Na Said Mwishehe


NATAKA niseme kabisa na utaamua uwe upande gani lakini ukweli Oktoba 29 mwaka huu katika nchi yetu tumeshuhudia makundi ya vibaka na wahalifu.

Ndio Oktoba 29 nchi yetu haikuwa na waandamanaji, kwanza hatukuona mahali kokote watu wakiandamana ila macho na masikio yetu yameshuhudia vibaka wakipora, kuiba na kuharibu mali za Watanzania wenzao.

Ni mambo ya hovyo kabisa kuwahi kutokea katika nchi. yetu. Ndio tangu nchi imepata uhuru hatujawahi kushuhudia tulichokishuhudia Oktoba 29 mwaka huu.

Naona unataka kuuliza kama hayakuwa maandamano ilikuwa nini? Acha kujitoa ufahamu, iko hivi wandamanaji huwa na utaratibu wa eneo la kuanzia maandamano na pale watakapoishia.

Kwa mfano maandamano yataanza pointi A na yatakwenda Pointi B.Yaani ni hivi maandamano yataanzia Jangwani na kuishia Temeke.Sasa tujiulize maandano ya Oktoba 29 yalianzia wapi na kuishia wapi? Tulichoshuhudia ni makundi ya watu walioamua kufanya waliyoyafanya.

Lakini pili maandamano yanakuwa na ujumbe maalumu dhidi ya kile ambacho wanakitaka kwa Serikali au mamlaka husika. Kwa mfano wanataka Tume Huru ya Uchaguzi basi tulipaswa kuona mabango yenye ujumbe kuhusu madai yao.

Oktoba 29 haikuwa hivyo, hakuna aliyekuwa na bango kuonesha ujumbe wao.Hakuna maandamabo ya namna hiyo.Ukweli tulishuhudia watu waliokuwa na lengo la kufanya uhalifu tena uhalifu mkubwa.

Hebu kwa akili ya kawaida tujiuilize yaani mnaandamana mnakwenda kwenye baa mnavunja mnaingia kaunta mnabeba vileo, mnachukua televisheni,mnachukua hela ,mnachukua muziki uliopo.Hebu tujiulize hayo ndio maandamano?

Tujiulize watu wanafunga barabara ambazo ni haki kutumiwa na raia wengine mnataka watu wasipite.Kibaya zaidi wamesimamisha malori yenye mizigo inayosafirishwa ndani na nje ya nchi yetu wamechoma moto.

Hao ambao mnawaita waandamanaji wameharibu miundombinu ya usafiri kwa mfano Dar es Salaam vituo vya mwendo kasi vimechomwa moto,mabasi yameteketezwa .Hivi ndio kuandamana huko? Kwahiyo kuchoma mwendokasi ndio tumepata Katiba Mpya?

Vituo vya polisi vimechomwa katika maeneo mbalimbali, unashangaa nini sasa ?Acha kujitoa akili.Hao unawaita waandamanaji wamechoma baadhi ya vituo vya polisi .Ninaposema walikuwa waalifu unielewe.

Tujiulize kudai Katiba Mpya kuna uhusiano gani na kuchoma vituo vya mafuta vilivyopo? Lake Oil vituo vyake saba vimechomwa Oktoba 29 halafu anatokea mtu anaona ni sawa tu.Tuna mijitu ya ajabu sana.

Tunaambiwa kitendo cha vituo saba vya Lake Oil kuchomwa moto Watanzania 300 wamepoteza ajira kwasababu tu kuna watu waliamua kufanya uharibu. Watu 300 kukosa kazi unajua nyuma yao kuna watu wangapi walikuwa wanawategemea?

Leo hii wakati wewe unatetea hao unaowaita wandamanaji akili kwako unatakiwa ufahamu kuna watu hawajui hatma ya maisha yao.Ndio kama alikokuwa anapategemea pamechomwa moto anaishije.

Tumekuwa tukijenga hoja nyingi kutetea ,unajenga hoja kutetea wezi na vibaka? Unatetea hadi mishipa ya shingo inakutoka. Hovyo kabisa.Unawatetea watu waliokuwa wamebeba viberiti na mafuta ya petroli kwa ajili ya kuchoma mali za watu wasio na hatia, kweli?

Mabasi ya Shabiby yana makosa gani katika nchi hii,au kutusafirisha kutoka mkoa mmoja hadi mwingine ndio kosa lao? Unachoma mabasi bila kuwa na huruma halafu unataka uonewe huruma.Nani anayemtetea au kumsemea Shabiby ambaye mabasi yake yamechomwa moto Oktoba 29.

Unakwenda kuchoma mabasi ya Ester kwasababu gani, kosa lake nini? Au kuwa na kampuni ya usafirishaji na kuajiri Watanzania wafanye kazi ndio kosa lake?

Hivi wenye mabasi wakiamua kuweka mabasi yao katika maegesho ninyi mnaojifanya waandamanaji mnatusaidiaje.

Nilijaribu kuuliza kwanini mabasi ya Shabiby na Ester yamechomwa eti naambiwa kwasababu wenyewe ni wanasiasa na wako chama tawala,sasa tujiulize katika nchi hii ukiwa mwanasiasa wa chama tawala ni dhambi?

