Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 kutoka kwa Bw. Charles Kichere Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 28 Machi, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2022/2023 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna wa Polisi Salum Hamduni Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 28 Machi, 2024. 


Dar es Salaam - Machi 27, 2024. Katika jitihada za kuongeza upatikanaji na matumizi ya simu janja ili kuziba pengo la kidijitali nchini, makampuni ya Vodacom Tanzania PLC na Benki ya CRDB wamezindua mpango wa kuwezesha Wateja wao kumiliki simujanja zenye ubora kwa gharama nafuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo wa kukopesha simu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alieleza kuwa kampuni hiyo ya simu inatekeleza mipango mbalimbali ya kupunguza gharama za vifaa vya mawasiliano ili kuwawezesha wateja wake kuhama kutoka kwenye matumizi ya mtandao wa 2G na kumiliki simu zenye uwezo wa 4G na kutumia fursa hiyo ili kunufaika na faida kemkem zinazopatikana kupitia mtandao huo.
"Tukiwa ni mdau na mshirika mkubwa wa sekta ya mawasiliano na teknolojia, Vodacom tunajivunia kuzindua mpango huu na Benki ya CRDB ambayo ni taasisi kubwa ya fedha nchini. Ushirikiano wetu unalenga kuwawezesha wateja kutoka pande zote mbili kupata aina mbalimbali za simujanja kwa bei nafuu na mpango wa malipo kwa awamu kwa kipindi fulani. Ili kujua kama amekidhi vigezo, mteja atatakiwa kupiga *150*00*44# nbaada ya hapo atafanya malipo ya awali na kupewa simujanja. Mkopo huu unaweza kulipwa kwa siku, kwa wiki au kwa mwezi kwa kipindi cha hadi miezi 12 kupitia M-Pesa," alifafanua bwana Besiimire.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema, “ushirikiano huu baina yetu na Vodacom ni fursa nzuri kwa Watanzania kupata huduma za kifedha na mawasiliano kwa gharama nafuu. Kwa hiyo kama wadau muhimu tunapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha wananchi wake wanafaidika na ukuaji na maendeleo katika sekta hizi.” 
Bwana Nsekela aliongeza kuwa, “Kwa mtandao wetu ulioenea nchi nzima, CRDB tumekuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya Watanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha. Hivyo basi, kwa kushirikiana na Vodacom, tutaweza kutoa mchango wetu ili kuongeza matumizi ya simujanja nchini.”


Licha ya juhudi za mamlaka nchini kusogeza huduma za mawasiliano, wananchi wengi bado wanatumia huduma za mtandao wa 2G. Hii inapunguza upatikanaji wa fursa zilizopo mtandaoni pamoja na kufurahia na kunufaika na intaneti yenye kasi zaidi kutoka Vodacom pamoja na bidhaa nyingine za kidijitali.

Matumizi ya simujanja na intaneti yana faida kwa jamii kama vile kukuza ukuaji wa kiuchumi kwa kuwezesha ujasiriamali wa kidijitali na kuchochea uvumbuzi, utafutaji masoko mitandaoni pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi wanaoamua kujiajili kupitia dijitali.
Vodacom Tanzania imekuwa ikishirikiana na watengenezaji mbalimbali wa simu za mkononi na taasisi za kifedha ili kuwezesha Watanzania kumiliki simu kupitia mikopo nafuu na mipango rafiki ya malipo kwa mteja. 

Mwezi August 2020, Vodacom ilizindua programu ambayo inawaruhusu wateja wake kumiliki simujanja kupitia mkopo unaolipwa kwa awamu, huku kianzio kikiwa ni Shilingi 20,000 za Kitanzania kwa muda wa miezi 12. 

