NA EMMANUEL MBATILO, MOROGORO

WANAWAKE viongozi na vijana wanasiasa wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa tija kwa lengo la kupeana taarifa na kuondokana na matumizi mabaya yenye kuleta athari hasi kwa vijana wakike wanaotarajia kuwa viongozi wa baadae.

Wito huo umetolewa Aprili 16,2024 mkoani Morogoro na Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Ruth John wakati akifungua mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19.

Alisema kuwa miaka ya sasa wanasiasa na viongozi wanawake wamekuwa wakikumbwa na ukatili na mashambulizi mitandaoni kutoka kwa watu wasio na mapenzi mema kwa nchi.

"Wanawake ni jeshi kubwa sana na ndio taswira ya taifa na mwanamke huyu anapochafuliwa katika mitandao ataathiri jeshi kubwa ambalo liko nyuma yake hasa vijana wanaochipukia kuwa viongozi hapo baadae", alisema.

Aidha alieleza kuwa mafunzo hayo yanakwenda kujenga uwezo na uelewa kwa wanawake kuhusiana na kutunza taarifa zao pamoja na namna ya kukabiliana na kudhibiti vitendo vya ukatili jambo ambalo litaweka uhakika wa kuwaweka salama wakati wote.

Pamoja na hayo Mhe.Ruth aliwaasa viongozi na wanasiasa kuwa makini na maudhui yao wanayoyaweka mitandaoni,ambapo amebainisha kuwa kukosekana kwa umakini na weledi husababisha mianya na matumizi mabaya ya maudhui ambayo yanaweza kuwaathiri wao na jamii yao.

Pamoja na hayo alitoa pongezi kwa Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE),YOGE pamoja na Article 19 kwa kuanzisha mafunzo hayo ambayo yataleta matokeo chanya kwa viongozi.

Kwa Upande wake Mwanzilishi wa Shirika la (TAMCODE) Bi.Rose Ngunangwa alisema wameamua kuanzisha mafunzo hayo baada ya kugundua kuwa kuna changamoto kwa wanawake kushambuliwa hasa kipindi cha uchaguzi unapokaribia jambo ambalo linadhoofisha nguvu zao katika kuwania nafasi za uongozi.

"Wanawake bado hawajapata ujuzi wa kutosha kwenye matumizi ya mitandao katika kujiwezesha kiuchumi ndio maana sisi TAMCODE,YOGE pamoja na Article 19 tumeona tuanze kuwajengea uwezo wanawake madiwani kwa ukanda wa pwani ili kuwawezesha wanapoelekea katika uchaguzi watumie mitandao kunadi sera zao", alieleza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender equality Bi.Philomena Mwalongo alisema mafunzo hayo yamelenga kuwainua wanawake na vijana katika nyanja ya kiuchumi,Siasa pamoja na Teknolojia.

"Tulifanya tafiti tukagundua kuna ombwe kubwa katika ushiriki wa Wanawake viongozi na wanasiasa katika kutambua matumizi salama ya mitandao,na sio tu kujinufaisha wanawake binafsi waliohudhuria hapa Ila kuwagusa wanawake wengine ambao hawapo hapa", alisema

Vilevile Diwani wa kata ya Mji Mpya,Manispaa ya Morogoro Bi.Emmy Kiula ametoa shuhuda ya kuchafuliwa mtandoni ambapo ameeleza kuwa jambo hilo halipendezi kwani linaondoa imani kwa wananchi ambao wamempa dhamana ya uongozi.

"Serikali iangalie sasa kwa wale ambao watabainika sheria iwe kali, watu waadhibiwe na waache tupo katika ulimwengu wa maendeleo,lakini sasa tunapoitumia tofauti mitandao inakatisha tamaa,mtu anapoitumia mitandao kutoa lugha chafu haipendezi,utu wa mtu ni kuheshimiana,"Bi.Emmy alieleza.

Mafunzo hayo,yamejuimuisha wanawake viongozi na vijana wanasiasa katika ukanda wa Mkoa wa pwani,Dar es Salaam pamoja na Morogoro yamejikita hasa kuwainua wanawake katika nyanja ya Uchumi,kisiasa na kiteknolojia kwa kuwajengea uwezo katika masuala hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender equality Bi.Philomena Mwalongo akizungumza wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Ruth John akifungua mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender equality Bi.Philomena Mwalongo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.
Mwanzilishi wa Shirika la (TAMCODE) Bi.Rose Ngunangwa akizungumza wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.