Lazima ifike wakati kwenye ukweli tuseme,tutetee panapostahili na pale ambapo tunaona kilichofanyika sio sawa tuseme ukweli.Narudia tena kilichotokea Oktoba 29 ni baadhi ya watu wameamua kufanya uporaji na uharibifu wa mali tena nyingine za watu wasiokuwa na hatia kabisa.

Kwa uchumi wa watu wengi wa Taifa hili ukiona ana kaeneo kake ka biashara ujue ametumia nguvu na akili nyingi kupata mtaji halafu anatokea mtu au kikundi cha watu wanachoma moto. Hivi ninyi waandamanaji mnajua ni kwa kiasi gani mmepanda mbegu ya chuki katika mioyo ya watu wema.

Unaweza kusema na hao ndio wale wale sasa nakwambia hivi kama ukisema ukweli ndio wale wale basi niko tayari,ila utakavyotaka,sema utakavyojisikia lakini haitabadilisha ukweli kilichofanyika Oktoba 29 ni wizi, uporaji na uharibifu wa mali.

Kuna wengine waliokuwa wakifanya hizo vurugu ni kama walikuwa wamevaa roho za magaidi kabisa maana sifa ya magadaidi mojawapo ni kujenga hofu kwa raia wema na hicho ndicho walichokifanya siku hiyo. Unachoma magari, unafunga barabara ili watu wasipite?.

Nini kifanyike? Kuna haja ya kujitafakari kama Taifa,tulikotoka tulipo na tunakokwenda. Kilichotokea Oktoba 29 hakileti picha nzuri kwa Watanzania ambao msingi wetu mkuu ni amani,umoja ,upendo na mshikamano.

Tuhakikishe tunadumisha amani ya nchi yetu,tuilinde na kuipenda Tanzania yetu,hatuna Tanzania nyingine zaidi ya hii tuliyonayo.

Nafahamu nguvu ya viongozi wa dini katika kuhamasisha amani ya nchi yetu ,niwaombe viongozi wa dini zote mtusaidie kuhubiri amani. Hata baba Askofu Gwajima nawe unayo nafasi ya kuhubiri amani ya Taifa hili.

Lakini natambua tunao viongozi wa kisiasa nataka niwaambie hatma ya amani ya Taifa letu iko katika mikono yenu,umoja na mshikamano wa Taifa la Tanzania uko katika vinywa vyenu. Zungumzeni yanayojenga badala ya kubomoa,jadilini yanayotuunganisha badala ya kutugawa,hubiri amani badala ya vita.

Wakati tunaelekea Oktoba 29 tumesikia kauli nyingi za wanasiasa. Hata zile za kwamba lazima Oktoba 29 tukinukishe tunazikumbuka. Haya mmekinukisha mmepata faida gani au mnafurahia damu zilizomwagika. Chungeni ndimi zenu.

Kwa waandishi wa habari wa Tanzania uzalendo ni kitu muhimu sana,mnayo nafasi kubwa ya kuliunganisha Taifa hili kupitia vyombo vya habari mnavyovitumikia.Tuangalie utanzania wetu zaidi badala ya maslahi yetu binafsi.

Vyombo vya nje haviwezi kuizungumzia Tanzania yetu vizuri,kuharibikiwa kwetu ndio furaha yao.Utulivu wa nchi yetu unawaumiza wengi wanatamani kuona tunaharibikiwa.

Hivyo Media ya Tanzania ndio inayoweza kuliponya Taifa hili maana nguvu ya kalamu ya mwanahabari ni kubwa kuliko nguvu ya risasi.

Jadilini maoni ya kujenga maana waandishi wa nje ya Tanzania wao wamejikita katika maswali chonganishi.Wanapenda kusikia tukitamka mabaya ili wapate cha kuandika.

Lakini nitoa ushauri kwa wanaharakati na wale wanaopigania haki za binadamu tunajua wapo wanaowafadhili lakini huo ufadhili wao usiwapofushe macho ,usiwatoe akili mkasahau nchi yenu,mkasahau umuhimu wa amani ili kuwafurahisha wanaowatumikia.

Pamoja na yooote hayo kuna hii kitu inaitwa kupigania haki,ni kweli unapigania haki lakini tuulizane ni haki gani ambayo unaipigania.Ni haki ya kuwa viongozi wakuu wa nchi?

Ninyi ambao mnapambana kusaka hiyo haki ya kuwafikisha kwenye uongozi wa nchi acheni kutumia rasilimali watu wa taifa hili vibaya.

Na ukweli hakuna haki mnayopigania zaidi ya kupigania maslahi yenu, mko tayari kuona watu wanakufa ili mambo yenu yawanyookee.Kwa vijana tupunguze mihemko, tusiwe kama kasuku kila unachoambiwa unakifuatisha,tusiwe

Kama Manyumbu hata kwenye hatari tupo tupo.Tumepewa akili na Mungu ili zitusaidie kuwaza na kufikiria .

Tusiishi kwa mihemko kwasababu wale wameharibu amani yao na sisi tuiharibu ya kwenda. Sishangai kuona majirani zetu wanavyoshabikia kilichotokea Oktoba 29 kama wanavyoshabikia mpira katika vibanda umiza.

Inatosha kwa leo. Waliotangulia mbele ya haki Allah uwapokee na kila mmoja umpe haki yake kwa jinsi anavyostahili maana wewe ni mwenye haki.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...