Na Mean Wetu,Dodoma

MADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya elimu ya usalama barabarani yalivyo wafumbua macho na kuwafanya kufahamu sheria mbalimbali za barabarani na hivyo kuendelea na kazi yao wakiwa salama.

Wamesema hayo mbele ya waandishi wa habari waliokuwa wametembelea kijiwe cha bodaboda cha Kijiwe Pesa ambapo baadhi ya bodaboda walikuwa wakifanya tathimini kuhusu mafunzo waliyopata kutoka Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi ambao wameendelea kufanikisha kutolewa kwa mafunzo hayo.

Madereva hao bodaboda katika kijiwe hicho wamesema awali hawakuwa wakifahamu vema sheria za usalama barabarani hasa taa zinazoongoza magari na jinsi ya kupita kwenye makutano ya barabara ilikuwa ni kitendawili kwao.

"Kupitia mafunzo ya usalama barabarani ambayo tumeyapata kutoka kwa wenzetu wa Amend kwa kushirikiana na wadau wengine kama Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani sasa tunafahamu vema sheria za usalama barabarani pamoja na alama zilizopo,"amesema dereva bodaboda Jonathan Chidawi

Kwa upande wake Amiri Matimba ambaye ni Msaidizi wa Miradi kutoka Shirika la Amend Tanzania anasema wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa madereva bodaboda 47 kwa wiki ya kwanza jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa wanaendelea kutembea katika vijiwe mbalimbali vya bodaboda kwa ajili ya kuhamasisha maofisa hao kusafirishaji(bodaboda)kujiunga katika mafunzo hayo yanayotolewa bila gharama yoyote.

Wakati huo huo Mkufunzi wa Mafunzo hayo ambae pia ni Katibu wa Chama cha Walimu wa madereva Tanzania (CHAWATA) Massava Ponera akieleza tathimi ya mafunzo hayo toka walipoanza hadi walipofikia amesema mafunzo yanaendelea na madereva wengi wamefikiwa na mafunzo hayo.

Amefafanua kwa Dodoma hiyo ni awamu ya pili kutolewa kwa mafunzo hayo ambayo yamedhaminiwa na ubalozi wa Uswisi ili kuwezesha elimu ya usalama barabarani inafika kwa kundi la bodaboda ambalo jamii siku zote hulitazama kwa jicho la tofauti na kuamini ni wavunjaji wa sheria wakubwa.









JITIHADA za Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu kwa kushirikiana na wanachi zimesaidia kukamilisha kazi ya upauaji wa madarasa mawili katika Shule Shikizi ya Mwitumi hatua itakayoondoa changamoto ya watoto kusafiri umbali wa kilomita 9 na kuvuka mito miwili kufuata shule mama ya Msingi Nkundi.

Katika jitihada hizo wananchi walitumia nguvu yao kujenga hadi usawa wa Lenta na mbunge akawaunga mkono kwa kutoa Sh Milioni 13 ambazo zilinunua Bati 110, mbao zote na Saruji ya kupiga lipu na Sakafu.

Akizungumza na kituo hiki April 24,2024,Mtaturu amesema kukosekana kwa madarasa hayo kumesababisha utoro wa wanafunzi wakati wa masika na hivyo kushusha kiwango cha ufaulu.

Amewashukuru wananchi wa Kitongoji cha Mwitumi, Kijiji cha Nkundi Kata ya Kikio kwa Ushirikiano mkubwa walioutoa wa kushirikiana nae na kumaliza shughuli ya ujenzi wa Darasa

"Hatimaye imewezekana kwa kushirikiana na wananchi tumepaua vyumba viwili vya madarasa katika kuhakikisha changamoto ya watoto wanaosafiri mwendo mrefu na kuvuka mito miwili kufuata shule mama ya Msingi Nkundi inaisha,nawashukuru sana wananchi kwa jitihada zenu,".ameshukuru.

#VitendoVinasautiKulikoManeno#SingidaMashariki#TunaendeleaKuwafikia#

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewashauri wenye visima vya maji kuhakikisha maji yanapimwa ili kukidhi ubora na kulinda usalama wa afya zao.

