— Yakabidhi Sh29.82 Bilioni kwa Rais Samia; 

— Mchechu asifu ubunifu na nidhamu ya taasisi; Silayo aeleza mikakati mipya ya mapato endelevu


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kujiimarisha kama taasisi kinara katika kuchangia mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali, baada ya kukabidhi hundi ya Sh29.82 bilioni kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, Jumanne, Juni 10, 2025.

Kiasi hicho kimeiweka TFS katika nafasi ya tatu kitaifa, ikitanguliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), miongoni mwa taasisi zinazowasilisha asilimia 15 ya mapato ghafi moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika hafla ya Siku ya Gawio 2025 iliyoongozwa na Rais Samia, yenye kaulimbiu “Mageuzi ya Mashirika ya Umma na Wajibu wa Kuchangia Maendeleo ya Tanzania,” Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema TFS imebadilisha mwelekeo wa kimapato kwa kuwekeza kwenye vyanzo endelevu visivyoegemea biashara ya mkaa.

 “TFS wamechangia Shilingi bilioni 29.8 kutoka Sh21.3 bilioni mwaka uliopita. Mheshimiwa Rais, wametekeleza maagizo yako—hawajategemea mapato ya mkaa. Asanteni sana. Kama mkitusaidia hata kwa asilimia 50 ya hii bilioni 29.8, mwaka ujao tutajipanga vizuri zaidi kuhakikisha ongezeko linaendelea,” alisema Mchechu.

Katika mahojiano maalum muda mfupi baada ya kukabidhi hundi hiyo, Kamishna wa Uhifadhi na Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisema mafanikio hayo yametokana na ubunifu, uimarishaji wa nidhamu ya kazi kwa watumishi, na mabadiliko ya mtazamo kuhusu thamani ya misitu.

“TFS imewekeza katika rasilimali watu, teknolojia na miundombinu ya ukusanyaji mapato kutoka mashamba ya miti, ufugaji nyuki, utalii wa misitu, na sasa biashara ya kaboni,” alisema, na kuongeza kuwa mapato ghafi ya wakala yamekuwa yakikua kwa wastani wa asilimia tisa kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.

Alibainisha kuwa huduma mpya kama utalii wa ikolojia, mbio za magari katika mapori ya hifadhi, michezo ya boti na makasia kwenye mabwawa, pamoja na huduma za kupiga picha katika misitu iliyohifadhiwa (photographic safaris), zimeongeza mvuto wa misitu kama maeneo ya burudani na vyanzo vya ajira.

Miongoni mwa sababu kuu zilizosukuma ongezeko la mapato ni matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyounganishwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao. Mfumo wa e-Misitu unaruhusu malipo ya vibali, ada na tozo za mazao ya misitu kwa njia ya kielektroniki—hatua iliyosaidia kupunguza uvujaji wa mapato na kuongeza uwazi.

“Tuliweka mifumo ya ufuatiliaji wa dakika hadi dakika (real-time) ili kuona kila shilingi inayoingia na kutoka. Sasa tunaweza kutambua mianya ya upotevu na kuchukua hatua haraka kuongeza tija,” alieleza Prof. Silayo.

Aliongeza kuwa, katika maandalizi ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa (Zero-Net Emissions 2050), TFS tayari imetambua akiba ya hewa ukaa (carbon stock) katika misitu yake mikuu na ipo katika mazungumzo na wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kaboni itakayouzwa kimataifa.

“Tumeanza hatua za tafiti za msingi (baseline studies) na tayari tunao washirika waliotoa nia. Kilichobaki ni kukamilisha tafiti za kina na kuingia mikataba ya kimataifa. Sheria na miongozo ya kitaifa sasa ipo tayari kuhakikisha uwekezaji una ulinzi wa kisheria,” alisema Prof. Silayo.

Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, ongezeko la gawio kutoka taasisi kama TFS litaiwezesha Serikali kugharamia miradi ya kipaumbele kama ujenzi wa shule, vituo vya afya na miundombinu ya maji safi, hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje.

Hata hivyo, Bw. Mchechu alizitaka taasisi za umma ambazo bado hazijafikia viwango vya kutoa gawio au asilimia 15 ya mapato ghafi, kubadili mwelekeo wa utendaji wao.“Muda wa visingizio umeisha. Gawio ni kipimo cha utendaji, uwajibikaji na thamani ya fedha za umma,” alionya.

Akihitimisha hafla hiyo, Rais Samia aliipongeza TFS pamoja na taasisi nyingine zilizokabidhi hundi za gawio, akisisitiza: “Mageuzi ya kiuchumi tunayoyataka hayatatokana na chanzo kimoja cha mapato, bali ubunifu na uwajibikaji wa kila taasisi.”








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...