Na. Damian Kunambi, Njombe

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva akiambatana na Mkurugenzi wa Halamashauri, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wilayani humo wamefanya Dua/Kisomo Maalum cha kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili azidi kupata kheri, hekmana baraka.

Akizungumza mara baada ya kufanyika kisomo hicho katika msikiti wa Wilaya ya Ludewa mkuu huyo wa wilaya amesema Rais Dkt. Samia amekuwa ni kiongozi anaye liongoza vyema Taifa la Tanzania hivyo anapopata baraka taifa zima linapata baraka pia kupitia yeye.

"Rais wetu amekuwa ni kiongozi bora na mwenye hekma, hivyo hatuna budi kumwombea kwa Mungu ili aweze kuendeleza ubora alio nao na kile ambacho Mungu amekiweka ndani yake".

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo Sunday Deogratius amempongeza mkuu huyo wa Wilaya kwa kuandaa kisomo hicho kilicho ambatana na futari na kuongeza kuwa Rais Dkt. Samia amefanya maendeleo makubwa katika halmashauri mbalimbali ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ambayo imepiga hatua kwenye maendeleo ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na sekta nyinginezo.

Aidha kwa upande wake shekhe wa Wilaya hiyo Haruna Rahim amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kuwaunganisha katika kufanya kisomo hicho pamoja na kupata futari kwani kwa kufanya hivyo kunaongeza Swawabu kutoka kwa mwenyezi Mungu na hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.

Kisomo hicho cha kumwombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiliambatana na Iftari iliyo andaliwa na mkuu huyo wa Wilaya Victoria Mwanziva katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambapo waumini wote wa kiislamu na wageni waalikwa walijuika pamoja kupata ftari hiyo.

Sanjari na kisomo hicho na futari lakini pia mkuu huyo wa Wilaya alimkabidhi Shekhe Haruna zawadi ya pikipiki aina ya King lion 150 yenye thamani ya shilingi 2,600,000 milion ili iweze kumsaidia katika mizunguko yake mbalimbali huku mbunge wa jimbo la Ludewa akitoa hundi ya shilingi 1,000,000 kwaajili ya ujenzi wa msikiti.








Na Janeth Raphael -MichuziTv Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka waganga wafawidhi nchini na Watumishi ndani ya Sekta ya Afya kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya.

Pia amesema sekta binafsi imesaidia kwa kiwango kikubwa kuipunguzia Serikali mzigo hasa upande wa ajira kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia sekta binafsi, hali ambayo sio rahisi kuiachia mzigo serikali pekee.

Dtk. Mollel ameyasema hayo Machi 27,2024 wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki na kuchangia mada zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo.

Dkt. Mollel amewaasa Wakurugenzi wa OR- TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuhakikisha vinapata vituo hivyo mapema iwezekanavyo.

“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mambo mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja, nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati”, amesema Mollel na kuongeza .

“Tunataka tutakapokutana tena katika mkutano wa mwaka 2026 tutazungumza masula mengine kama kuajiri watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuongezwa” amesisitiza Mollel.

Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.

“Sekta ya Afya ni moja na kazi nyingi za afya zinaanzia katika ngazi ya msingi na dada yangu Dkt. Grace amesisitiza hapa hakuna huduma za afya bila msingi kwani huduma zote zinaanzia huko kwa wananchi walio wengi ndipo wanaanzia kabla ya kuja huku juu kupatiwa huduma,” amesema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Grace Magembe amesema, ili kufanikiwa katika sekta ya Afya ni lazima kuboresha sekta kuanzia ngazi ya msingi na ustawi wa Jamii

"Hakuna Afya, bila kuhakikisha tunaboresha eneo la Afya ya Msingi na ustawi wa Jamii lipo sawa, mafaniko yetu tutaweza kujipima vizuri endapo tutatoa kipaumbele katika eneo la afya ya msingi," ameeleza Dkt. Magembe

Akitoa salaam za Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela, amesema kuwa kupitia mkutano huo mapendekezo kadhaa yameweza kutolewa kupitia majadiliano yaliyofanyika ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa huduma za afya ya msingi.

“Mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti za afya za mifumo ya bima na jambo hili limesisitizwa kwa ukubwa na wakashauri vyanzo mbalimbali viweze kutumika ikiwemo kuwashirikisha wadau kama Wizara ya Fedha,”amesema.

