Mkuu wa huduma za Ustawi wa Jamii jiji la Dar es Salaam, Waziri Nashiri (Katikati) akishirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben pamoja na Mwakilishi wa GIZ, Nora Loehr kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa "Sauti Zetu", uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2025.
Mkuu wa huduma za Ustawi wa Jamii jiji la Dar es Salaam, Waziri Nashiri (Katikati) akisoma kipeperushi ambacho wanawake na watoto wanatakiwa kinachotoa mwiongozo 10 ya namna ya kujilinda dhidi ya Ukatili mtandao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa "Sauti Zetu", uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2025.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limezindua mradi uitwao “Sauti Zetu” wenye lengo la kupaza sauti za wanawake na watoto pamoja na kuelimisha jamii juu ya kupambana na ukatili wa kijinsia, hususan ule unaotokea katika majukwaa ya kidijitali. Uzinduzi huu umekuja wakati dunia ikijiandaa kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10.
Akizungumza katika uzinduzi huo leo Novemba 14, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben amesema kuwa ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii limeambatana na changamoto kubwa za ukatili wa kidijitali unaowalenga zaidi wanawake na wasichana.
Ameeleza kuwa kundi hili bado halina uelewa wa kutosha juu ya kujilinda na kulinda taarifa zao mtandaoni, jambo linalochangia madhara ya kimwili na kisaikolojia.
"Licha ya juhudi za serikali, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na wadau wa maendeleo kuweka misingi ya usalama mtandaoni, bado elimu kwa jamii ni ndogo." Amesema Dkt. Rose
Pia ameeleza kuwa mifano ya vitendo vya kusambaza picha za faragha bila ridhaa, kuunda akaunti bandia, vitisho, na maudhui ya chuki kama miongoni mwa ukatili unaoongezeka nchini.
Aidha, wasichana wanaotumia majukwaa kama WhatsApp, TikTok na Snapchat wametajwa kuwa katika hatari kubwa zaidi.
Kupitia mradi huu, TAMWA imetangaza kuanza utekelezaji wa Mwongozo wa Kanuni 10 za Kujilinda na Ukatili wa Kidijitali, ambao utatumika kuongeza uelewa wa umma na kuwasaidia wanawake kujilinda dhidi ya madhila ya kimtandao. Mwongozo huo ni sehemu ya kampeni pana ya “Kupaza Sauti Ili Kupunguza Ukatili kwa Wanawake na Watoto Kupitia Vyombo vya Habari”.
Mradi wa “Sauti Zetu” unatarajiwa kutumia vyombo vya habari kama daraja muhimu kufikisha elimu kuhusu maana ya ukatili wa kijinsia, vyanzo vyake, na huduma zinazopatikana kwa waathirika.
Kupitia taarifa, vipindi, mijadala na kampeni za uelimishaji, mradi utawezesha jamii kuelewa mifumo ya kisheria, haki za waathirika na njia za kupata msaada.
Mradi unatekelezwa katika mikoa mitatu: Dar es Salaam (Kinondoni na Temeke), Dodoma (Chamwino na Bahi), na Tanga (Lushoto na Tanga Mjini).
Kwa upande wa Mwakilishi wa GIZ, Nora Loehr, akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo amesema kuwa Mradi wa Sauti Zetu una uwezo mkubwa wa kuboresha upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto kupitia matumizi ya vyombo vya habari katika kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia.
Amesema kuwa taarifa kupitia redio, televisheni, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya jamii zinaweza kuwa mwanga muhimu kwa waathirika, hasa walioko maeneo ya vijijini ambako huduma za msaada ni adimu.
Aidha, imeelezwa kuwa kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia kumeibua aina mpya za ukatili wa kijinsia unaofanyika mtandaoni, ikiwemo unyanyasaji wa kimtandao, usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa, udanganyifu wa kidijitali, na matumizi ya “deepfakes”. Wanawake, wasichana, wanafunzi, waandishi wa habari na wanaharakati wameripotiwa kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kushambuliwa kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Hali hii imefanya elimu ya usalama wa kidijitali kuwa jambo la msingi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hizo, TAMWA na washirika wake wamezindua kifurushi cha taarifa chenye mwongozo wa kanuni 10 za usalama mtandaoni kwa wanawake na watoto. Mwongozo huo umeandaliwa kwa lugha rahisi, ili kuwawezesha watumiaji kutambua hatari za mtandaoni, kulinda taarifa binafsi na kutumia majukwaa ya kidijitali kwa usalama zaidi.
Uzinduzi wa mradi wa Sauti Zetu umeambatana na wito wa kuimarisha mazingira salama mtandaoni na nje ya mtandao, ili kuhakikisha kuwa kila mmoja, hususan wanawake na wasichana, anaweza kusikilizwa na kupata haki.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza amesema amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji nguvu ya pamoja, hasa katika kipindi hiki ambacho maudhui ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yamelenga ukatili unaotokea kwenye majukwaa ya kidijitali.
Kwa ushirikiano wa wadau na nguvu ya vyombo vya habari, TAMWA inatarajia kuwa mradi huu utaongeza mwamko, kuhamasisha hatua na kuchochea jitihada za kukomesha ukatili wa kijinsia, hususan katika zama hizi za kidijitali.
Mwakilishi wa GIZ, Nora Loehr akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa "Sauti Zetu", uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2025.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...