Hayo yamebainishwa Leo Aprili 24,2024 na Afisa udhibiti Ubora (TBS) Bw.Ibrahim Feruzi  wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za TBS, Jijini Dar es Salaam.

Amesema wananchi wamekuwa na desturi ya kujitafutia vyanzo vya maji kutokana na uchache wa vyanzo vya maji salama ili kujipatia suluhisho endelevu ambapo changamoto inayojitokeza ni kutokuwa na uhakika wa ubora na usalama wa maji hayo.

Aidha Bw.Feruzi amesema kuwa TBS kupitia maabara zake inapima maji katika maeneo mawili ambayo ni Mikrobiolojia pamoja na kemikali ambapo maabara hizo zina ithibati hivyo majibu yake yanakubalika popote duniani.

Pamoja na hayo ameeleza umuhimu wa  wananchi kufahamu usalama na ubora wa maji  ili kuepuka maambukizi ya vimelea hatarishi.

"Kuna vimelea hatarishi kama aina mbalimbali za bakteria kama vile salmonella wanaosababisha ugonjwa wa typhoid ambao wengi mnaufahamu, kuna wadudu wanaitwa Vibrio wanaosababisha ugonjwa wa kipindupindu na wadudu wengine wanaoitwa shigella ambao wanasababisha matumbo ya kuhara, uwepo wa wadudu hao unatupatia kila sababu ya kuhakikisha maji yanapimwa na kutibiwa ili kuwa salama"Bw.Feruzi ameeleza.

Vilevile Bw.Feruzi  amesema kupimwa kwa maji kunajumuisha vigezo mbalimbali kama kuangalia kiwango cha Oksijeni,kiwango cha tope,tindikali ya madini mbalimbali hasa metali nzito ambapo inasaidia  kufanya tathmini ya ubora na usalama wa maji.

"Viwango vya juu vya metali nzito mfano zebaki (Mercury) vinaweza kusababisha athari kubwa za kiafya kama kansa za ngozi,matatizo ya figo,matatizo ya maini na mengineyo"Bw.Feruzi amesema.

Bw.Feruzi amebainisha kuwa Shughuli za kibinadamu katika rasilimali maji zinanaweza kuchangia uchafuzi wa maji ambayo awali yalikuwa salama hivyo ni vema kufanya upimaji mara kwa mara ili kubaini  mapema aina ya uchafuzi na kuitatua mapema ili kulinda mifumo ya ikolojia.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Masoko , Bi. Gladness Kaseka amesema upimaji wa maji ya kisima kwa matumizi binafsi ni wa hiari ila  kwa wale wanaotaka kusambaza kwa ajili ya matumizi ya watu wengi upimaji ni wa lazima ili kulinda afya za watumiaji.

Kaseka ametoa rai kwa wenye visima binafsi na wale wanaosambaza maji kupima  kama biashara kuwa na tamaduni za kupima kujihakikisha usalama na ubora wa maji husika ili kuepuka changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kwa watumiaji, na muda wa upimaji hadi kupata majibu ni siku 14.


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewataka wazazi na walezi pindi wanapoona mvua kubwa zinanyesha kutowaruhusu watoto kwenda shule ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza kutoka na mafuriko na kuharibika kwa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa leo Aprili 24,2024 jijini Dar es salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Wizara baada ya kuharibika kwa miundombinu ya shule.

Amesema  walimu wakuu wanapaswa kuchukua hatua za haraka na kutoa maamuzi pindi wanapoona hali mbaya ya hali ya hewa aidha kwa kuwaruhusu watoto mapema na kufunga shule lakini pia kwa kuwasiliana na wazazi.

Aidha amesema endapo shule zimefungwa kutokana na mafuriko na familia zimehama hivyo kule wanapohamia watoto wanapaswa kupelekwa kwenye shule zilizokaribu ili kuendelea na masomo yao.

