
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuna mengi zaidi ambayo Serikali imejipanga kuyafanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo huku akisisitiza ni dhima ya Serikali kuendeleza ukuaji wa Uchumi.
Hivyo amesema katika kipindi hiki Serikali itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 hadi 2050, ikilenga kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
Akizungumza Bungeni Mjini Dodoma leo Novemba 14,2025 akilihutubia Bunge la Tanzania la 13,Rais Dk.Samia amesema Dira mpya imeweka vigezo vya kuchagua sekta na maeneo ya kupewa kipaumbele yaliyobainishwa kwenye andiko la Dira yenyewe.
Amesema kati ya mikakati itakayofanyiwa kazi ni kuwekeza zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi na miongoni mwa sekta hizo ni kilimo, utalii, viwanda, ujenzi na madini.
“Malengo yetu ya kiuchumi ni kupandisha kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.6 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 7 kuelekea mwaka 2030. Ukuaji huu utaiwezesha Serikali kuboresha huduma za kijamii na kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi.
“Tutaimarisha masoko ya mitaji kwa kuhamasisha uwekezaji wa ndani, na kutumia rasilimali zetu kama madini kudhamini mikopo ya uwekezaji, badala ya kuweka mzigo mkubwa kwenye Deni la Taifa. Mwelekeo wetu ni kukua kwa pamoja kwa uchumi unaogusa maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi jumla.
“Mtakubaliana nami sekta binafsi ni nguzo muhimu ya ukuzaji wa uchumi, hususan Sekta Binafsi ya ndani. Tutaboresha zaidi mazingira ya biashara nchini kwa kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).”
Pia amesema Serikali itatekeleza mapendekezo ya Tume niliyoiunda ya Kuboresha Mifumo ya Kodi nchini ili kuwapatia wafanyabiashara wepesi katika kufanya biashara zao.
Ameongeza Serikali itaendelea kuweka nguvu zaidi kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa ambayo ni hatua muhimu katika kupunguza gharama za maisha kwa Wananchi.
“Pia tutaweka motisha kwa viwanda vya ndani ili viweze kuzalisha kwa gharama nafuu na kuuza kwenye soko la ndani na nje. Tutaongeza vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuchochea uzalishaji na kukuza ushindani wa bidhaa za ndani.
“Mbali na mikopo, tutafungua fursa mahsusi kuhamasisha vijana na wamiliki wa biashara ndogo kupata elimu ya biashara na kuweza kujisajili katika Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Serikali (TANSIS).”
Rais Dk.Samia amesema vile vile kupitia vyuo vyetu vya ufundi stadi VETA Serikali itaongeza programu maalum za mafunzo ya ufundi stadi na kuunganisha programu hizi na miradi ya mikakati kama reli ya kisasa (SGR), uendelezaji wa bandari, uchumi wa buluu, madini na gesi ili vijana hawa wapate uzoefu na waweze kuajirika.
Amesisitiza Serikali itaanzisha Kanda za Kuendeleza Ujuzi zitakazowawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika makampuni ya sekta binafsi, na kuangalia uwezekano wa kutoa vivutio maalum kwa makampuni yatakayotoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana.
Aidha, wataweka mazingira ya kuhakikisha wanakuza vijana kwenye uongozi kwa kuwezesha vyuo vyetu kufanya mafunzo ya ulezi na ukuzaji wa vijana viongozi (mentorship).
“Tutataizama mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya Halmashauri zetu ili kuboresha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa walengwa. Vile vile, ni vyema walengwa wakajua kwamba Fedha hizi ni mkopo na sio msaada, ni mbegu na sio mavuno na ni mtaji na sio ruzuku, hivyo marejesho na tija yake lazima ionekane.
“Matamanio yangu ni kuona ifikapo mwaka 2030, tuwe tumetengeneza wawekezaji vijana ambao watatoa ajira kwa vijana wenzao.
Kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo tutahamasisha ufadhili kwa biashara za wanawake…
“Ili kuwasaidia wanawake wanaofanya kazi kwenye masoko, tutaongeza na kuratibu kwa karibu Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kurasimisha biashara zao na kuwawezesha kukopesheka.”
Ameongeza Serikali itawekeza katika kuboresha miundombinu ya masoko, mifumo ya maji safi na maji taka, huduma za afya, na vituo vya matunzo ya watoto kwenye masoko.
Katika hatua nyingine, Serikali itatoa kipaumbele suala la kutenga maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ili Serikali iwatambue na kuwarasimisha ili waweze kufanya kazi zao bila bughudha na wachangie kwenye Pato la Taifa.
Rais Dk.Samia amesema kwa rasilimali ambazo nchi yetu imebarikiwa na nguvu kazi kubwa tuliyonayo, anaamini tunaweza kabisa kujipanga na kufikia lengo hilo. “Kwa kufanya hivyo, ndio tutafikia lengo letu la kuzalisha ajira milioni 8.5 katika sekta mbalimbali ifikapo mwaka 2030.”
Kuhusu huduma za kijamii, amesema maendeleo makubwa yamepatikana kwenye sekta ya maji, ambapo hali ya upatikanaji wa maji ilipanda kutoka asilimia 84 hadi asilimia 91.6 mijini, na kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 85 vijijini.
“Tumefika pazuri kuliko pale tulipokuwa mwaka 2021. Hata hivyo, azma ya Serikali ni kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa maji safi, salama na uhakika. Hivyo tunakwenda kuongeza nguvu ili kuyafikia yale maeneo machache ambayo upatikanaji wa maji bado ni changamoto.
“Katika miaka 5 ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji ambayo itategemea maji kutoka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Tutakamilisha miradi mikubwa ya maji inayoendelea ikiwemo miradi ya maji ya miji 28, na miradi mikubwa ya bwawa la Kiwira (itakayohudumia Mbeya).
“Bwawa la Kidunda, Bonde la Mto Rufiji (itakayohudumia Dar es Salaam, Lindi na Pwani), Same-Mwanga-Korogwe (itakayohudumia Kilimanjaro na Tanga), na upanuzi wa Capri Point (itakayohudumia Mwanza), kwa kuitaja kwa uchache.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...