Benki ya CRDB kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii, Aprili 24 - 25, 2024 ilikabidhi madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kikilo na madarasa mengine mawili katika Shule ya Msingi Isabe zote za wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki hiyo.

Hafla ya kukabidhi madarasa hayo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa pamoja na Maafisa Elimu Sekondari na Msingi.

Katika hafla zote mbili Dkt. Khamis Mkanachi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali maombi ya ujenzi wa madarasa katika Wilaya ya Kondoa, ambayo yapo katika vijiji vya Kikilo na Bukulu. Huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani mazingira ya shule yanaendelea kuboreshwa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Mashauri Vicent aliyekabidhiwa madarasa hayo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya elimu pia kuahidi kuwa watahakikisha madarasa hayo yanakuwa ni sehemu ya kuchagiza ongezeko la wanufaika ambayo ni watoto kwenye jamii ya Kondoa.

Kwa upande wa Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay aliyeongozana na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji kwa Jamii pamoja na Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, amesema kuwa Benki ya CRDB imeweka sera ya uwekezaji kwa jamii inayolenga kuchangia maendeleo mbalimbali katika jamii hasa katika swala la Elimu, Mazingira, Afya, Vijana na Wanawake. Aidha, ametoa rai kwa wazazi wa shule hizo kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa shule katika kuboresha miundombinu ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay wakiwa pamoja na viongozi wengine pamoja na Wanafunzi katika moja ya madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 katika Shule ya Msingi Isabe, iliyopo katika kijiji cha Bukuru, Wilayani Kondoa, katika hafla  iliyofanyika Aprili 25, 202.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi (wanne kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB pamoja na wa Halmashauri ya Kondoa wakiwa katika picha ya paamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikilo, muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili katika shule hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.












Na WAF, TABORA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameziasa Kamati za Ulinzi na Usalama nchini kuona umuhimu wakuifanya ajenda yakutokomeza Malaria iwe yakudumu kwenye vikao vya maamuzi.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo, Aprili 25, 2024 akiwa amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye kilele cha Siku ya Malaria Duniani iliyofanyika mkoani Tabora na kusema kuwa kama nchi imeendelea kupiga hatua katika vita hivyo ikilinganishwa na miaka zaidi ya ishini iliyopita ambapo maambuki na vifo vya Malaria vilikuwa kati ya asilimia 45 hadi 50.

Aidha Dkt. Mollel amesema azma ya Serikali ni kufikia asilimia 3.5 ifikapo 2025 na kuwa na ziro Malaria 2030 huku akisisitiza kwa kusema itafikiwa endapo juhudi za Makusudi zitafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali na wadau

"Leo tunazungumza asilimia 8.1 kama nchi lakini miaka ya 1998, tulikuwa na kiwango cha juu sana, hivyo ili tuweze kufikia adhma yakumaliza kabisa malaria ifikapo 2030 kila mmoja wetu anawajibu wakufanya" amesema Mollel.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Samsoni Maella, amesema Utumiaji wa Mifumo ya GoTHOMIS na FFARS imekuwa chachu ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya ngazi ya maamuzi, hali iliyochangia kufanya maamuzi sahihi kutokana na kuwa na takwimu sahihi.

"Kama Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumefanikiwa kuimarisha miundo mbinu ya Afya na Rasilimali watu mathalani miaka mitatu nyuma tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 leo hii tunazo 177 hizi zimechochea sana uimarishaji wa huduma” amesema Mahela.

Naye Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI Dkt. Hamis Kigwangala ametoa wito kwa serikali na wadau kuongeza afua za kutibu watoto Shuleni, pia wafike maeneo ya Migodi, Mashamba Makubwa na maeneo ya Wafugaji.

Awali Msimamizi wa Miradi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim, akiwa amemwakilisha Katibu Mkuu, amesema kuchaguliwa kwa mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Wiki ya Malaria, ni pamoja na kuongeza nguvu ya afua za kupambana na Malaria kutokana na Mkoa huo kuwa na Maambukizi ya juu ya Ugonjwa huo ya asilimia 23.4 kwa sasa kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2011.






Mkutano Maalum wa 53 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika leo tarehe 25 Aprili 2024 Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mkutano huo, pamoja na masuala mengine umejadili na kupitisha Makadrio ya Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.).

Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb.) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi

Mkutano huo umefanyika kufuatia kukamilika kwa kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 24 Aprili 2024 ambacho kilitanguliwa na kikao cha ngazi ya Wataalam cha tarehe 23 Aprili 2024.







