Na Mwandishi Maalumu, Kampala

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amewaasa vijana wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa chachu ya utengamano katika Jumuiya hiyo kwa hatua zilizobakia za Umoja wa Kifedha na Shirikisho la Kisiasa.

Ameyasema hayo katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.

Mkutano huo uliojadili umuhimu na nafasi ya viongozi waliopo madarakani kuandaa viongozi wanaochipukia ulihudhuriwa na zaidi ya marais na viongozi wa sasa na waliowahi kuwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya nchini Uganda zaidi ya 1,000.

Makamu wa Rais wa Uganda, Bi. Jessica Allupo na Waziri Mkuu Mstaafu wa nchi hiyo Ruhakana Rugunda pia walishiriki katika mkutano huo uliofanyikia katika Chuo Kikuu maarufu cha Makerere, Kampala nchini Uganda.

Pamoja na mambo mengine, washiriki wa mkutano huo, ambao wengi ni vijana, walijadili kwa kina na uwazi fursa, changamoto na matamanio yao kama vijana ambai tayari wameonesha uwezo wa kuongoza na namna serikali na jamii ya Uganda inavyoweza kuwatumia katika nafasi mbalimbali za kiongozi serikalini, kwenye mashirika mbalimbali na kwenye jamii kwa ujumla.

Aidha, suala la kufanya siasa za vyama ndani ya vyuo vikuu lilijadiliwa kwa kirefu ambapo washiriki walitofautiana maoni ambapo wapo walioona kuwa ushiriki kwenye siasa za vyama kwa wanafunzi waliopo vyuoni ni jambo la msingi katika kutetea maslahi ya wanafunzi na kuwaandaa wanafunzi kuwa viongozi na wanasiasa wazuri wa siku za usoni, huku wengine wakieleza mtizamo wao kuwa mwanafunzi makini anaweza kuwa kiongozi katika nafasi mbalimbali kwenye jamii bioa ya kufungamana na vyana vya siasa.

Waliounga mkono hoja hii walieleza kuwa, siasa vya vyama zinaweza kufungamanisha na kufunga mawazo mazuri ya kimaendeleo aliyonayo mwanafunzi kwa ajenda za kiasiasa za chama cha siasa ambacho ni mwanachama na kumfanya kutoona maeneo mengine kwenye jamii ambayo anaweza kuonesha uwezo wake wa kiuongozi.

Kwa upande wake Rais Mstaafu Kikwete aliwapa uzoefu wake katika siasa za vyuo vikuu alipokuwa Rais Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 - 1973 na namna alivyojifunza kipindi hiko umuhimu wa viongozi vijana kuwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati.

Akawaasa viongozi hao kujifunza kujenga hoja za nguvu ya kufanya mabadiliko katika mambo wanayoyataka na kujiepusha na kishawishi cha kulazimisha jambo ambalo wakati wake bado haujafika au kwa kukiuka taratibu ambazo zimewekwa kwa makubaliano ya pamoja.

Akaongeza kuwa kijana yoyote, si lazima awe kiongozi, ana uwezo wa kutumia vyema kipaji chake, uwezo wake wa kufikiri na nguvu alizonazo kupaza sauti itakayoleta mabadiliko katika jamii na taifa lake kwa ujumla.

Aidha, kwa nafasi yake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Kikwete alieleza kuvutiwa kwake na ubunifu wa mkutano huo kwa kuwakutanisha viongozi wa sasa na wa zamani wa vyuo vikuu pamoja na viongozi wa serikali kwani unatoa fursa ya kujadili na kulinganisha hatua zilizofikiwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ambayo serikali za wanafunzi zimekuwa zikiyafuatilia kwa nyakati tofauti.

Vile vile, alishauri kuwa itakua jambo la busara kwa mkutano huo sasa kuandaliwa katika ngazi ya vyuo vyote kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuwa jukwaa jingine la vijana kijadili masuala ya jumuiya na kuwa chachu ya kuharakisha jitihada za utenganamano wa kikanda katika nchi za EAC.

Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Jopo la Wazee la Jumuiya ya Maendelo Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Mstaafu Dkt. Kikwete alitumia fursa ya kuwa Uganda kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na usalama katika ukanda wa maziwa makuu na kusini mwa afrika.

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akifurahia jambo kabla ya kuhutubia katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi jana Jumatatu.
Makamu wa Rais wa Uganda, Bi. Jessica Allupo  akifuatilia hotuba ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda.

Wahudhuriaji katika katika mkutano mkuu wa kwanza wa marais na viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Uganda ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameridhia kutoa tani 189 za mbegu za mpunga, mahindi na alizeti ili zisambazwe kwa wakulima wa wilaya ya Kilombero.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa wananchi wote walioathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazonyesha nchini, lakini pia ametoa mbegu hizo ili kuhakikisha wale waliopata athari katika mashamba yao waweze kuendelea na shughuli za kilimo pale hali itakapokaa sawa,” amesema.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 16, 2024) wakati akizungumza na wananchi wa maeneo ya Mlimba, Taweta, Masagati wilayani Kilombero, mkoani Morogoro ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko.