Amesema pendekezo lingine lililotolewa ni kwa wadau pamoja na Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ya msingi, rasilimali watu na vifaa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora.




-Dkt. Kijaji: Watanzania tumieni fursa kupeleka bidhaa Uingereza.

Serikali imewashauri watanzania kutumia fursa ya mpango wa biashara wa Nchi zinazoendelea kwa kuhakikisha wanapeleka bidhaa katika nchi ya Uingereza ili kukuza Uchumi pamoja na pato la Taifa.

Mpango huo mpya umeanza kutumika mwaka jana 2023 ambapo Serikali ya Uingereza iko tayari kupokea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini zikiwemo zenye kulipiwa ushuru na zisizolipiwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo leo Dar es Salaam katika semina ya wafanyabiashara kuhusu fursa ya kuuza bidhaa katika soko la Uingereza na Nchi zinazoendelea (UK- DCTS).

Akizungumza Mhe.Dkt. Kijaji amesema mpango huo wa bishara na Nchi zinazoendelea kwa Tanzania umekuja muda muafaka kwa kuwa Nchi imerekebisha na kuboresha mazingira ya biashara ili kufanya kukuza kipato na biashara nchini.

Amesema kwa mwaka 2022 mauzo ya Tanzania kwenda Uingereza yalifikia sh. bil 44 ikilinganishwa na manunuzi ya sh. trilioni 3.08 ya bidhaa kutoka Uingereza.

Amesema kupitia takwimu hizo ongezeko la mauzo kwenda Uingereza ni ndogo sana ikilinganishwa na ununuzi wa bidhaa kutoka Uingereza Kwenda Tanzania kwani kwa miaka miwili imeongezeka sh. bilioni mbili wakati bidhaa zilizonunuliwa ni zenye thamani ya sh. triloni 1.06.

“Inahitaji nguvu ili kuweza kuvuka na kufikia malengo halisi ya kuanzishwa kwa mpango huo,” amesema Waziri Kijaji.

Aidha, ametolea mfano taarifa ya Kituo cha Uwekezaji nchini ( TIC) kuanzia mwaka 1997-2024 jumla ya miradi 980 ya kampuni ya Uingereza yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5655.38 zilizotoa ajira za wastani wa watu 126,322 katika sekta mbalimbali ziliwekezwa nchini.

“ Tuweze kutumia mpango huo na kuchochea mapato pamoja na fedha za kigeni, lakini pia kupitia mpango huo Taifa litakuwa na manufaa mbalimbali ambayo ni kupungua kwa masharti ya kupeleka bidhaa na kwa wenye viwanda ni muhimu kuwa na malighafi zitakazochochea ushindani wa bidhaa za Tanzania,” amesema.

Ameongeza pia manufaa ya mpango huo ni kupungua kwa gharama za kufanya biashara kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa Tanzania na hata kushirikiana na kampuni za Uingereza kuwekeza na kuzalisha bidhaa bora Tanzania.

Amehamasisha wafanyabiashara kuona umuhimu wa uadilifu katika kuziona fursa na kwamba wapeleke bidhaa zinazokidhi soko hilo.

“Serikali yetu ya awamu ya sita imechukua hatua nyingi za kujenga mahusiano ya kidipolomasia na Uingereza ambapo Nchi hiyo pia ilianza kutoa fedha kupitia huduma mbalimbali ambazo zimeelekezwa katika Miradi mbalimbali,” amesema.

Mhe. Dkt.Kijaji ameongeza kuwa mpango huo umezingatia pia sekta ya biashara kwa kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika ukuaji wa viwanda.

Akitoa ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania David Cancar amesema chini ya mpango huo Tanzania ndio yenye bidhaa zinazotakiwa na Uingereza.

Amesema kupitia mpango huo kwa Pamoja kutakuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya Tanzania na Uingereza.








Na Janeth Raphael -MichuziTv Dodoma

Watanzania wote waalikwa katika ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 Hayati Edward Moringe Sokoine,aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayofanyika Monduli juu mkoani Arusha Aprili 12,2024.