Bwana Nsekela alimalizia kwamba anaamini kuwa taasisi hizo mbili zina huduma mbalimbali za kibunifu ambazo zitawanufaisha na kuboresha maisha ya wateja wao. Pia alitoa wito kwa Watanzania wanaotumia simu za kawaida na wanataka zenye ubora zaidi kufika katika maduka ya Vodacom na kupata simujanja kwa bei nafuu ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali duniani.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati lililolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kuzisaidia nchi za kipato cha kati kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Mkutao huo umefanyika kwa njia ya Mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akitoa wito kwa taasisi za fedha za kimataifa kuongeza fedha kwaajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati wakati akifungua mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati lililolenga kujadili namna mashirika hayo ya fedha yanavyoweza kuongeza fedha kwa nchi hizo. Mkutano huo umefanyika kwa njia ya Mtandao kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwaka, akitoa mada wakati wa mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati, ambapo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) aliongoza mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizaraya Fedha, Bi Amina Khamis Shaaban na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara hiyo, Bw. John Kuchaka, wakifuatilia uwasilishwaji wa taarifa wakati wa mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati, ambapo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)


Na. Peter Haule, WF, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati uliolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi zao itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Akifungua mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Dunia inakabiliwa na migogoro mingi na changamoto za maendeleo ya kiuchumi ambazo zinasababisha kutofikiwa kikamilifu kwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Alisema kuwa kupungua kwa nafasi ya kifedha katika kushughulikia migogoro hiyo kunadhoofisha uwezo wa Serikali za nchi hizo kufadhili programu za kijamii, kuharakisha ufufuaji wa Uchumi na pia kuongeza madeni katika nchi hizo.

“Mizozo inayoendelea nchini Urusi na Ukraine, Mashariki ya Kati na baadhi ya nchi nyingine za Afrika imechochea kupanda kwa bei ya vyakula na kuwasukuma mamilioni ya watu kwenye uhaba wa chakula”, alisema Dkt. Nchemba.

Aidha Dkt. Nchemba aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake wa kuzijengea uwezo taasisi katika kuyafikia maendeleo endelevu lakini pia kufufua uchumi kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokea Duniani.

Vilevile alisema kuwa kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia sio kazi rahisi kwa nchi moja, hivyo ameomba kuwa na nguvu ya pamoja katika Kanda na Bara la Afrika katika kutafuta utatuzi wa changamoto hizo.

Dkt. Nchemba ameishukuru Benki ya Dunia kwa kummwamini kuongoza kikao hicho kikubwa lakini pia amewashukuru viongozi mbalimbali waliotoa mada ambazo zimewafunbua macho kwa kuona fursa zilizopo katika kukuza una kuwezesha biashara na pia kuwa na majadiliano mazuri wakati wa mikutano ijayo ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) itakayofanyika mwezi Aprili, 2024 jijini Washington D.C nchini Marekani.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwaka, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ilitoa misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni tatu kwa nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema kuwa mwaka wa fedha uliopita Benki ya Dunia kupitia Mfuko wa IDA ilitoa dola bilioni 2.4 na kwamba kiwango cha misaada na mikopo hiyo imeendelea kuongezeka na miongoni mwa nchi zilizonufaika na mpango huo ni Tanzania, Kenya na Eswatini.

Aidha, Bi. Kwakwa amevitaja vipaumbele vya Benki hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha nchi zitapata umeme wa uhakika, kuwa na maendeleo ya kidigitali, upatikanaji wa ajira, mapinduzi ya kiuchumi, kujenga uwezo kwa rasilimali watu na masuala ya elimu.

Baadhi ya Viongozi walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika, Bw. Sergio Pimenta, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Bi. Anshula Kant, Mawaziri wa fedha na Mipango (Magavana) na wajumbe wengine.
Katika kuhadhimisha mwezi wa kumsheherekea Mwanamke na kukaribisha sikuukuu za Pasaka, Halotel Tanzania yatoa msaada kwa wanawake chini ya Taasisi ya ‘Jukwaa la wanawake na wasichana wenye ulemavu Mtwara’ kusaidia changamoto mbalimbali wanazozipata wanawkae hao.

Halotel ikiwa ni kampuni ya mawasiliano Tanzania, ikitoa huduma mbalimbali za mawasiliano na ikiendelea kukidhi mahitaji ya wateja wao. Kwa kuzingatia usalama na uaminifu Halotel inaendelea kutoa huduma bora na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya mawasiliano na jamii kiujumla.

Akiongea katika tukio hilo Mkurugenzi wa Halotel tawi la Mtwara Bwana Emmanuel Monyo “Halotel inaendelea kusimama imara katika kufanikisha malengo yake ya kukuza usawa na ujumuishaji katika pande zote za jamii.