-95.28% kuelekezwa kwenye maendeleo
-Serikali kuja na Kanuni ya Uwajibikaji kwa wananchi Miradi ya Mafuta na Gesi Asilia
-Dkt. Biteko aagiza Halmashauri kupeleka fedha za Ushuru wa Huduma vijijini
-Masharti ufunguzi wa vituo vya CNG yarekebishwa kuvutia uwekezaji
-Kapinga atilia mkazo utekelezaji Nishati Safi ya Kupikia na CNG

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha shilingi Trilioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo asilimia 95 ya bajeti hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akijibu hoja mbalimbali za Wabunge ameeleza kuwa, ili wananchi wanaozunguka miradi ya Gesi Asilia na Mafuta wafaidike na rasilimali hiyo Serikali itapitisha kanuni itakayoongoza Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ili kampuni ziweze kuwajibika ipasavyo kwa jamii.

Aidha, kuhusu ushuru wa huduma (service levy) unaotolewa na kampuni za Mafuta na Gesi kwa Halmashauri mbalimbali nchini, Dkt. Biteko ameagiza Halmashauri hizo zihakikishe kuwa sehemu ya fedha hizo zinarudi kwenye vijiji ambapo miradi inatekelezwa.

“Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuja na mpango wa utekelezaji wa service levy ili fedha zinazotolewa ziende pia kwenye maeneo ambapo miradi inatekelezwa, Rais ameshaeleza hataki kuona malalamiko sehemu ambapo Gesi inachimbwa, Service Levy na CSR sasa zitaanza kufanyiwa kazi kwa kasi kubwa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesisitiza kuwa, suala la CSR si siri bali ni kitu cha wazi kwa wananchi na Wabunge hivyo ni haki kwa wananchi hao kupata taarifa za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na kusisitiza kampuni za kitanzania kupewa kipaumbele kwenye miradi ili wananchi wanufaike na rasilimali zilizopo nchini.

Kuhusu hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara miezi kadhaa nyuma, amesema ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa umeme wa megawati 410 lakini sasa uwezo wa kuzalisha umeme umekuwa mkubwa kuliko mahitaji huku mitambo minne ya Kinyerezi ikizimwa na kusubiri changamoto itakayojitokeza.

Amesema kwa sasa kukatika kwa umeme kunaweza kutokea si sababu ya upungufu wa umeme bali baadhi ya miundombinu ya umeme kuchoka kutokana na kuwa ya muda mrefu pia uhujumu wa miundombinu akitolea mfano wizi wa transfoma takribani 87 na nyaya za umeme pamoja na mvua zilizozidi kipimo ambapo mpaka sasa nguzo 651 na transfoma 36 zimeondolewa na maji.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na maboresho ya miundombinu ya umeme pamoja na uwekezaji kwenye miundombinu hiyo ikiwemo ujenzi wa vituo vya kupoza umeme.

Kwa wakandarasi wanaosuasua katika kutekeleza miradi ya umeme nchini ikiwemo kampuni za Serikali kama vile ya ETDCO, Dkt. Biteko amesema watachukuliwa hatua kali ikiwemo za kutowapa tena miradi mingine ya umeme.

Akizungumzia usambazaji umeme vijijini, amesema suala linalotiliwa mkazo na Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji kwanza, kisha vitongoji na baadaye kwenye nyumba na kwamba suala la kuwaunganishia umeme wananchi ni endelevu.

Kwa mikoa iliyo nje ya gridi kama vile Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara ameeleza kuwa mikoa hiyo itaunganishwa na gridi kupitia miradi mbalimbali inayoendelea na hii inajumuisha miradi ya kusafirisha umeme kwenda nchi nyingine za Afrika kama vile Kenya na Uganda.

Kuhusu bei ya umeme kwenye maeneo yanayojulikana kama Vijiji-Miji (Sh. 320,000) amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo la kuyatambua maeneo hayo na uchambuzi umeshafanyika huku maeneo 1,570 yakipatikana hivyo suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali ambapo utaratibu wa malipo kwenye maeneo hayo utaelezwa.

Akizungumzis uanzishaji wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG), Dkt. Biteko amesema suala hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa na sasa masharti ya kuanzisha vituo hivyo yamepunguzwa ambapo wawekezaji wakikamilisha nyaraka zinazohitajika ndani ya Siku Tatu watakuwa wamepata leseni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati kupitia miradi mbalimbali kielelezo na maendeleo inayoendelea nchini.

Akizungumzia Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Kapinga amesema kuwa, ni nyenzo muhimu ya kusaidia kutunza mazingira na kwamba mkakati wa kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia umeshapitishwa na Baraza la Mawaziri na upo tayari kufanyiwa kazi.