Taarifa hiyo imetolewa mapema leo hii Jijini Dodoma na Msemaji wa familia ya Hayati Sokoine Bwana Lembus Kipuyo alipokuwa akiongea na wanahabari, na kuongeza kuwa kumbukizi hii imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya hayat Edward Moringe Sokoine.

"Nawaalika watanzania wote kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayofanyika Ijumaa Aprili 12, 2024, katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha".

"Ibada hiyo itakayofanyika siku ya Ijumaa Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi, imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine".

Aidha Bwana Kipuyo amesema Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt Samia Suluhu Hassan atawaongoza viongozi mbalimbali wa serikali katika kumbukizi hii.

"Ibada hiyo ya kumbukumbu ya Hayati Sokoine itawashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan".

Pia amezungumzia malengo ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ya ya Hayati Edward Moringe Sokoine kuwa ni kuenzi mema aliyoyafanya katika Utumishi na enzi za uhai wake.

"Lengo kubwa la kuanzishwa kwa Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine, ni kuenzi mema aliyoyafanya, kwani aliacha alama kubwa ambayo taifa linamkumbuka hadi leo".

"Taasisi hiyo imejikita katika masuala ya elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, vyanzo vya maji pamoja na afya".

Sambamba na hayo yote hakuacha kuelezea uzalendo uliokuwa nao Hayati Edward Moringe Sokoine kwa taifa na wananchi kwa ujumla.

"Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake".

"Hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza. Alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha".



Shirika la Viwango Tanzania ( TBS ) , Leo Machi 28, 2024 limeadhimisha siku ya viwango Afrika na kutoa vyeti na zawadi kwa Washindi 10 Bora wa Mashindano ya Insha ambapo Washindi wa nafasi tatu za Mwanzo (waliopewa Zawadi za Fedha Taslimu) watashiriki Mashindano ya Insha Afrika.

Akizungumza katika Hafla iyo iliyofanyika makao makuu ya TBS Jijini Dar Es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hassan Bomboko ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert Chalamila , amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania kwa kazi na Jitihada kubwa za kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na Bidhaa zilizo Bora hasa katika kipindi hiki cha Miaka Mitatu ya Serikali ya awamu ya SITA inayooongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

" Niwapongeze TBS kwa kuadhimisha siku hii muhimu kwa namna ya Kitofauti lakini pia niwapongeze washiriki wote zaidi ya 300 waliojitokeza kushiriki mashindano ya Insha hadi sasa tumewapata 10 bora , nyinyi kama wataalamu wetu wa badae wa masuala ya Viwango mmefanya jambo kubwa sana , Juzi wakati tukiadhimisha miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan TBS ni moja kati ya Mashirika yaliyofanya vizuri niwapongezeni sana " alisema Mhe. Bomboko

Akitoa Historia ya Siku ya Viwango Afrika , Mkurugenzi Mkuu TBS , Dkt. Athuman Ngenya amesema
" Shirika la Viwango Afrika lilianzishwa mwaka 1977 likiwa na jukumu kuu la Kuoanisha viwango Afrika ili kukuza biashara na kupunguza vikwazo vya Kibiashara barani Afrika pamoja na kuimarisha ukuaji wa Viwanda Afrika .





Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
ASKARI wawili wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji wamejeruhiwa wakiwa katika harakati za kuokoa marehemu waliokuwa wamenasia kwenye gari baada ya kuzuka moto ghafla na magari kuwaka moto .

Hayo yamesemwa leo Machi 28 na Kamanda wa Polisi Mkoa Mkoa wa Pwani (SACP) Pius Lutumo alipozungumza na Waandishiwa Habari.

RPC Lutumo amewataja askari waliojeruhiwa kuwa ni Koplo Elias Bwire na Koplo Hamisi Kungwi wote wamekimbizwa Hospitali ya Taifa Mloganzila kwa matibabu na hali zao zinzendelea vizuri.

" Machi 28 mwaka huu majira ya saa 10:15 alfajiri katika bonde la Ruvu Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani barabara ya Morogoro, Dar es Salaam gari namba T668 DTF aina ya Scania Kampuni ya Sauli ikiendeshwa na dereva Idd Aloyce (35),mkazi wa Mafinga ikitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta ya Petroli lenye namba za usajiri RAF672N na tela lenye namban RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda likiendeshwa na dereva Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake".