 Lakini kwa kuwasaidia wanawake hawa Mtwara Halotel inaonyesha dhamira yake ya kuleta mabadiliko katika jamii na kuunda ulimwengu weye uwezekano na fursa kwa wote”.

Afisa uhusiano na mawasiliano wa Halotel, Roxana Kadio ambae aliwasilisha msaada huo alisema Halotel inaedelea kujenga ujumuishaji ambao kila mtu bila kujali uwezo wao anaweza kushiriki kikamilifu katika jamii, aliendelea kusema kuwa Halotel iliamua kuwaunga mkono wanawake wa Mtwara baada ya kujifunza kuwa wanapitia changamoto za chakula na vifaa vya nyumbani na kama kampuni inayokua nia yetu kutoa mkono wa msaada kwa jamii ya kitanzania.

“Mahitaji yaliyotolewa na Halotel ni pamoja na Chakula kama Mchele, Sukari na Mafuta ya kupikia lakini pia kutoa msaada wa magodoro na vifaa vingine vya nyumbani. Vyote hivi ni katika kuwahudumia wanawake hawa na kuwaonesha kuwa hawako peke yao katika changamoto wanazozipita” Roxana alisema.

 Aliendelea kusema kuwa msaada huu pia unalenga katika kuwatoa upweke wanawake hawa katika mahitaji yao. Na kwamba Halotel haitoishia kusaidia tu wanawake na wako kwenye mpango wa kukuza uhitaji wa jamii kiujumla.

Halotel itaendelea kutoa ushirikiano kwa majukwaa ambayo yanajikita katika kuwainua wanawake. Lakini pia Halotel itaendelea kutia chachu ya maendeleo kwa wateja wake na jamii kiujumla.



Halotel wakikabidhi msaada wa Vifaa vya nyumbani na Chakula katika taasisi ya Jukwaa la Wanawake walemavu Mtwara. Kushoto akiwa Mkurugenzi wa Tawi la Halotel Mtwara Bw. Emmanuel Monyo, Kati ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Jukwaa la Wanawake walemavu Mtwara Bi. Fatuma Mohamed Mkondomoka, Kulia Afisa uhusiano na Mawasiliano makao makuu Halotel Bi. Roxana Kadio.






Upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufungua Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufungua Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.
Diwani wa wilaya ya Mtwara, Farida Abdallah akizungumza wakati akitoa Kestoria yake ya kuwania nafasi ya uongozi katika Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.
Diwani wa wilaya ya Mtwara, Farida Abdallah akizungumza wakati akitoa Kestoria yake ya kuwania nafasi ya uongozi katika Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.

Diwani wa wilaya ya Mtwara, Farida Abdallah akizungumza wakati akitoa Kestoria yake ya kuwania nafasi ya uongozi katika Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.
Diwani wa wilaya ya Mtwara, Farida Abdallah akizungumza wakati akitoa Kestoria yake ya kuwania nafasi ya uongozi katika Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.
Wanawake na Wasichana ambao ni washiriki kutoka Dar es Salaam, Pwani na Mtwara wakimsikiliza Diwani wa wilaya ya Mtwara, Farida Abdallah wakati akitoa Kestoria yake ya kuwania nafasi ya uongozi katika Kilinge salama kwa Wanawake, Wasichana na Viongozi kilichofanyika leo Machi 28, 2024 katika Ukumbi wa Mtandao huo Jijini Dar es Salaam.

KILINGE Salama (Safe Space) kilichoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) Chamwibua Diwani, Farida Abdallah ambaye ni Diwani wa wilaya ya Mtwara ambapo ameeleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wanawake viongozi ikiwemwo kukatishwa tamaa ili wasiweze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Akizungumza leo Machi 28, 2024 wakati wa kilinge salama kilichofanyika katika ukumbi wa TGNP jijini Dar es Salaam, Diwani huyo ambaye aliishia kidato cha pili na kupata ujauzito huku akimpote Mama yake mzazi amewaasa wanawake kutokukata tamaa pale yanapojitokeza maneno ya kukatisha tamaa pale yanapojitokeza wakati wa harakati za kutafuta nafasi za uongozi.

“Wakati nawania nafasi ya uongozi watu walikuja kunikatisha tamaa ili ni sigombee….. hata kwenda kumshawishi Mme wangu ili anikatishe tamaa lakini hawakufanikiwa….” Amesema Farida.

