Na Pamela Mollel,Arusha
Wadau wa elimu mkoani Arusha wamepitisha mpango mkakati mpya kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu kwa mwaka wa masomo 2026.
Hatua hii imefikiwa kufuatia tathmini ya utekelezaji wa malengo ya elimu kwa mwaka 2025, tathmini iliyowezesha kubainisha mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
Kikao kazi hicho kimefanyika Desemba 1, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kikiwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka Serikali na sekta binafsi. Madhumuni yake makuu yalikuwa kuunda mpango wa pamoja utakaosaidia kukuza taaluma na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika ngazi zote.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha tathmini ya hali ya elimu mwaka 2025, Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Elimu, Mwl. Vicent Kyombo, alisema kuwa kikao hicho kimelenga kuimarisha uelewa wa pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Mwl. Kyombo, mikakati iliyoafikiwa ni pamoja na kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu ili kuhakikisha viongozi wana uwezo wa kuongoza, kubuni na kusimamia mipango ya kielimu.
Vilevile, wadau wamekubaliana kuimarisha mifumo ya motisha kwa walimu na wanafunzi, kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji, kuwezesha upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni, pamoja na kuendeleza michezo, vipaji na ukakamavu kwa wanafunzi.
Aidha, alibainisha kuwa idara ya elimu itaendelea kuimarisha mpango huu kwa njia shirikishi ili kuwahusisha wadau wote muhimu katika kupanga na kutekeleza maono ya pamoja. Hii inalenga kuinua kiwango cha taaluma na kuongeza ufaulu katika mitihani ya ndani na ile ya kitaifa.
Kaulimbiu ya kikao kazi hicho ilikuwa:
“Elimu Bora ni Msingi wa Maendeleo Endelevu — Kila Mdau Mkoa wa Arusha





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...