"Kama shule zimefungwa na maji yamejaa na familia zimehama kule wanapokwenda wapokelewe wakati maafisa elimu kata wakiwa wanashughulikia taratibu nyingine ikiwa kama mtoto ataendelea kwenye shule hiyo au atakuwepo kwa muda na shule yake ikakarabatiwa anarudi",Amesema.

Prof. Mkenda amesema kuwa Wizara inashirikiana na wazazi ambao watoto wao wanasoma kwenye shule binafsi kuhakikisha wanapata shule ambazo watazichagua wao kwa maelewano yao ili kuwapeleka watoto.

Sambamba na hayo ametoa onyo kwa madereva wa magari ya shule kutopitisha magar hayo kwenye mabwawa ya maji au sehemu yenye maji mengi ili kuepuka kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

"Kitu cha kwanza katika shule zetu ni usalama wa watoto wetu na usalama wa wafanyakazi katika taasisi zetu madereva kama wakiona dalili zozote za hatari waache wasije wakaingiza watoto wetu kwenye hatari",

Aidha ameongeza kuwa kamishna wa elimu atoatoa mongozo na kuruhusu mabadiliko katika kalenda ya ufundishaji ili kusaidia kwenye swala la mvua watoto wasiumie. 

Amezipongeza shule binafsi ambazo walipooana hali ya hewa mbaya wakaamua kusitisha kwa muda masomo kwenye shule zao ili kupisha hali hiyo.

Akizungumzia miundombinu iliyoharibika amesema serikali kupitia wizara wamesema wanafuatilia taarifa za hali ya hewa ili waweze kuirejesha miundombinu hiyo ambapo shule ambazo zilizokuwa mabondeni wataangali sehemu salama na kuzijenga.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Wizara baada ya kuharibika kwa miundombinu ya shule. Amezungumza leo Aprili 24,2024 katika Ofisi za Wizara jijini Dar es salaam 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Wizara baada ya kuharibika kwa miundombinu ya shule. Amezungumza leo Aprili 24,2024 katika Ofisi za Wizara jijini Dar es salaam 




Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Wizara baada ya kuharibika kwa miundombinu ya shule. Amezungumza leo Aprili 24,2024 katika Ofisi za Wizara jijini Dar es salaam 

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

 WANACHAMA wa Kishindo cha Mama kwa kushirikiana na TOGABE Mills watoa Msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Wametoa misaada mbalimbali ya kibinadamu vikiwemo Unga, Maharage, Mchele, Mafuta ya Kupikia pamoja na nguo.
MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele (Watano kutoka kushoto) Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiwa katika picha ya pamoja wakiwa na vyakula vilivyotolewa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Baadhi ya wanakibiti wakisaidia kushusha baadhi ya misaada iliyotolewa na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills mara baada ya kutolewa walipotembelewa na wanachama hao.
MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiondoka na vyakula vilivyotolewa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.



MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele (Wapili kutoka kushoto) akizungumza na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills mara baada ya kukabidhi msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele akiwa na Tisheti aliyopewa na wanachama wa Kishindo Cha Mama.
Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kutoa Msaada kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Picha ya pamoja.

MKuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa misaada na Wanachama wa Kishindo cha Mama na TOGABE Mills vilivyo kwa waathirika wa Mafuriko Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Afisa Masoko wa TOGABE Mills, Ramadhan Kimomwe akizungumza na waandishi mara baada ya kutoa msaada kwa waathirika wa Mafuriki Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

*Wakumbushwa kutekeleza majukumu yao bila kuathiri afya zao

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Taasisi zake kwa kujisimamia vyema katika utekelezaji wa majukumu kwa kufuata miongozo ya Serikali na kuwataka kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miiko ya utumishi wa Umma pamoja na kujali usalama wa afya zao kwa kufanya mazoezi, kupata lishe bora pamoja na kupima afya zao.

Akizungumza Leo jijini Dar es Salam wakati akifungua Mkutano wa 37 wa mwaka 2023/2024 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amesema katika kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa Fedha ni lazima kazi zifanywe kwa ubunifu na ushirikiano wa Wizara, idara, vitengo na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo nyeti na muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Nchi.

