Na Mwandishi Wetu, Tanga

CHAMA cha National League for Democracy (NLD), kimeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutosita kuvifuta au kuvifungia vyama vyote vya siasa vinavyokiuka sheria na kuhatarisha amani ya nchi, kikitaka wanasiasa wanaoshindwa kufuata sheria wajitoe na kuwa wanaharakati.

Wito huo umetolewa Leo mei 25 jijini Tanga na Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kisiasa nchini, kufuatia hatua ya CHADEMA kuitisha maandamano ya nchi nzima kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wao, Tundu Lissu.

Doyo alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, na kuwataka Watanzania kuacha tabia ya kulalamika na kuishutumu mamlaka hiyo kuwa inaegemea upande mmoja pale inapochukua hatua za kisheria.

"Msajili haipendelei chama chochote, kila chama kinaonywa na kuadhibiwa kadiri kinavyofanya makosa. Baada ya CHADEMA kutoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani, waliandikiwa barua ya kujieleza, lakini hata CCM nao waliandikiwa barua kufuatia kauli ya Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda, aliyesema angekuwa Rais kwa dakika moja angekifuta CHADEMA. Hii inathibitisha msajili haangalii uso wa mtu," alisema Doyo.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa vyama vyote vimesajiliwa kisheria, hivyo vinapaswa kuendesha shughuli zake ndani ya kanuni zilizowekwa na sio kujiendesha kama makundi ya harakati mitaani.

Aliongeza kuwa, pamoja na kelele na maneno mengi ya kisiasa, CHADEMA wametekeleza takwa la kisheria kwa kujibu barua ya msajili, na sasa ni jukumu la Ofisi ya Msajili kuweka wazi kwa umma kile ambacho chama hicho kimekijibu ili kuondoa sintofahamu.

"Kama kuna chama kinataka kujiendesha tofauti na sheria, wajitoe rasmi tujue ni wanaharakati. Kulinda amani ya nchi hii sio jukumu la Chama Tawala (CCM) pekee, ni jukumu letu sote wanasiasa kufanya siasa za kisheria, alieleza.

Doyo alirejea kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya ya kuleta umoja na utulivu kupitia falsafa yake ya maridhiano, ambayo imetoa uwanja mpana kwa vyama vyote kufanya siasa za kistaarabu.

Akizungumzia ziara yake mkoani Tanga, Doyo alisema mara ya mwisho kufika mkoani hapa ilikuwa ni wakati wa kuzindua kampeni za Urais mwaka 2025, na sasa amerejea maeneo hayo kwa ajili ya kuimarisha na kukisuka chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa NLD unaotarajiwa kufanyika mwakani (2027).




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...