Na Janeth Raphael MichuziTv - Iringa


WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi nchini kuacha kufanya mambo kwa mazoea na kuaminiana pekee, hasa katika masuala ya ardhi na mali, akisema kupungua kwa uaminifu katika jamii kunachochea migogoro mikubwa ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo wilayani Kilolo mkoani Iringa wakati akihutubia wananchi katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo, ambapo amesisitiza umuhimu wa wananchi kufuata taratibu rasmi za kisheria katika umiliki, uazimishaji na makubaliano mbalimbali ya mali.

Amesema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakifanya makubaliano ya ardhi kwa mazoea bila kuyaweka kisheria, hali ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro pindi mmoja wa wahusika anapofariki dunia au kutokea sintofahamu ndani ya familia.

“Mtu anaazimisha shamba kutoka kwa familia fulani, lakini wakabaki wanaaminiana tu bila kuandika makubaliano yoyote. Sasa mwenye shamba anapofariki au aliyekodishwa akitaka kubaki na eneo hilo, migogoro inaanza. Mkifika mahakamani inakuwa vigumu kushinda kwa sababu hakuna nyaraka wala utaratibu wa kisheria uliofuatwa,” amesema Dkt. Mwigulu.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya maisha na kupungua kwa uaminifu katika baadhi ya maeneo ya jamii yanapaswa kuwa somo kwa wananchi kuona umuhimu wa kuweka kumbukumbu rasmi za kila makubaliano yanayohusu ardhi au mali nyingine muhimu.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia migogoro ya ardhi nchini kwa karibu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao pamoja na suluhisho la kudumu la migogoro hiyo.

Amesisitiza kuwa kufuata sheria na taratibu kutasaidia kupunguza kesi nyingi mahakamani, kuimarisha amani ndani ya familia na kulinda haki za pande zote zinazohusika katika umiliki wa mali.

Dkt. Mwigulu pia amewahimiza viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wataalamu wa ardhi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuandikisha mikataba na kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro inayoweza kuzuilika.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamepongeza kauli ya Waziri Mkuu wakisema changamoto za migogoro ya ardhi zimekuwa zikisababisha migawanyiko ndani ya familia na hata kuchelewesha maendeleo katika jamii.

Ziara ya Dkt. Mwigulu mkoani Iringa inaendelea ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali katika maeneo tofauti ya mkoa huo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...