Aidha basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer Kampuni ya New Force lenye namba za usajiri RAF672N na likiendeshwa na dereva aitwaye Burton Jacob (33),.mkazi wa Mbeya ambapo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Saul lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wawili ambao hawakufahamika majina yao na majeruhi watatu ambao ni Salimu Daud (50) mkazi wa Mbozi Mbeya, Farida Idrisa (26)mkazi wa Tabata Dar es Salaam na Kiambile Geofrey mkazi wa Uyole Mbeya.

RPC Lutumo chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine huku yakiwa yamefatana.

"Pamoja na hayo uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Saul iliyokua imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kuripua petroli wakati wa uokoaji"amesema RPC Lutumo.

"Wito wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani unawataka madereva kutii sheria za Usalama Barabarani kwa mujibu wa taaluma zao na ifahamike kwamba madereva wanachukua dhamana kubwa ya maisha na mali za watu"

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema atayafungia mabasi yatakayoendelea kuvunja Sheria za Usalama Barabarani baada ya ajali iliyotokea alfajiri ya leo.

RC Kunenge amesema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Kibaha Mkoani Pwani, amesema yeye ameamua kwa kushirikiana na wanaotoa lesseni, LATRA na Jeshi la Polisi kuwa wataweka mkakati wa kudhibiti ajali ndani ya Mkoa wa Pwani.

" Mtagundua kuwa Mkoa wa Pwani hii Barabara ni kubwa na mabasi yakitoka kule stendi kuu ya Dar es salaam Mbezi idadi ya mabasi ni mengi yakiwa yamekaguliwa lakini bado hapa pia tunakagua " amesema.















Kocha Mkuu wa Timu ya Tabora United Denis Laurence amesema kuwa katika kipindi cha siku saba tangu alipojiunga na timu anaridhishwa na viwango vya wachezaji kutokana na kujituma kwao kwenye mazoezi uwanjani.

Kocha Laurence amesema kuwa ameshangwaza kuona wachezaji kwa kipindi kifupi tangu alipojiunga na Timu hiyo yenye Makazi yake Mkoani Tabora wanamuonesha ushirikiano wakutosha nakusikiliza kila anachowaelekeza kwenye uwanja wa mazoezi na kwamba hajapata changamoto yoyote hadi sasa.

Ameongeza kuwa ushirikiano ambao wachezaji wanampa unatoa  taswira njema kuelekea kwenye michezo tisa ya Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Azam Sport Federation dhidi ya Singida Fountain Gate kufanya vizuri kwani ndio mkakati uliopo kwa sasa kama Timu.

“Nafurahi kuona wachezaji wananisikiliza vizuri, tunakwenda sawa ,tunazungumza Lugha moja , kwa huumuda mfupi ambao nimekuwa nao hapa kwangu ni maajabu, wanafuata ninachowaambia lakini pia wanafanyia kazi, hii kwangu ni kubwa sana kama kocha, muhimu nazidi kuwasisitiza kila mmoja ananafasi kwenye kikosi changu cha kwanza” amesema Kocha Laurence.

Ukiangalia kila mmoja anauwezo mkubwa, nahii ni kawaida kwa wachezaji wa  Afrika, muhimu ninachokifanya ni kuwaweka kwa pamoja wacheze kitimu ili tuweze kushinda, morali na hari zao zipo juu hivyo ninafurahia sana kuwepo na wachezaji wangu mazoezini na mazingira yote kwa ujumla.

Aidha katika hatua nyingine Kocha Laurence amesema kuwa hadi sasa tayari ameshapata kikosi chake cha kwanza lakini akasisitiza sio ndio kitadumu milele hapana kwani mfumo wake ni kuhitaji kila mmoja aweze kucheza kweye michezo hii iliyosalia kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2023/2024.

Tabora United itakuwa ugenini siku ya Aprili Nne katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ikiwakabili Singida Fountain Gate kwenye mchezo wa ASFC na badae Aprili 14 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi hapa Mjini Tabora.

Imetolewa leo Machi 28

Na Christina Mwagala

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano

Tabora United


Na MWANDISHI WETU


WAWEKEZAJI kutoka China wamekutana na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kujadiliana kuhusu uwekezaji hususan katika uzalishaji wa Nishati safi ya kupikia kwa lengo la kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati ya kupikia.