Matukio ya picha mbalimbali wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.


Matukio ya picha mbalimbali wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.





Matukio ya picha mbalimbali wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.



 Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Ruth John akiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro.

  (PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)


Rais Mstaafu Dkt. Kikwete akiwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Uongozi cha Julius Nyerere, Dkt. Nansozi Muwanga alipotembelea Kituo hicho kilichopo ndani ya Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda, jana Jumatatu.


Kituo hicho, kinachotoa mafunzo ya uongozi na kuandaa vijana kuwa viongozi bora, kinaratibiwa na chuo Kikuu cha hicho kikongwe Afrika Mashariki.


Dkt Kikwete alitembelea chuoni hapo alipoalikwa kama mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi. Mkutano huo, uliojadili umuhimu na nafasi ya viongozi waliopo madarakani kuandaa viongozi wanaochipukia, ulihudhuriwa na zaidi ya marais na viongozi wa sasa na waliowahi kuwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya nchini Uganda zaidi ya 1,000.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo utakaofanyika Aprili 16-18,2024 jijini Washington DC nchini Marekani.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha mashirikiano na usimamizi wa misitu ya miombo kwa nchi wanachama za SADC, upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya usimamizi wa misitu ya miombo kwa nchi wanachama wa SADC,namna ya kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda nishati safi pamoja na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mifumo ya ikolojia na uhifadhi wa viumbe hai.

Waziri Kairuki pamoja na ujumbe wake amewasili katika Ofisi za Ubalozi jijini Washington DC na kusaini kitabu cha wageni ambapo katika ujumbe huo ameambatana na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith Bwoyo.

Mkutano huo utafanyika chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Wakuu wa Nchi kutoka nchi za SADC pamoja na Mawaziri kutoka nchi za Msumbiji, Namibia na Angola, Wabunge kutoka Malawi, Botswana,Tanzania pamoja na Maafisa Waandamizi katika Sekta ya Misitu wa nchi hizo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (katikati) akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024. Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Deusdedith Bwoyo (kushoto).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kushoto) akijadili jambo  na Balozi wa Tanzania Nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kushoto) katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza (kulia) alipowasili katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani uliopo jijini Washington DC Aprili 15,2024.

Na Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Gungu Silanga amewataka madiwani na wabunge walioko Wilaya ya Bunda mkoani Mara kutokuwa na mashaka na watu wanaopita kupiga kelele na badala yake wafanye kazi kwani wananchi wanaona utekelezaji wa Ilani unaendelea kufanywa na Serikali ya Chama hicho.

Silanga ameyasema hayo leo Aprili 15,2025 katika kikao cha ndani ya Wanachama wa CCM Wilaya ya Bunda mkoani Mara baada ya kupewa nafasi ya kusalimia wanaCCM hao waliohudhuria kikao kazi cha Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ambaye yuko katika ziara katika wilaya hiyo akitokea Serengeti. Rorya, Tarime na Butiama.

“Wana Bunda kwanza nawapongeza kwa ushindi ambao umeupata mwaka 2020 kwa kupata madiwani na wabunge wengi.Watu wa Bunda wako timamu na sidhani kama kutakuwa na shida yoyote, wana Bunda ni wachapakazi , wapambanaji na mfumo wa Chama chetu ni kufanya kazi kwa uwazi na ukweli.

“Madiwani na viongozi wengine fanyeni kazi ya kutekeleza llani ya 20220, wanaopita na kupiga kelele achaneni nao, ukifanya kazi wananchi na wana CCM wanaona.Fanyeni kazi Chama kipo imara, Rais Samia Suluhu Hassan yuko imara na Kamati ya siasa Wilaya ya Bunda inafanya kazi,”amesema.

Pia amewahimiza wanaCCM kuendelea kushikamana kwani Chama hicho ili kiendelee kushika dola ni pale tu ambapo kuna muungano.




Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Aprili 16, 2024 amewasili Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro ambapo atakagua athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini katika maeneo ya Taweta, Masagati, Utengule na Malinyi.