Amesema azma ya Serikali ni kuongeza kasi ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwemo gesi ambapo mkakati una lengo la kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi, salama, endelevu, yenye uhakika pamoja na kuondoa matumizi ya kuni na mkaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge.

Kuhusu gharama za mitungi ya Gesi amesema suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao umeanza kutoa ruzuku ya mitungi na mpaka sasa wameshatoa mitungi 83,500 na mingine 450,000 itatolewa kwa wananchi.

Aidha, kuhusu suala la kuwa na mitungi ya kilo chache ili wananchi waipate kwa gharama ndogo amesema tayari mitungi ya kilo tatu imeanza kuingia sokoni na Serikali inaendelea kusimamia ili kuwa na Mawakala wengi zaidi wa kusambaza gesi hata katika maeneo yaliyo mbali.

Vilevile kuhusu ujenzi wa vituo CNG na vya kubadilsha mifumo ya magari ili kutumia gesi amesema kuwa tayari ujenzi wa kituo mama umeanza katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam, vituo viwili vingine vinajengwa katika eneo la Kairuki na Muhimbili na vingine 20 vitajengwa kwa kushirikiana na Sekta binafsi.

Bajeti ya Wizara ya Nishati iliyoidhinishwa na Bunge ni shilingi 1,883,759,455,000 ambapo Shilingi 1,794,866,832,000 sawa na asilimia 95.28 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Shilingi 88,892,623,000 sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu ya viwango vya ubora kwa Wajasiriamali wadogo waliojitikeza katika Maonesho ya Kibiashara ya Miaka 60 ya Muungano katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo leo Aprili 25,2024, Afisa Masoko (TBS), Bw. Mussa Luhombero amesema wametoa elimu kwa Wajasiriamali hao jinsi ya kuzalisha bidhaa bora pamoja na ujuzi ambao utawawezesha kupata alama ya ubora ambayo itawafungulia wigo wa soko la ndani na la Kimataifa.

“Alama ya ubora kutoka TBS itawasaidia Wajasiriamali kuaminika sokoni na kukubalika katika masoko ya ndani na ya Kimataifa ambapo itawapatia mafanikio yenye tija kwao na Taifa kwa ujumla”. Amesema

Amesema wameshiriki katika maadhimisho hayo kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi hasa katika makundi mbalimbali ambayo ni wazalishaji,waagizaji,watumiaji wa bidhaa pamoja na wajasiriamali.

Aidha ametoa wito kwa waingizaji wa vipodozi nchini,kuingiza vipodozi ambavyo vimesajiliwa ambapo amesema kuwa kupitia tovuti yao kuna orodha ya vipodozi hivyo ambavyo haviruhusiwi kuingia nchini.

"Lakini pia wanaotumia vipozi wanaweza kututembelea ili tuweze kuwapa matumizi sahihi ya vipodozi na kwa wale wenye maduka ya chakula na vipodozi ambapo pia tunatoa elimu jinsi gani ya kusajiri maduka yao ya chakula au vipodozi". Amesema Bw. Luhombero

Sambamba na hayo Bw.Luhombero ametoa hamasa kwa wananchi wote kutumia bidhaa yenye alama ya ubora ya (TBS) ambapo itasaidia kuepukana na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora ambazo zinaweza kuhatarisha afya kwa watumiaji.

Kwa Upande wake, Mfanyabiashara wa Vipodozi, Bw.Hamza Kamba ambaye ni muagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ameeleza kuwa yeye kama mdau ametembelea banda la TBS na amejifunza bidhaa ambazo ni bora na zisizobora.

TBS ili kuhakikisha inalinda usalama wa wananchi imetoa namba yake kupiga bure ili kuripoti bidhaa ambazo ziko sokoni zenye kutiliwa shaka kuhusiana na kuthibitishwa na Shirika la viwango ambayo ni 0800 110 827.



Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, akizungumza na viongozi wa serikali wakiwemo wa vyama vya siasa wakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),leo katika uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI mkoani Mwanza kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imezindua kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya mawasiliano inayolenga kufikisha huduma hiyo kwa wananchi waishio maeneo yaliyo mbali vijijini yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma.

Pia,imewataka wadau wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini washirikiane na UCSAF kuhakikisha minara hiyo inakamilika kwa wakati wananchi wafikiwe na huduma hiyo.

Akizindua kampeni hiyo,leo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,amesema lengo ni kuelimisha wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa,hatua zilizofikiwa na serikali katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini na maeneo machache ya mijini.

