Na Mwandishi Wetu, Morogoro.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeimarisha safu yake ya uongozi baada ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, kuwapandisha vyeo watumishi watatu walioteuliwa kuwa Makamishna Wasaidizi, kutokana na mchango wao katika kulinda na kusimamia rasilimali za misitu nchini.
Walioinuliwa ni Mathew Ntilicha, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki; Getruda Nganyagwa, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini; na Emanuel Laizer, aliyekuwa Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Watatu hao wametambuliwa kwa uadilifu, uwajibikaji na utendaji uliosaidia kupunguza vitendo vya uharibifu wa misitu katika maeneo yao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika leo Novemba 14, 2025 mjini Morogoro, Prof. Silayo aliwataka viongozi hao wapya kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni za utumishi wa umma na maadili ya taaluma, akibainisha kuwa nafasi walizopata zinahitaji uongozi thabiti na uadilifu kwa manufaa ya nchi.
“Kupandishwa cheo ni heshima, lakini pia ni wajibu mkubwa. Serikali inatarajia kuona mnatimiza majukumu yenu kwa uadilifu na uaminifu. Tunalinda rasilimali za taifa; hivyo kazi yenu ni muhimu kwa uchumi na mazingira ya nchi yetu,” alisema.
Wakati huo huo, Prof. Silayo amewataka watumishi wapya wa TFS wanaomaliza mafunzo ya awali kuwa na nidhamu, uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wanapoanza utekelezaji wa majukumu yao.
Akifunga mafunzo hayo, alisema taifa linawategemea katika kulinda rasilimali za misitu na nyuki, hivyo ni muhimu wakafanya kazi kwa weledi na bila kusukumwa.
“Watumishi hawa wanakwenda moja kwa moja kazini. Ni lazima wawe na uelewa sahihi wa sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma ili kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Prof. Silayo.
Aliongeza kuwa TFS inaendelea kuboresha mifumo yake ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ubunifu katika utendaji, huku akisisitiza kuwa watumishi wapya wanapaswa kuwa mfano wa uzalendo, uaminifu na utumishi uliotukuka.
Aidha, aliwahimiza kuongeza tija kupitia maarifa waliyojifunza ili kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya misitu na mazingira nchini.
Hafla hizo mbili zilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa TFS.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...