Pia Mheshimiwa Majaliwa atazungumza na wananchi waliothirika na mafuriko hayo.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa pia ataelekea Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani ambapo pia atakagua athari za mafuriko pamoja na kuzungumza na wananchi katika maeneo ya Muhoro na Chimbi




Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeshauriwa kushirikiana na wadau wa kilimo ikolojia kutoa elimu kuhusu kilimo hicho ambacho kina tija kwenye soko na ni salama kwa afya za watumiaji.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Kilimo, Deo Mwanyika wakati akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma baada ya kukutana na Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima kilichokutana na kamati hiyo.

Mwanyika amesema kikosi kazi hicho kimeonesha kuna changamoto ya utekelezaji wa mkakati wa kilimo ikoloji ambao ulizinduliwa Novemba 9, 2023, hivyo ni wakati muafaka wa kuweka nguvu kwenye eneo hilo, hasa kwa kutoa elimu kwa wakulima na jamii juu ya faida ya kilimo hicho.

Amesema ni vema utekelezaji wa mkakati ukanza ili kilimo kinachotumia mbegu za wakulima kupewa kipaumbele.

"Mikoa mingi ya Nyanda za Juu Kusuni inazalisha mazao kwa wingi, ila inaonekana kukabiliana na changamoto ya lishe duni na udumavu, hivyo ni wakati muafaka wa kuelekeza nguvu kwenye kilimo hai, hasa kwenye kutoa elimu ambayo itazingatia mkakati wa kilimo ikolojia," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema historia inaonesha babu na bibi zetu waliweka mkazo kwenye matumizi ya mbolea za asili, hivyo kuna haja ya kurejea katika kilimo hicho pamoja na ukweli kwamba hawawezi kuacha kilimo cha kisasa moja kwa moja kutoka na mahitaji ya chakula duniani.

Amesema iwapo kutakuwa na mkazo wa kuwekeza nguvu kwenye mbegu za wakulima ni wazi kuwa jamii ya Kitanzania itakuwa salama kiafya kwa asilimia kubwa pamoja na uhakika wa soko.

"Kazi ya Bunge na kamati zake ni kushauri, kushawishi na kuweka msukumo kwenye mambo ambayo yanahusu jamii na sisi kama kamati tutafanya hivyo ili serikali iweze kuchukua hatua kwenye kilimo ikolojia ambacho kina tija kwa nchi na wananchi, " amesema.

Mjumbe wa Kamati, Dk Christine Ishengoma amesema watatumia nafasi zao kuhakikisha serikali kupitia wizara ya kilimo wanaweka kipaumbele kwenye matumizi ya mbegu za wakulima.

"Sisi tumezaliwa na kukuzwa kwa vyakula vya asili, hivyo tunakiri kuwa mbegu za asili ni nzuri kiafya, ila pia mnatakiwa kufanya utafiti ambao utaonesha mbegu za asili ni nzuri kuliko za kisasa, sisi tutaendelea kutoa elimu na kuishawishi serikali," amesema.

Mbunge wa Viti Maalum, Kuntu Majala amesema katika kuunga mkono juhudi za Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima yupo tayari kushirikiana nao kusambaza mbegu za wakulima katika shule 197 zilizopo wilayani Chemba mkoani Dodoma kwa kuwa mbegu hizo zina faida kwa afya ya binadamu.

Naye Mbunge anayewakilisha Vijana, Ng'wasi Kamani amesema kamati yao itahakikisha inashauri serikali ifanyie marekebisho ya sheria ya mbegu ili iweze kulinda wakulima wa mbegu asili, huku akishauri Kikosi Kazi cha Mbegu za Wakulima kuongeza juhudi katika kutoa elimu zaidi.

Mratibu wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi amesema wamefurahishwa na ushirikiano ambao wamepewa na kamati hiyo na kwamba wanapata nguvu ya kupigania mbegu za wakulima kwa moyo mmoja.

Mkindi amesema wadau wa kikosi kazi cha mbegu za wakulima wanatamani kuwepo kwa sheria ambayo itaweza kusaidia mbegu za mkulima ili zipewe nguvu ya kisheria na kuendelezwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Islands of Peace (IDP) Tanzania, Ayesiga Buberwa amesema ombi lao la kukutana na kamati hiyo ni kuhakikisha mbegu za mkulima zinalindwa na kuendelezaa hali ambayo itaiondoa nchi kwenye utegemezi wa mbegu na chakula.

