Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika banda lao kwenye Maonyesho ya 31 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha, ili kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi na huduma nyingine muhimu zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa EWURA, Mhandisi Lorivii Long'idu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, ambapo alieleza kuwa EWURA inatumia maonyesho hayo kama jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, hususan katika sekta za mafuta, umeme, gesi, na maji.

“Tunatumia fursa hii kusisitiza matumizi ya nishati safi siyo tu kwa ajili ya kulinda afya ya jamii, bali pia kwa kulinda mazingira,” alisema Mhandisi Long’idu, akisisitiza kuwa tafiti mbalimbali, ikiwemo zile kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), zimebaini kuwa magonjwa mengi ya mfumo wa upumuaji yanatokana na matumizi ya kuni na mkaa majumbani.


Mhandisi Long'idu alibainisha kuwa EWURA ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa miaka 10 wa Serikali unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 30 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi kama gesi, badala ya kuni na mkaa.

Aidha, aliongeza kuwa EWURA inasimamia kwa karibu ubora na usambazaji wa gesi, kuhakikisha kuwa wananchi wanapata bidhaa yenye ujazo sahihi. Alisema baadhi ya mawakala wasio waaminifu tayari wamechukuliwa hatua za kisheria na kesi zao zipo mahakamani.

“Ni jukumu la kila msambazaji mkubwa kuhakikisha kuwa wauzaji wadogo wanafuata sheria. Wananchi nao wanapaswa kuhakiki kuwa gesi wanayonunua imejaa kikamilifu na kupimwa vizuri,” alieleza.

Sambamba na hilo, alitoa wito kwa wananchi kufika kwenye banda la EWURA kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo, pamoja na kutoa taarifa au malalamiko kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kwenye huduma za umeme, maji, mafuta na gesi ili zitafutiwe suluhisho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...