Kwa Upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufungua Kilinge salama ambapo ni mazingira ambayo ni rasmi au yasiyo rasmi ambayo wanawake na wasichana wanapata nafasi ya kujadili kwa uhuru masuala yao, amesema kuwa Katika mwezi Machi wa wanawake, TGNP imekuwa ikiandaa vilinge hivyo ili kuhamasisha wanawake kuingia katika nafasi za uongozi. 

“Mategemeo yangu ni kwamba mwisho wa siku ya leo tutaungana kwa pamoja kuendelea kusimamia Agenda ya mwanamke na uongozi katika mkoa wetu wa Dar es Salaam.” 

Pia Mkurugenzi Mtendaji Lilian ameweka bayana takwimu za Wenyeviti wa vijiji kuwa ni asilimia 2.1, Wenyeviti vitongoji ni asilimia 6.7 na Wenyeviti mitaa ni asilimia 12.6. 

Kwa upande wa Wabunge wa kuchaguliwa, wanawake ni 25 ya Wabunge 264 ambayo ni sawa na asilimia 9.5 tu ya Wabunge wote, idadi ya Wabunge wanawake wa Viti Maalumu ni 113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya Wabunge wote.  Jumla ya Wabunge Wanawake ni 142 sawa na asilimia 37 ya idadi ya Wabunge wote ambao ni 393 ambapo ili kufikia 50 kwa 50 ya uongozi wa Wanawake Viongozi lazima ifikiwe kwa kutoa elimu kwa wanawake na wasichana waweze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Lilia pia ameeleza kuwa malengo ya Kilinge salama kwa Wasichana na Wanawake ni kukaa pamoja na viongozi wanawake wanaochipukia na viongozi wanawake wenye uzoefu, kuandika na kusambazi kestoria za safari za uongozi za wanawake viongozi mahiri ili kuonesha michango waliyonayo katika maendeleo ya nchi.

Pia kutoa hamasa kwa viongozi wanawake wanaochipukia au wanawake wanaotamani kuwa viongozi. 

Kilinge Salama kwa Wanawake na Wasichana pamoja na viongozi leo ni kutoka mkoa wa Dar es Salaam, halmashauri za Ilala, Kinondoni na Temeke, Mtwara, Lindi na Pwani.

 

Na: Mwandishi Wetu – KILIMANJARO

 Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameeleza hadi sasa maandalizi ya uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru yamefikia zaidi ya asilimia 90 huku akihimiza Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha unahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria.

 

Amesema hayo wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Mkoani Kilimanjaro.

 

Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema kuwa Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2024 zinaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa rasmi mwaka 1964 zikienda sanjari na Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

 

Vile vile, Mhe. Katambi ameupongeza mkoa huo kwa utayari na maandalizi mazuri ya tukio hilo la kitaifa na kuongeza kuwa mwenge huo ni alama ya umoja, hivyo utakimbizwa katika halmashuri 195 kwa lengo la kuunganisha wananchi sambamba na kukagua viwango vya utekelezaji wa miradi ya serikali katika kuwahudumia wananchi.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Rajab amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara hiyo wamekua wakishirikiana kwa karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo wa Kilimanjaro katika kuhakikisha maandalizi yanakamilika ndani ya muda uliopangwa.

 

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Jackson Masaka amesema kuwa viongozi wa mkoa wamekua na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi ikiwemo Bodaboda, Wazee, Wafanyabiashara, Wanawake kwa lengo la kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.

 

Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2024 zinaogozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Kamati ya Mkoa wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024 zitakazofanyika katika Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akikagua baadhi ya maeneo alipotembelea Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024 zitakazofanyika Mkoani Kilimanjaro.Vijana wa Halaiki wakiwa katika mazoezi kwenye uwanja wa shule ya msingi Mwereni, uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024 zitakazofanyika katika Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akifuatilia vijana wa halaiki wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024 zitakazofanyika katika Uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Mkoani Kilimanjaro. Wa tatu kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Rajab.


 

 

Na Seif Mangwangi Mbarali


KUNDI kubwa la zaidi ya Ng'ombe 500 na punda3 wamekamatwa na askari wa Jeshi Usu la  Uhifadhi katika hifadhi ya Taifa  Ruaha Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya huku wamiliki wa mifugo hiyo wakikimbia .

