Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassanakiwahutubia Wabunge pamoja na viongozi mbalimbali kabla ya kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma tarehe 14 Novemba, 2025.

*Pia aelezea umuhimu wa umeme nchini katika kuleta maendeleo ya Nchi

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake eneo lingine ambalo litakaloipa uzito mkubwa ni sekta ya ujenzi na kipaumbele chao kitakuwa kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambazo tayari zimeanza na zinaendelea.

Amesema Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara kupitia TANROADS, ili tufikie lengo letu la kuunganisha Wilaya zote na Makao Makuu ya Mikoa kwa kiwango cha lami.

Akizungumza leo Novemba 14,2025 alipokuwa akihutubua Bunge la Tanzania la 13 ambalo amelizindua rasmi Dk.Samia pamoja na kuelezea mikakati mbalimbali ya Serikali amezungumzia pia ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam, Serikali itaboresha barabara kuu kwa kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara katika maeneo ya Morocco, Mwenge, Magomeni na Tabata, na ujenzi wa awamu zilizobaki za miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT).

Pia wataijengea uwezo UDART ili iweze kusimamia vyema uendeshaji wa mabasi haya. Tutakamilisha pia ujenzi wa daraja muhimu, Daraja la Mto Msimbazi.

“Tutaongeza pia bajeti na uwezo wa TARURA kuboresha barabara za ndani na za vijijini ili kuhakikisha zinapitika mwaka mzima, na kuwa wakulima wanaweza kuyafikia masoko kwa urahisi.”

Kuhusu ujenzi wa makazi, amesema jitihada zao zitajielekeza kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili tuwawezeshe wananchi kujenga makazi bora huku akisisitiza kuweka mkazo maalum kwenye nyumba bora na nafuu.

“Tutasimamia utekelezaji wa sera zinazolenga kuboresha hali ya makazi kwenye maeneo yenye makazi duni. Tutashirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji kwenye miradi ya uendelezaji miji kwa kujielekeza kwenye ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

“Sambamba na hilo, tutaongeza kasi ya urasimishaji wa maeneo ya makazi, na kuimarisha utatuzi wa migogoro ya ardhi, kwa kupima ardhi nchi nzima kwa teknolojia ya kisasa ya satelaiti.

Wakati huo huo Dk.Samia akitoa hotuba yake Bungeni amesema pia hakuna maendeleo ya kiuchumi na kijamii bila nishati ya umeme wa uhakika na wenye nafuu.

Amefafanua katika kipindi kilichopita Serikali imeongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kutoka Megawati 1,600 na kufikia Megawati 4,000 na pia kufikisha miundombinu ya umeme kwenye kila kijiji.

“Tunapoelekea mwaka 2030, tumejiwekea lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme maradufu kufikia Megawati 8,000 na tutaendelea kupanua mtandao wa umeme ili kuvifikia vitongoji vyote nchini.

“Tutaongeza uzalishaji kwa kutumia vyanzo vya nishati mbalimbali ambazo nchi yetu imebarikiwa nazo ikiwemo maji, jua, gesi, joto ardhi na upepo, na hata umeme utokanao na nguvu ya nyuklia.”

Pia amesema kupitia mpango wa Gridi Imara Serikali itakamilisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme na tutaongeza vituo vya kupoza umeme ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na makazi yanapata umeme wenye nguvu inayotakiwa.

Rais Dk.Samia amesema lengo ifikapo 2030, mikoa yote ya Tanzania iwe imeunganishwa na gridi ya Taifa ya umeme.

“Ili kuihakikishia nchi usalama wa nishati ya mafuta, tutaboresha miundombinu ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari zetu na maeneo ya kimkakati.

“Tutasimamia utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia Nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, hatua itakayopunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya za watumiaji.

“Kwa upande wa gesi asilia, niwatoe hofu kuwa tupo kwenye hatua nzuri za majadiliano. Tuna dhamira ya dhati ni kukamilisha majadiliano hayo ya mradi huu mkubwa na wa kihistoria wa dola bilioni 42 wa uchimbaji wa gesi asilia.

“Kama tutakubaliana na wawekezaji, Mradi huo utabadilisha kabisa taswira na sura ya uchumi wetu. Katika majadiliano yetu tumechelewa kidogo kwa sababu tunahakikisha majadiliano hayo yanazingatia maslahi mapana ya nchi na kuhakikisha mradi huu utawanufaisha Watanzania moja kwa moja.

Vilevile, amesema Serikali itajielekeza pia kwenye kuongeza utafiti wa gesi asilia maeneo ya baharini na nchi kavu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...