Waziri Mkuu ambaye pia alikagua bonde la mto Kilombero linalojumuisha wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi, amesema Rais Samia ameelekeza Serikali iendelee kuwahudumia wananchi wote waliopata athari ikiwemo kuimarisha maeneo ya utoaji huduma za afya, kugawa vyakula na kurejesha miundombinu ikiwemo barabara na reli.

“Watanzania tuwe watulivu, Serikali yenu ipo kazini. Rais wetu Dkt. Samia ametupa maelekezo ya kuhakikisha tunawahudumia na kurejesha hali, tutaleta vyakula na tayari madaktari takribani 20 wameshasambazwa kwenye mikoa ya Morogoro na Pwani ili waweke kambi za utoaji huduma za afya.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.

Waziri Mkuu anaelekea Ikwiriri, Muhoro na Chumbi wilayani Rufiji, mkoani Pwani ambako atakagua athari za mafuriko na kuwasalimia wananchi.



Na Shalua Mpanda

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Sixtus Mapunda ameonesha kukasirishwa na tabia ya madereva wa malori na wamiliki wa viwanda kuegesha malori pembezoni mwa hifadhi ya barabara.

Akiwa katika ziara ya kushtukiza katika eneo la barabara ya Mbozi iliyopo kata ya Chang'ombe wilayani humu leo Aprili 16,2024 , Mapunda amesema, umefika wakati wa kila mmoja kuheshimu Sheria zilizowekwa ili kuepusha kero kwa watumiaji wengine wa barabara.

"Nimeshatoa maagizo,hawa wote walioegesha magari yao pembezoni mwa hii barabara,Mamlaka husika zichukue hatua stahiki....leo hii hapa ikitokea ajali ya moto gari za zimamoto zitaweza kupita hapa?"Alihoji Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha Mapunda amewataka wenye viwanda na bandari kavu kuweka utaratibu wa kuwa na maeneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya malori wakati wa kusubiria kuingia kwenye viwanda hivyo.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioongea na mwandishi wa habari hizi walisema uegeshaji huo
umechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa miundombinu ya barabara hiyo.

Barabara hiyo muhimu ya Mbozi imekuwa na msongamano mkubwa wa malori hasa nyakati za asubuhi na jioni kutokana na malori mengi yakiwemo mabovu kuegeshwa pembezoni hali inayochangia kwa kiasi kikubwa foleni hiyo.



 

Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Sixtus Mapunda akiwa katika ziara ya kikazi,akikaangalia uegeshaji malori ambao ameoneshwa kukerwa nao

Zaidi ya tani 200,000 (laki mbili) za korosho ghafi, zimesafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara katika msimu wa mwaka 2023/2024. 

Akizungumza tarehe 16 Aprili, 2024 kwenye mkutano wa Wadau wa maendeo wa ushoroba wa Mtwara uliofanyika mjini Mtwara, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Mhandisi Juma Kijavara amesema mafanikio hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa mwezi Septemba mwaka 2023.

Amesema Korosho ghafi kutoka Mtwara zilikuwa zinasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam lakini kuanzia msimu wa 2023/2024, Korosho zimekuwa zinapitia Bandari ya Mtwara ikiwa pia ni baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Bandari hiyo ikiwemo kuongeza vifaa vya kisasa zikiwemo mashine za kupakia na kupakua mizigo na kuongeza idadi ya Wafanyakazi katika Bandari hiyo.

Kuhusu Ujenzi wa Bandari maalumu kwa mzigo mchafu ya Kisiwa Mgao, Mhandisi Kijavara amesema Mkandarasi wa ujenzi wa Bandari hiyo ameshapatikana na kwamba ujenzi unatarajia kuanza Mwezi Mei 2024, na utatekelezwa kwa miezi 24.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini Bi. Devotha Gabriel, amesema ushoroba wa Mtwara ni lango kuu la biashara na uwekezaji kwa ukanda wa kusini na Tanzania kwa ujumla na ukiendelezwa ipasavyo utaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya Wananchi.












Na Mwandishi wetu;-

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) amewakumbusha Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuzingatia Afya sambamba na kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili kwa sababu kazi ya maokozi inahitaji nguvu na maarifa.

Mhe. Sillo ameyasema hayo leo Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana tangu kuapishwa kwake tarehe 4 Aprili, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kulipongeza kwani utendaji kazi wake unaonekana hauna kificho.

"Hongera sana Kamishna Jenerali wa Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji na Makamanda wote nimejifunza na kujua lengo kuu la kuanzishwa kwa Jeshi hili kuwa ni Kuokoa Maisha na Mali za Watanzania na hata wasio Watanzania hivyo mzingatie sana na kuweka moyoni kwamba kazi yenu ni kuwahudumia Watanzania hivyo fanyeni kazi kifua mbele kwa kujitoa kuwahudumia kwa weledi na uzalendo" Alisema Mhe. Sillo.