"Sisi juhudi zetu ni kuona kuna mizani inayofanana hasa kwenye kulinda na kutunza mbegu zetu za asili ambazo zina lishe bora, tunaamini kamati itashauri serikali kufanikisha mipango yote ambayo inaenda kuleta tija kwenye mbegu za wakulima," amesema.

Joanita Kahangwa, Mwanachama wa Shirikisho la Wakulima Tanzania (CHIWAKUTA), kutoka mkoani Kagera, ameishauri Serikali iweke nguvu kwenye mbegu asili kwa kuwa zinaweza kukabiliana na wadudu, mabadiliko ya tabianchi na niendelevu.

"Tunaomba Serikali ilinde mbegu za asili kwa kuwa hazina madhara kama mbegu za kisasa, naamini kinachohitajika ni mafunzo zaidi ya kuzilinda na kuzitunza,"amesema.

Naye Elibaraka Joseph Mwanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA) amesema wabunge wanawajibu wa kulinda wakulima na Watanzania kwa nguvu zote, ili kuwa na taifa la watu wasio na changamoto za kiafya.

Baadhi ya zinazosishiki katika kikosi kazi cha mbegu za wakulima TABIO,, IDP, PELUM, TOAM), SAT, ECHO EA, ESAFF, AFRONET, ENVIROCARE, MVIWAARUSHA, MVIWAMA, MVIWAKI, (MVIWAMORO), TUSHIRIKI, ActionAid Tanzania na SwissAid Tanzania, ACB, ANSAF, VOCHAWOTA, SHIWAKUTA, FLORESTA na wengine







Na Mwandishi Wetu

MCHEZA gofu wa ridhaa kutoka klabu ya TPC mkoani Kilimanjaro, Ally Isanzu na mcheza gofu wa kulipwa kutoka Dar es Salaam, Hassan Kadio wameibuka vinara wa raundi ya pili ya michuano ya gofu ya Lina PG yaliyomalizika hivi karibuni mjini Morogoro.

Licha ya ushindi wao ambao unawaweka katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kucheza katika michuano ya kimataifa katika Falme za Kiarabu mabingwa hao pia walizawadiwa donge nono la fedha kwa ushindi wao.

Kadio ambaye alikuwa mshindi wa kwanza katika mashindano hayo alijizolea kitita cha Sh. Milioni 6.8 huku Isanzu akiondoka na Sh. Milioni 2 kama mshindi wa gofu ya ridhaa.

Licha ya kuwa bora katka kitengo cha ridhaa, Isanzu ndiye alikuwa na matokeo bora zaidi katika michuano hiyo baada kupata mikwaju 74,73,72 na 78 katika siku nne za michuano ambazo ilipitia mashimo 72.

Isanzu alimaliza na matokeo ya jumla ya +9 na kufuatiwa na Kadio mwenye matokeo ya +12. Aidha mchezaji Abddalah Yusuf aliyepata jumla ya alama +16 alikuwa wa pili kwa wachezaji wa kulipwa mbele ya mshindi wa tatu Nuru Mollel aliyepata alama +17.

Bryszon Nyenza ambaye alimaliza na + 18 alikuwa wa nne wakati nafasi ya tano ikienda kwa Isack Wanyeche aliyerudisha alama +22

Washindi watakaokwenda Dubai ni wale wenye matokeo mazuri ya jumla baada ya kumalizika kwa raundi ya tano za mashindano hayo.

Baada ya raundi ya pili ya Morogoro, Arusha Gymkhana sasa itakuwa ni mwenyeji wa raundi ya tatu na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa michuano hiyo, Yasmin Challi amesema kuwa raundi ya tatu itachezwa mwezi Julai mwaka huu.

Amesema kuwa wachezaji wengine katika kiwango cha kumi bora walikuwa ni Fadhil Nkya, Frank Roman, Salum Dilunga Ninja, na Athumani Chiundu.