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, shirika la hifadhi za Taifa Tanzania na Mkuu wa hifadhi ya Ruaha, Goodwill Meng'ataki amesema mifugo hiyo imekamatwa katika eneo la ukwaheri ndani ya bonde Oevu la Ihefu.

Akizungumza katika eneo ambalo mifugo hiyo imehifadhiwa baada ya kukamatwa, Meng'ataki amesema eneo hilo ambalo mifugo hiyo imekamatwa ni  katikati ya hifadhi ya Ruaha katika bonde la Ihefu mahala ambapo ni chanzo cha maji ya mto Ruaha mkuu.

Amesema baada ya kukamatwa kwa mifugo hiyo, walifikisha suala hilo Polisi na baadae katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali na tayari Mahakama imeshatoa hukumu ya kutaifishwa kwa mifugo hiyo nakuagiza iuzwe.

"Kwa kawaida tunavyokamata mifugo ndani ya hifadhi, tunawasiliana na Polisi na kuifikisha Mahakamani. Tayari Mahakama imetolea maamuzi mifugo iliyokamatwa na imeagiza iuzwe, tunasubiri wanunuzi ambao tayari wako njiani kuja hapa Ukwaheri kwaajili ya kununua,"amesema.

Amesema wafugaji katika bonde la Ihefu katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha,  wamekuwa wabishi kuelewa katazo la kutochungia mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo na wamekuwa wakitumia mwanya wa eneo hilo kuwa na maji mengi kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa na Askari wa Jeshi Usu la Uhifadhi.

" Kipindi hiki Kuna mvua nyingi zinanyesha ukanda huu, hawa wafugaji wamekuwa wakitumia mwanya huo huo kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yenye maji mengi wakijua Askari wetu hawawezi kufika huko, lakini tunajitahidi kukabiliana nao,"amesema.

Amesema changamoto nyingine ni Askari wake kukabiliana na wafugaji ambao wamekuwa wakitumia silaha za jadi ikiwemo mishale na mikuki pindi wanapokamatiwa mifugo yao wakitaka kuitorosha.

Afisa Uhifadhi daraja la pili na Mkuu wa Kanda ya Usangu, Abisai  Nassari amesema baada ya kukamata mifugo hiyo 547 na punda 3,  walitumia msaada wa helkopta kuisogeza  hadi katika eneo lenye maji machache ndipo askari wake wakaisogeza hadi eneo la ukwaheri.

"Tunashukuru Serikali ya Rais Mama Samia kutuletea vifaa vichache vinavyotusaidia kupambana na mifugo na majangili wa wanyamapori, tunaomba kuongezewa  vifaa zaidi ili tuweze kufanyakazi yetu kwa ufanisi zaidi,"anasema.

Anasema changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni namna ya kuwakabili wafugaji wanaoingiza mifugo katika bonde la Ihefu kwa kuwa eneo hilo ni chepechepe lililojaa matope kutokana na kuteremsha maji wakati wote.

Licha ya kundi kubwa kukamatwa na kutaifishwa, mwandishi wa habari hizi akiwa ndani ya Helkopta angani bado aliweza kushuhudia baadhi ya makundi makubwa ya ng'ombe wakiwa ndani ya eneo Oevu la Ihefu katika hifadhi ya Ruaha.


 


 

 

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Machi 28

KATIBU Tawala wilaya ya Kibaha , mkoa wa Pwani, Moses Magogwa amewaasa wananchi kujiepusha na ukataji miti kiholela na badala yake wajenge tabia ya kupanda miti na kuitunza kwani  ndio jawabu la kupambana na uharibifu wa mazingira.

Ameeleza hayo wakati Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilipofanya maadhimisho ya siku ya upandaji miti kata ya Kikongo, wilayani humo.

Magogwa akimuwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Nickson Simon John alieleza, kampeni ya kupanda miti Tanzania zilianza tangu mwaka 1999 , ambapo  ilionekana hali na kasi ya ukataji miti inaongezeka.

"Maana yake nini, kama jitihada hizi zisingewekwa mapema hali ingekua mbaya sana leo hii, na ndio maana leo tupo hapa kuendelea kuwa sehemu ya upandaji miti ili dunia yetu ibaki salama ," alisisitiza Magogwa.