“Niwapongeze kwa utendaji kazi wa Wizara ya Fedha na taasisi zake kupitia Government Structure inavyotekeleza majukumu yake sipati malalamiko ya moja kwa moja kuhusu Wizara yetu, Nawapongeza wakuu wa Taasisi na bodi za wakurugenzi na wafanyakazi kwa kujiendesha vyema chini ya bodi…..Wizara ya Fedha tupo vizuri taasisi zinajisimamia vizuri sana.” Amefafanua.

Amesema baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu la majadiliano mahali pa kazi lililoundwa kwa mujibu wa Sheria na kuipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria la kuunda baraza la wafanyakazi ili kutoa fursa ya majadiliano ya masuala ya ajira na mazingira ya kazi baina ya mwajiri na mwajiriwa.

“Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu cha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi muhimu yanayohusu uendeshaji na utendaji wa Wizara…..Nasisitiza na kuelekeza kuwa ni lazima tuzingatie matakwa ya kisheria ya kufanya mkutano wa baraza la wafanyakazi na nipate taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya baraza kila tunapofanya mkutano kwa kuwa kupitia mikutano hii tukiwa taasisi nyeti tunapata fursa ya kuzungumza na kupanga mikakati bora ya kutoa huduma kwa wananchi na wadau wetu.” Amesema.

Aidha amesema kuwa, Hoja zitakazojadiliwa katika mkutano huo zilenge kuboresha mazingira ya kazi, mifumo ya usimamizi na mipango wa Wizara na huduma kwa wadau wa ndani na nje.

“Katika kupiga hatua zaidi niwahakikishie kuwa Ofisi yangu ipo wazi kwa majadiliano ya hoja zote za kiutumishi, kiutawala na kiutendaji ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi na huduma kwa wadau wetu…..Pia ni muhimu kuandaa programu za mafunzo ya masuala ya kitaaluma, kitaalam, maadili na umahiri mahala pa kazi na pia tuzingatie mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kutokea katika mifumo ya usimamizi wa fedha, mipango, uchumi, utawala bora na mazingira hii italeta chachu katika kutekeleza majukumu kwa weledi, ubunifu na uadilifu.” Ameeleza.

Kuhusiana na suala la afya Dkt. Natu amewataka wajumbe wa mkutano huo kutekeleza majukumu yao bila kuathiri afya zao kwa kutenga muda kwa ajili ya mazoezi, kuzingatika lishe bora na kupima afya mara kwa mara kwa kuwa maisha ya utumishi bila magonjwa sugu inawezekana.

“Niwapongeze watumishi 301 wa Wizara ya Fedha waliojitokeza katika zoezi la uelimishaji na upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukiza mahali pa kazi Mwezi huu Aprili, watumishi 179 walikuwa wanawake sawa na asilimia 56.5 ya watumishi wote waliojitokeza na wanaume walikuwa asilimia 43.5 na watumishi hao walipata elimu na kupima sukari, msukumo wa damu, macho, afya ya akili na UKIMWI.” Amesema.

Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa wengi wanakabiliwa na matumizi makubwa ya sukari, chumvi na mafuta kuliko mahitaji pamoja kutopata muda wa kupumzika hali inayopelekea wengi kuwa na uzito uliopitiliza na kuwashauri kuzingatia taratibu za afya wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Hazina Scholastica Okudo amesema kuwa mkutano huo unafanyika kila mwaka kwa mujibu wa Sheria na Wizara imekuwa ikitumia fursa hiyo kukutana na kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi na wadau mbalimbali na kuchochea uchumi wa Taifa.

Amesema Wizara ya fedha imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa uwazi na utawala bora hali inapelekea utekelezaji wa urahisi katika kuziba mianya ya rushwa.

Katika mkutano huo wa siku mbili wajumbe wao watapata fursa ya kujadili mada mbalimbali ya Wizara hiyo ili kuendelea kuleta matokeo chanya kwa Taifa.  

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 37 wa mwaka 2023/2024 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha leo Aprili 24,2024 Jijini Dar es Salaam














Top News