Pia, kampeni hiyo inalenga kuweka msukumo wa kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio vijijini,hivyo wadau na UCSAF wakishirikiana kukamilisha mradi wa ujenzi wa minara 758,huduma za mawasiliano ya simu (Sauti na intenet/data),zitapatikana za uhakika maeneo yote.

Masala amesema huduma za mawasiliano ya simu zinagusa maisha ya watu,ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla,hivyo viongozi walioshikiri uzinduzi huo wawe mabalozi wazuri wa kuisemea serikali vizuri kwa wananchi utokana na elimu waliyoipata.

“Tunazindua kampeni hii kuhakikisha jamii ya Watanzania maeneo mbalimbali wanapata taarifa muhimu za utekelezaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano,licha ya kuzinduliwa Mwanza,itaendelea mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (Shinyanga,Mara,Simiyu,Geita na Kagera),iliyofaidika na mradi huu na mengine ya mawasiliano, ”amesema.

Masala amesema serikali kupitia UCSAF iliingia makataba na makampuni (watoa huduma ya mawasiliano ya simu) kufikisha mawasiliano katika kata 713 kwa kujenga minara 758, inayopaswa kukamilika 2024/25.

“UCSAF imewaita viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali mnaowakilisha Watanzania mpate elimu hii nanyi mkaisambaze,mkaisemee vizuri serikali kuhusu utekelezaji wa mradi huu, wananchi wafahamu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza masuala ya mawasiliano bila ubaguzi kwa Mtanzania yeyote,”amesema .

MKuu huyo wa Wilaya ya Ilemela amesema Ibara ya 61 ya Ilani ya CCM inaelekeza katika kipindi cha miaka mitano,sekta ya mawasiliano itajikita kuimarisha ubora wa mawasiliano nchini na kuhakikisha wigo unaongezeka na kuwafikia wananchi wote,katika kutekeleza hilo, Rais Dk.Samia alishudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano.

Pia,alishuhudia utiaji saini wa kuboresha na kuongeza nguvu minara 304 kutoka teknolojia ya 2G ya sauti pekee kwenda teknolojia ya intaneti/data ya 3G,4G na zaidi,hivyo kujengwa kwa minara hiyo vijijini ni utekelezaji wa ilani hiyo ya uchaguzi 2020-2025.
Naye Mratibu wa UCSAF Kanda ya Ziwa,Benard Buremo amesema baada ya makubaliano ya ujenzi wa minara hiyo kati ya wadau hao na serikali,watoa huduma walipewa miezi 24 ya kuikamilisha,kabla ya uchaguzi mkuu 2025 na kufafanua idadi ya minara hiyo 758 kwa kila kampuni ambapo Airtel inajenga 169,TTCL 104,Vodacom 190,Tigo 261 na Halotel 34.
Awali Ofisa Uhusiano wa UCSAF,Celina Mwakabwale amesema katika kuongeza ushindani katika soko la mawasiliano lilijitokeza ombwe lililosababishwa na nguvu za ushindani kujikita kupeleka mawasiliano maeneo yenye mvuto wa kibiashara na kuyaacha maeneo ya vijijini na ya mijini yasio na mvuto huo.

Amesema makampuni ya simu ni wabia wa serikali katika kutekeleza mradi huo unaogharimu sh.bilioni 126,ushirikiano huo umekuwa imara katika kufikisha huduma za mawasiliano hadi vijijini.


“Changamoto ya wananchi hawaufahamu Mfuko wa UCSAF,ulioanzishwa na Serikali kwa Sheria ya Bunge Namba 11 ya mwaka 2006 sura ya 422,kuwezesha na kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo machache mijini na mengine ya mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma wakihofia hasara,”ameeleza Mwakabwale.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano huyo serikali kupitia UCSAF imeingia mikataba na watoa huduma ya mawasiliano kufikisha huduma hiyo katika kata 1,974 zenye vijiji 5,111 kwa kujenga minara 2,158,ikikamilika wananchi 23,978,848 watapata huduma ya mawasiliano ya simu kwa uhakika.sssss
Ofisa Uhusiano wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),Celina Mwakabwale,leo akizungumza na wadau (hawapo pichani) waliodhuria uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.
Wakuu wa Wilaya za Misungwi na Sengerema,Johari Samizi (kushoto) na Senyi Ngaga (katikati), wakiwa katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya elimu kwa umma leo.Walioketi nyuma ni makatibu tawala wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
Maofisa Tarafa na Watendaji Kata mbalimbali mkoani Mwanza,wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa,leo wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.
Picha zote na Baltazar Mashaka

Top News