Magogwa anaeleza, misitu ni ubunifu inabidi tutumie nishati mbadala ili kuachana na kuharibu mazingira .

"Mfano nikitazama mkoa wa Dar es salaam ndio Jiji linaloongoza kwa utumiaji wa mkaa huku bidhaa hizo zikitokea mkoa wa Pwani, tutaanda utaratibu maalum ikiwezekana Serikali ione haja ya kuongeza kasi kupeleka njia za mbadala mbalimbali ili maeneo mengine yasalimike katika kutunza misitu" alieleza Magogwa.

"Tunawajibu wa kupanda miti na kuifuatilia, hivyo ubunifu wetu ni kutafuta energy mbadala ili misitu yetu isiharibike, wenyeviti wote wa vijiji msiuze maeneo bila kufuata utaratibu, endeleeni kupokea maombi  ila taarifa zifike ofisi ya Mkurugenzi, atume wataalamu ili kujiridhisha"

Alieleza kwa utaratibu huo utasaidia kupunguza  pia matatizo ya migogoro ya ardhi  na ufyekaji wa maeneo ya misitu ambayo bado haipo kwa uangalizi wa TFS.

Hata hivyo, Magogwa aliipongeza TFS kwa kazi nzuri wanayofanya na wilaya itaendelea kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha misitu inabaki salama kwa manufaa ya nchi.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mkali Saidi Kanusu  aliwataka wanaccm na wananchi kuiga mfano huo bora ambao umeonyeshwa kwa vitendo na Ofisi ya mkuu wa Wilaya pamoja na TFS.




 

 



Usiku wa kuamkia leo Machi 28,2024 kumetokea ajali iliyohusisha mabasi mawili na roli la mafuta katika eneo la JKT Club karibu na Mlandizi mkoani Pwani.

Mabasi hayo ni Kampuni ya Sauli pamoja na New Force Taarifa zaidi za chanzo cha ajali hiyo na majeruhi zitatolewa baadaye leo na kamanda wa polisi. 

Endelea kutufuatilia kwenye page zetu Michuzi Tv, Michuzi blog kupata taarifa zaidi

 

Na.Abel Paul,Jeshi la Polisi- Arusha.

Jeshi la Polisi Nchini limesema machi 31,2024 Waumini wa Dini za Kikristo wataungana na wenzao Duniani katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka huku likibainisha kuwa limehimarisha ulinzi na usalama kuelekea sikukuu hizo.

 Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Msemaji  wa Jeshi la Polisi nchini Naibu kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Sherehe hiyo hutanguliwa na waumini wa dini hizo hukusanyika kwa wingi na kushiriki Ibada ambazo hufanyika nyakati za mchana na usiku,siku za Alhamis,Ijumaa,Jumamosi na Jumapili na Jumatatu ya Pasaka.

 Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kujiimarisha ulinzi na kuhakikisha kwamba ibada na sherehe hizo zinafanyika katika hali ya amani, utulivu na usalama wa kutosha ambapo amebainisha kuwa Jeshi hilo limejipanga kufanya doria katika mitaa na barabara zote kuu ili kuzuia uhalifu au uvunjifu wowote ule wa amani.

 Sambamba na hilo amesema katika barabara zote kuu, kutakuwa na doria za Askari ili kuzuia ajali za barabarani, Pamoja na kukagua watakao kiuka sheria za usalama barabarani kama vile kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, wakiwa wamelewa pombe na kujaza abiria kupita kupita kiasi.

 Msemaji wa Jeshi hilo amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Viongozi wa nyumba za ibada ambao watakuwa na ibada katika kipindi hiki cha Juma Kuu wasisite kuwasiliana na Viongozi wa Polisi katika maeneo yao ili washirikiane katika kuimarisha usalama kwa kipindi chote.

 Vile vile Jeshi hilo Pia linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuzingatia kanuni ya kiusalama inayosema “usalama unaanza na mimi mwenyewe”

 Pia Pamoja na hilo Jeshi la Polisi nchini limewataka wananchi kuchukua tahadhari na kujiepusha na marafiki wa mitandaoni na matapeli wanaojitangaza kuwa wanatoa mikopo kupitia mitandao.

Na Munir Shemweta, NZEGA


 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya Mji wa Nzega mkoa wa Tabora.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 27 Machi 2027 wilayani Nzega na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe, Japhet Hasunga wakati wa ziara ya Kamati yake kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji mradi wa LTIP kwenye halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.