Kwa upande wa wachezaji gofu ya ridhaa, baada ya Isanzu aliyemaliza kwa alama +9, nafasi ya pili ilichukuliwa na Isiaka Daudi Mtubwi mwenye +24 wakati Michael Massawe aliyemaliza na alama +30, alikuwa wa tatu na nafasi yha nne kushikwa na Victor Joseph mwenye alama +30 wakati nafasi ya tano ilishikwa na Seif Mcharo mwenye alama +32.







 

Na Munir Shemweta, MLELE


 

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda kilichopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi wametakiwa kusoma kwa bidii na malengo ili wapate kile walichokusudia kukipata kwenye chuo hicho.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 15 April 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe. Geophrey Pinda alipokutana na kufanya mazungumzo na wanafunzi wa chuo hicho cha Kilimo kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.

 

Amesema, ni vyema wanafunzi wanaosoma chuo hicho Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi kuangalia malengo yaliyowapeleka chuoni hapo sambamba na yale ya wazazi wao ili kupata kile wanachohitaji kutoka chuo hapo.

 

"Kama umekubali kuja katika chuo cha Katavi ambacho kiko mbali na macho yaliyo wazi na umekubali kuja hapa kuwa ‘serious’ na masomo yako utapata kitu kikubwa sana" alisema Mhe. Pinda.

 

Wanafunzi wa chuo hicho ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro mbali na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Kavuu mkoani Katavi kwa kuwatembelea ili kujua changamoto zinazowakabili, wamemuomba kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali chuoni hapo ikiwemo kupatiwa Mizinga ya Nyuki kwa ajili ya Masomo ya Vitendo, Mipira kwa ajili ya mpira wa Miguu na Pete pamoja na Televisheni.

 

Aidha, wamemuomba kusaidia upatikanaji mikopo kwa wale wanafunzi wasiopata mikopo ya elimu ya juu. Wamesema pamoja na mikopo kupatikana kwa asilimia tofauti kwa wanafunzi wa chuo hicho lakini wapo baadhi yao hawakupata kabisa jambo linalowafanya kuishi kwa shida.

 

"Ukiangalia mtu hana uwezo na mfano ni kwa mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo chetu wakati mwingine inatulazimu sisi wanafunzi wenzake timchangie" Wamesema wanafunzi.

 

"Hapa kuna wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawajapata mikopo ya elimu ya juu na yupo mmoja ukimuangalia hana uwezo kabisa tulilazimika kumchangia fedha". Walisema.

 

Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi Prof Anna Sikila amesema, pamoja na chuo hicho kuwa na mazingira mazuri lakini wanafunzi wamekuwa wakisoma vizuri na kujituma katika masomo yao.

 

Kwa mujibu wa Profesa Sikila, kujituma na kusoma kwa bidii kwa wanafunzi wa chuo hicho kumesababisha mwaka jana 2023 mwanafunzi kutoka chuo hicho kuongoza kimasoma kwa vyuo vyote viwili vya Morogoro na Katavi.

 

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda kinatoa kozi tatu za Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki, Stashahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao pamoja na Astashahada ya Uongozaji Watalii na Uwindaji wa Kitalii.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati wa kikao chake na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokione cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi. Kulia ni Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Profesa Anna Sikila na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano Debora Magesa.
Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila akizungumza wakati wa kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (Kushoto) na wanafunzi wa chuo hicho tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa katavi. Kulia ni Rais wa Serikali ya wanafunzi William Bulongo.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Geophrey Pinda (Hayupo pichani) wakati wa kikao chao kilichofanyika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024.

 
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Geophrey Pinda (Hayupo pichani) wakati wa kikao chao kilichofanyika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa tatu kulia), Naibu RASI wa Ndaki  Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Anna Sikila (wa kwanza kulia), Rais wa Serikali ya Wanafunzi William Bulongo pamoja na Wakuu wa idara wa chuo hicho wakiondoka mara baada ya kikao chao kilichofanyika chuoni hapo tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia) akizungumza na Naibu RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila (kulia) mara baada ya kikao chake na wanafunzi kilichofanyika chuoni hapo katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 15 April 2024. Wengine pichani ni wakuu wa Idara za ICT na Usimamizi Rasilimali Nyuki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda (wa tatu kulia) pamoja na RASI wa Ndaki Taaluma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda Prof Anna Sikila (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa chuo hicho mara baada ya kuzungumza nao tarehe 15 April 2024 wilayani Mlele mkoa wa Katavi.

 


Top News