KIBAHA:
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, amekabidhi rasmi gari jipya kwa Divisheni ya Ardhi na Mipango Miji, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi katika utatuzi wa changamoto za ardhi.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mhe. Simon alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka kipaumbele katika utatuzi wa migogoro ya ardhi na upatikanaji wa maeneo ya viwanda na uwekezaji.
“Hili gari limeletwa ili muweze kuwafikia wananchi kwa haraka na kuhakikisha changamoto za ardhi zinatatuliwa kwa wakati. Nawaomba mlitunze na mlitumie kwa kazi iliyokusudiwa,” alisema Mhe. Simon, huku akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kutekeleza maagizo kwa ufanisi.
Awali, akiwasilisha taarifa fupi, Dkt. Shemwelekwa alibainisha kuwa gari hilo linathamani ya shilingi milioni 170, na litakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza kasi ya utoaji huduma bora hususan katika Divisheni ya Ardhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Ardhi, Denis Kahumba, amesema changamoto ya usafiri ambayo ilikua ikikwamisha utendaji sasa imepatiwa ufumbuzi.
“Ahadi yangu ni kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tunashukuru kwa vitendea kazi na mazingira mazuri ya kazi ambayo yameongeza morali kwa watumishi,” alisema Kahumba.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Rugambwa Banyikila, ametoa pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Kibaha kwa kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili ofisi ya ardhi na kuwataka watumishi kuongeza bidii na uwajibikaji.
Makabidhiano haya yanatarajiwa kuongeza kasi ya usimamizi wa ardhi, kutatua migogoro, na kuimarisha huduma kwa wananchi wa Kibaha, huku yakiendana na dira ya Serikali ya kujenga mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...