu, uongozi wa mabadiliko wa maisha ya watu"alielezea Marcelina.
Alimkaribisha mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ,Petro Paulo Kimiti aliomba Serikali kuwapa kibali cha eneo la hekari 500 ili kujenga makumbusho rasmi ya Baba wa Taifa huko makao makuu ya nchi Dodoma.
Alisema kwa hatua hiyo sio kwamba kutakuwa na makao makuu ya Serikali bali kutakuwa na kumbukizi ,utalii mkubwa na historia ya Mwalimu Nyerere.
Alisema siasa ya kujitegemea ndio nguzo ya Taifa na ambao tumekuzwa nazo ni wajibu wao kusimamia malengo hayo ya baba wa Taifa.
"Tuyasimamie na tusipoteze misingi iliyojengwa na muasisi wetu kama sio juhudi zake tusingefika hapa tulipo"alisisitiza Kimiti.
Pia alisema miaka ya zamani kulikuwa kunatolewa tuzo kwa viongozi waliofanya vizuri nchini kwenye uongozi wao ,aliomba tuzo hizo zirejeshwe ili kuhamasisha wengine kujituma.
"Tuzo zinakufa sijui kwanini ,tuangalie upya hili , zamani tulipewa tuzo ili kuhamasisha wengine,kwa kurejesha tuzo itasaidia na kundi la vijana kujituma,waache kuchezea kazi ,tusimamie misingi hii kuwajenga vijana hawa "alieleza Kimiti.
Akichangia katika mdahalo Abbas Mwalimu, kutoka chuo Cha Diplomasia Kurasini alisema uongozi sio kutumia mabavu, uongozi ni kuwa na ushawishi kwa wengine na kuacha alama kwa wale unaowaongoza.
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Wilson Mukama alisisitiza uadilifu na uaminifu , huwezi Kuwa kiongozi Kama sio muaminifu hasa katika fedha.
Alieleza, rushwa ni kipimo vya uongozi , kiongozi anaefaa lazima akemee rushwa ,rushwa ni mwiko.
Vilevile aliyewahi kuwa Waziri wa Utumishi Fatma Saidi Ally akizungumzia mada ya wanawake na uongozi alisema kwasasa kuna mchango mkubwa kwa kundi la wanawake kushiriki kwenye ngazi mbalimbali za Uongozi na Maamuzi.
Alieleza ,mada hiyo amepewa kwa wakati muafaka kwani Tanzania imempata Rais wa kwanza mwanamke Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema , mafanikio haya ni misingi ya Mwalimu Nyerere kupigania wanawake kuwa ngazi mbalimbali za Maamuzi ambapo sasa imefikia asilimia 43 kwa upande wa utumishi,nafasi ya wakuu wa wilaya imefikia asilimia 44,majaji asilimia 45.
"Zamani Wanawake walikuwa waoga ,wakikatazwa kushiriki mambo makubwa , hawana uhuru wa kusema ,kufanya Maamuzi kwasasa mabadiliko makubwa yanaendelea kufanywa , hii yote Hayat Mwalimu Nyerere yupo nyuma yetu kwani UWT alikuwa akitoa ushauri mbalimbali."
Fatma aliomba wanawake wajiamini ,kwani wameshuhudia Rais Samia akienda mbio kufikia 50-50 . Nafasi ya ubunge viti maalum wanawake wamepata uzoefu sema kwenye ubunge bado haijakaa vizuri, mabadiliko haya yanahitajika ili kufikia 50 kwa 50 au kuzidi hapo.
Alitaka wanawake kupigania haki zao na watoto ,ili kupunguza matukio ya ubakaji na ulawiti yanayotokea kila siku ambapo unakuta mtoto anabakwa na baba ,mjomba wake au baba wa kambo.
Aliwataka wananchi waendelee kuunga mkono kazi kubwa anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan.



Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa ,Abdulrahman Kinana (wa tatu kulia) akiwa na viongozo Waandamizi wa Taaisis na Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere pamoja na Wageni waalikwa wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikitolewa ukumbini humo mara baada ya ufunguzi wa mdahalo wa kumbukizi ya miaka 23 ya Mwalimu Julius Nyerere,ulioandaliwa na Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere,Oktoba 12,2022 Kwamfipa Kibaha Mkoani Pwani.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-KIBAHA PWANI.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...