*Asema wengi walifuata mkumbo Oktoba 29,atoa maelekezo kuangaliwa viwango vya makosa
*Asisitiza kama Taifa linaendelea kujifunza na kujirekebisha,aizungumzia demokrasia
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika vurugu zilizotokea Oktoba 29 mwaka huu wapo vijana wengi ambao wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini kwatojua wanachokifanya hivyo ametangaza msamaha kulingana na kiwango cha makosa yaliyofanywa ba vijana hao.
Amefafanua kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki, hivyo anatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya.
Akizungumza leo Novemba 14,2025 Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akilihutubia Bunge la Tanzania la 15 Kama ishara ya kulizindua rasmi Rais Dk.Samia amesema akiwa Mama na Mlezi wa Taifa hili, anavielekeza vyombo vya sheria na hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana hao.
“Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao. Ninatoa msamaha huo kwa sababu, hata maneno ya Mungu katika Kitabu cha LUKA sura ya 23 Mstari wa 34 yanasema, na hapa nanukuu: “Yesu akasema, Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.”
“Ndugu zangu Watanzania, tujifunze kutokana na mapito yetu, hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, ila, demokrasia kamili inaweza kutafsiriwa kwenye mitazamo tofauti (haina formula moja).
“Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha. Hivyo basi, sote kwa umoja wetu tunapaswa tuitumie fursa hii tuendelee kujifunza, tujirekebishe na tukubaliane jinsi ya kuiendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu na sio za kuletewa.”
Akieleza zaidi Rais Dk.Samia amesema kama walivyoagizwa na Ilani ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, moja ya hatua itakayotufikisha kwenye maelewano hayo ni marekebisho ya Katiba yetu.
Ameongeza kwamba Serikali imeahidi kuanza kulifanyia kazi suala la mabadiliko ya Katiba ndani ya siku mia za muhula wa pili wa Awamu ya Sita kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano.
“Tunapozungumzia umoja wa Kitaifa tunaongozwa na uwepo wa Tunu ya Muungano wetu. Hivyo basi, kuudumisha kuimarisha na kuuenzi Muungano wetu kutaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali tunayoiunda.
“Tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha tunatatua changamoto za Muungano kila zinapojitokeza.
Kuhusu Serikali ya Awamu ya sita ameliambia Bunge kwamba iliendeleza waliyoyaanza katika awamu wa tano, na hivyo kaulimbiu yake ilikuwa 'Kazi Iendelee'.
“Ninyi ni mashahidi kuwa kazi iliendelezwa na mengi yalikamilishwa, kama nilivyoeleza katika hotuba ya kufunga Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 Juni mwaka huu 2025. Niwahakikishie katika miaka mitano ijayo tutalinda na kuendeleza mafanikio haya pamoja na kuleta mafanikio mengine na makubwa zaidi.”










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...