Na Karama Kenyunko - Michuzi Tv

Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya Uhujumu Uchumi, wakidaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh milioni 120.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutekeleza makosa hayo katika mipaka ya Sirari mkoani Mara, Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, kwa lengo la kujipatia vibali vya muda vya matumizi ya magari yaliyokuwa yamesajiliwa kwa namba za Afrika Kusini.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani na Wakili wa Serikali, Godfrey Nugu akisaidiana na Rozalia Rutagwerela, washtakiwa hao wametajwa kuwa ni George Kaiza (35), Hosiana Sanga (31) na Hamu Sanga (26).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila, upande wa mashtaka ulidai kuwa katika kesi namba 11588/2026 inayomkabili George Kaiza pekee, mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka saba.

Inadaiwa kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa TRA ili kuingiza nchini gari aina ya Toyota Fortuner lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kupata kibali cha muda.

Aidha, Februari 25, 2026 katika mpaka wa Sirari mkoani Mara, Kaiza anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa TRA wakati akiingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kujipatia kibali cha muda kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka ulidai pia kuwa Kaiza aliuza magari hayo kinyume cha sheria huku akijua kuwa yalikuwa yamepewa vibali vya muda na TRA.

Wakili Nugu alidai kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alikwepa kwa makusudi kulipa ushuru wa zaidi ya Sh milioni 84 kwa magari mawili ambayo ni Toyota Fortuner na Ford Ranger yaliyokuwa na namba za usajili za Afrika Kusini, jambo ambalo alifahamu kuwa ni kinyume na sheria.

Hata hivyo, Kaiza hakutakiwa kujibu chochote mahakamani kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi. Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kwa upande wa washtakiwa Hosiana na Hamu, wanadaiwa kuwa Januari 25, 2026 katika eneo la Tunduma mkoani Songwe walitoa taarifa za uongo ili kujipatia kibali cha muda na kuingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini.

Inadaiwa kuwa kwa kufanya hivyo, waliisababishia TRA hasara ya Sh milioni 35.5 kutokana na kukwepa kulipa ushuru wa uingizaji wa gari hilo huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Licha ya dhamana kuwa wazi, hadi wakati Michuzi Blog inaondoka mahakamani, washtakiwa wote walikuwa bado wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, kuweka fedha taslimu sawa na nusu ya kiasi cha hasara kinachodaiwa kusababishwa au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...