Mhe. Sillo amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji kuendelea kuboresha huduma kwa Wazimamoto na Waokoaji kwa kuongeza mikakati ya kuwapatia uwezo wa mafunzo na vifaa pamoja na msaada wa kisaikolojia kwani uwekezaji katika mafunzo kwa wazimamoto na waokoaji ni jambo la msingi na halipaswi kukwepa.

Aidha Mhe. Sillo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulijengea uwezo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vitendea kazi ambavyo ndivyo vinavyo tumika katika maokozi sehemu mbalimbali.

Kupitia hotuba yake Mhe. Sillo amewapa pole Askari wote waliopata ajali ya kuungua moto wakati wakiwa katika harakati za kufanya maokozi kwenye ajali ya basi pamoja na lori la mafuta iliyotokea hivi karibuni eneo la Mlandizi Mkoani Pwani.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga, alimpongeza na kumshukuru Mhe. Sillo kwa kuonesha shauku ya kutaka kujua majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na changamoto zake.











 

Na Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Gungu Silanga amewataka madiwani na wabunge walioko Wilaya ya Bunda mkoani Mara kutokuwa na mashaka na watu wanaopita kupiga kelele na badala yake wafanye kazi kwani wananchi wanaona utekelezaji wa Ilani unaendelea kufanywa na Serikali ya Chama hicho.

Silanga ameyasema hayo leo Aprili 15,2025 katika kikao cha ndani ya Wanachama wa CCM Wilaya ya Bunda mkoani Mara baada ya kupewa nafasi ya kusalimia wanaCCM hao waliohudhuria kikao kazi cha Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ambaye yuko katika ziara katika wilaya hiyo akitokea Serengeti. Rorya, Tarime na Butiama.

“Wana Bunda kwanza nawapongeza kwa ushindi ambao umeupata mwaka 2020 kwa kupata madiwani na wabunge wengi.Watu wa Bunda wako timamu na sidhani kama kutakuwa na shida yoyote, wana Bunda ni wachapakazi , wapambanaji na mfumo wa Chama chetu ni kufanya kazi kwa uwazi na ukweli.

“Madiwani na viongozi wengine fanyeni kazi ya kutekeleza llani ya 20220, wanaopita na kupiga kelele achaneni nao, ukifanya kazi wananchi na wana CCM wanaona.Fanyeni kazi Chama kipo imara, Rais Samia Suluhu Hassan yuko imara na Kamati ya siasa Wilaya ya Bunda inafanya kazi,”amesema.

Pia amewahimiza wanaCCM kuendelea kushikamana kwani Chama hicho ili  kiendelee kushika dola ni pale tu ambapo kuna muungano.




Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar imesifu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa jitihada inayofanya katika usimamizi wa sekta ya usafiri wa anga Tanzania bara na Zanzibar na kupelekea kuimarika usalama wa usafiri wa anga nchini.

Wajumbe wa kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake Mhe. Yahya Rashid Abdallah wametoa pongezi hizo wakati walipotembelea Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakiongozana na watendaji wa Mamalaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kwa ajili ya kujifunza na kuongeza uwezo wa kusimamia anga kwa njia za kisasa zenye usalama zaidi.

Akiupokea ujumbe huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Daniel Malanga amesema hata sasa wakati taifa linatimiza miaka 60 ya muungano, Mamlaka itaendelea kusimamia sekta hii muhimu kwa kufuata misingi na miongozo yote stahiki ya kitaifa na kimataifa ili Taifa liendelee kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta hii adhimu.

Wajumbe wa Baraza wamesema usalama wa anga unatakiwa kupewa kipaumbele na kutazamwa kwa upana wake katika kuimarisha huduma za uongozaji ndege ili kuiwezesha anga kuwa salama na kuleta tija.

Aidha wajumbe hao wameisisitiza TCAA kuhakikisha wakati wote inakua mstari wa mbele katika kupokea teknolojia mpya za sekta ya anga ili kuhakikisha taifa haliachwi nyuma na mageuzi yanayotokea kwa kasi duniani.

Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya baraza la wawakilishi ipo Tanzania bara kwa ajili ya shughuli za kawaida za kamati hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Daniel Malanga akiwasilisha majukumu ya Mamlaka mbele ya Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar lipotembelea Makao Makuu ya TCAA kujionea na kujifunza shughuli za usimamizi wa sekta ya usafiri wa anga nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar Yahya Rashid Abdallah akizungumza mara baada ya kamati hiyo kupata taarifa ya kazi zinazofanywa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Baadhi ya wanakamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar  wakiuliza maswali mara baada ya kupata maelezo kuhusu kazi zinazofanywa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) walipotembelea makao makuu wa Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanakamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar, Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, watendaji wa Mamalaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakifuatilia mada iliyokuwa inatolewa kuhusu Mamlaka hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Godlove Longole akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho kwa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar waliofika chuoni hapo kwa ajili ya kujifunza na kujua kazi hasa za TCAA.
Picha ya pamoja 

Top News