Wawekezaji hao waliongozwa na Shen Don kutoka Jimbo la Shangzhou ambapo wakiwa nchini wlikutana na wadau mbalimbali kutazama fursa za uwekezaji.

Kundi hilo la wawekezaji wameridhia kufanya uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani milioni 312 (zaidi ya sh. bilioni 800) katika maeneo ya nishati, afya, ujenzi, kilimo na vifaa vya uchakataji viwandani

Kutokana na hatua hiyo, UWT inaamini hiyo itakuwa fursa nzuri kwao kuwafikia na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lumumba jijini Das res Salaam, jana, Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo alisema wawekezaji hao ambao ujio wao umeratibiwa na Kampuni Canopus Energy Solution, wameonyesha utayari wa kushirikiana katika eneo la uzalishaji wa Nishati mbadala na maeneo mengine ya kimkakati.

“Chama Cha Mapinduzi kinachoongozwa na Mwenyekiti wetu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kilizielekeza jumuiya zote Chama kutazama na kujiendeleza kupitia fursa mbalimbali, hii kwetu ni fursa tumejipanga kuzalisha nishati mbadala kupitia makaa yam awe.

“Wenzetu hawa wameonyesha utayari, tumefanya mazungumzo ya awali na wametualika kwenda China katika maeneo yao ya uzalishaji wa huduma na bidhaa mbalimbali kujionea namna walivyo tayari kutokana na maendeleo ya teknolojia,” alisema.

Alieleza kuwa UWT ina dhamana kubwa ya kuwaendeleza wanawake wa Tanzania kupitia fursa mbalimbali, hivyo imejipanga kuunga mkono juhudi za kumtua mama kuni kichwani kwa kutengeneza mkaa mbadala ambao ni salama kwa afya za binadamu.Kwa mujibu wa Jokate mbali na nishati mbadala, pia wanatazama uwezekano wa wa kushirikiana na wadau hao katika sekta ya madini lakini hilo litafanyika baada ya hatua mbalimbali kutekelezwa ili kuwa na ushirikiano wenye tija.

Jokate alisisitiza kwamba UWT imejipanga kutengeneza fursa ambazo zitawanufaisha wanawake katika sekta mbalimbali hususan uchumi ambao utawainua na kimaisha.

"Fursa yoyote tunayoitengeneza lengo letu ni kuona wanufaika wa kwanza wanakuwa wanawake wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake Mhandisi Anna Nyangasi kutoka Kampuni ya Canopus Energy Solution, alisema ujio wa ujumbe huo ni fursa kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Anna alieleza kuwa wawekezaji hao waliongozwa na Shen Don kutoka Jimbo la Shangzhou ambapo ukiwa nchini ulikutana na wadau mbalimbali kabla ya jana kukamilisha ziara yao kwa kukutana na UWT ambapo wanaamini kuna kundi kubwa la wanawake ambalo linahitaji kuwa sehemu ya mabadiliko kutokana na uwekezaji unaoweza kufanywa na wawekezaji hao.

Kwa mujibu wa Anna, wawekezaji hao wameridhia kufanya uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani milioni 312 (zaidi ya sh. bilioni 800) katika maeneo ya nishati, afya, ujenzi, kilimo na vifaa vya uchakataji.

Pia, alisema ujumbe huo umeonesha nia kushirikiana na kutafuta wawekezaji katika maeneo takribani manane ambayo ni viwanda vya kuunganisha zana za kilimo (pawatila), kuzalisha vifaa vya trekta, majenereta, pampu za maji, vifaa tiba, viwanda vya bidhaa za umeme na ‘paneli’ za kuhifadhi baridi.

Mhandisi Anna alisema ujumbe huo wa watu 11 unahusisha wafanyabiashara, wawakilishi kutoka serikalini pamoja na ujumbe wa CCP, uliwasili nchini kwa mwaliko wa Canopus Energy Solution kwa kushirikiana na Kampuni ya Amec Group.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Jokate Mwegelo (kushoto) akisalimiana na ujumbe wa wafanyabiashara  kutoka China waliongozwa na Shen Don kutoka Jimbo la Shangzhou (wa pili kulia) baada ya kufika katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi(CCM) zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam








Top News