 

Mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Mji wa Nzega umepewa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 na kuongeza alama za msingi za upimaji 14.

 

"Niwapongeze kwa kazi hii mlioamua kuifanya tangu tupate uhuru tumekuwa na changamoto za ardhi kuanzia kutambua, kupima, kurasimisha na kadhalika, kumekuwa na shida" amesema Mhe, Hasunga.

 

Amesema, Mhe, Rais ameamua kutoa fedha nyingi za mradi wa LTIP na Bunge kuidhinisha ambapo kwa upande wa halmashauri ya Mji Nzega kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 kimeidhinishwa kwa ajili ya Kata tano hivyo wananchi watumie fursa ya kutambuliwa maeneo yao na hatimaye kupatiwa hati kupitia mradi huo.

 

Ameeleza kuwa, Kamati yake ya PAC itakwenda kupima thamani ya fedha zilizopitishwa na Bunge pale tu wananchi watakapokuwa na hati.

 

"Msipopata hati hii mingine yote ni michakato, sisi hatuhitaji michakato tunataka kuona watu wangapi wana hati" alisema Mhe, Hasunga.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amesema, wizara yake ina uhakika michakato yote itakapokamilika katika mji wa Nzega hati milki za ardhi zitaenda kutolewa kwa wananchi.

 

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaenda kutoa jumla ya hati milki za ardhi 1,500,000 kwa maeneo yote yanayopotiwa na mradi.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameweka wazi kuwa, kazi iliyofanyika kwa halmashauri ya Mji wa Nzega kwa sasa imefikia asilimia 55 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni asilimia 39.

 

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unatekelezwa kwa mkopo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milionin150 kutoka Benki ya Dunia kwa kupindi cha miaka 5 katika halmashauri 58 nchini. Mradi huo unalenga kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga akisalimiana na waratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) alipowasili na Kamati yake kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi huo  Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Waziri Mhe, Geophrey Pinda wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.Sehemu ya washiriki wa ziara Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.

Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI) 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Familia ya Mzee Daudi Suleiman Ali, alipofika nyumbani kwake Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja kwa ajili ya kumsalimia na kumjulia hali yake leo 23-2-2024.(Picha na Ikulu) 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kukabiliana na hali ya ugumu wa maisha kwa kadri ya hali itakavyoruhusu, ili kuwapunguzia mzigo mzito wananchi wake.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu ya Pagali, Pemba alipozungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Rais Dk. Mwinyi amesema kupanda kwa gharama za maisha kunachangiwa na changamoto nyingi za uchumi duniani, zikiwemo, vita, kupanda bei kwa bidhaa za nje na baadhi ya mataifa duniani kuzuia kuuza bidhaa zao kwa mataifa mengine, akitolea mfano nchi ya India iliyozuia kuuza bidhaa zake kwa mataifa mengine duniani.


Alieleza, hali hiyo kuchangia kuzorotesha uchumi wa mataifa mengi na bei kupanda maradufu.


Aidha, alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya kila linalowezekana kustawisha uchumi na hali za wananchi kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuimarisha hali ya uchumi kwa wananchi.


Akizungumzia changamoto ya bandari ya Mkoani na hali ya kupanda kwa bei za bidhaa nchini, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wazee hao na wananchi wa kisiwa cha Pemba kwamba Serikali yao ina nia ya kuleta meli ya moja kwa moja kutoka bandari ya Mombasa hadi bandari ya Mkoani kwaajili ya kushusha bidhaa ili kuwapunguza gharama za maisha na mfumko wa bei za bidhaa hizo.


Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaomba wazee hao kuendelea kuiombea dua nchi ili amani iendelee.


Kwa upande wa wazee hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua kubwa ya Maendeleo ya nchi ilivyopiga ndani ya muda mfupi.


Aidha, wazee hao walipongeza hatua ya Serikali kuendelea kuwalipa pensheni jamii, na kumshukuru, Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaongezea kima cha pencheni hiyo.


Pia, wazee hao walitumia fursa hiyo kumpa pole Rais Dk. Mwinyi kwa msiba wa baba yake mzazi uliotokea hivi karibuni.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU, ZANZIBAR

Top News