Katibu wa NEC Idara ya Organaizesheni na Mlezi wa Jumuiya zote za Chama Cha Mapinduzi Ndg. Issa Gavu amefunga Mafunzo Maalum kwa Viongozi wanawake Kutoka mikoa 9 ya Kanda ya ziwa na kanda ya ziwa Magharibi.

Comred Issa Gavu amefunga mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya ya wanawake Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa UWT Ndg. Mary Chatanda yaliyofanyika Mkoani Mwanza .

Lengo la Mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wanawake namna ya kuchochea Maendeleo ya Nchi na kuleta ufanisi wa Utendaji kazi katika Jamii na kujikwamua Kiuchumi.

Comred Issa Gavu amewasihi Viongozi wanawake waendelee kuunga Mkono Juhudi za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye ndiyo Mfano mzuri wa wanawake wote wanao onyesha kwa vitendo kujikwamua kiuchumi na ufanisi mzuri wa kazi, na yeye ndiye anawawakilisha katika ngazi ya Juu ya Uongozi wa Nchi.

Mafunzo hayo yaliyofungwa Mkoani mwanza katika Ukumbi wa Winterfell yamehusisha viongozi kutoka Mikoa ya Mwanza, Kagera, Katavi,Shinyanga, Simiyu,Geita, Kogoma,Tabora na Mkoa wa Mara leo Tarehe 27 Machi 2024.







Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAKAMU  wa Rais wa Dkt. Philip Mpango amewaita wawekezaji wa Kimataifa kuja nchini kuwekeza kutokana na  mazingira bora zaidi yanayovutia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji yanayotokana na  sera, utulivu, rasilimali na jiografia.

Dkt.Mpango ametoa mwito huo Machi 27,2024 wakati akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo ameyataja baadhi ya maeneo yenye fursa za uwekezaji ikiwemo afya, elimu na miundombinu na kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi.

Kongamano hilo ambalo pia limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali nchini, limejumuisha zaidi ya makampuni mia mbili, sitini yakiwa ni kutoka Mkoa wa Zhejiang nchini China, arobaini yakiwa ni makampuni ya China yaliyowekeza nchini, na makampuni zaidi ya mia moja yakiwa ni kutoka Tanzania.

Kuhusu uwekezaji, Dk Mpango amezisifu kampuni na wafanyabiashara kutoka China kwa kuendelea shiriki maendeleo ya uchumi nchini kupitia uwekezaji wao huku akitoa takwimu mbalimbali za kuongezeka kwa mapato na uchumi.

Ambapo ameeleza katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2023, kituo cha Uwekezaji Tanzania( TIC) kilisajili zaidi ya  kampuni 256 kutoka China, yakiwa na uwekezaji wa takribani Dola za Marekani bilioni B4.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema uukiifuatilia historia ya ushirikiano kati ya Tanzania na China pamoja na uhusiano wa kidiplomasia ambao leo unatimiza miaka 60, hivyo wao Wachina na Watanzania ni ndugu.

Amesema kuwa maendeleo makubwa ya utulivu pamoja na uongozi madhubuti wa Serikali, wafanyabiashara wengi wa China wamevutiwa kuja kuwekeza Tanzania, na zaidi mapokezi wanayopata yanawafanya waendelee kushiriki 

Pia amesema Tanzania ni kiungo muhimu katika ushirikiano kati ya Afrika na China, na hivi Karibuni, Rais Xi Jinping aliweka bayana kuwa Uhusiano wa China na Tanzania  ni ushirikiano namba moja kwa viwango ikilinganishwa na mahusiano mengine ya nchi mbili kati ya China na nchi za Afrika.

"Tuna matarajio makubwa ya Maendeleo ya ushirikiano wa Tanzania na China, ambao misingi yake imejengwa kwenye historia, ujenzi wa ushirikiano wa kiuchumi unaoendelea na urafiki wa kuamainia."

Awali Katibu wa  Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa serikali ya Jinhua nchini China Zhu Chonglie amesema wao kama Mkoa wa Zhejiang, na Serikali yao ya Jiji la Jinhua kama ilivyo katika maeneo mengine ya China na Tanzania wanashiriki kuadhimisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60.

"Mfano mzuri ni Kongamano kubwa la elimu liliratibiwa na chuo chetu cha Zhejiang (Zhejiang Normal University Tanzania China Education Forum)."

Akieleza zaidi amesema elimu ni moja ya maeneo yaliyowasaidia  pamoja kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria ambao unapaswa kuuendelezwa, na ndio maana chuo chao  cha Zhejiang kimewekeza zaidi kwenye mabadilishano ya kielimu na vyuo mbalimbali vya elimu barani Afrika.

Amefafanua mfano mzuri ni  Tanzania  katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia ujenzi wa Taasisi ya Confucius na maktaba Kuu.

Kwenye upande wa Utamaduni pia, amesema Jiji lao na Mkoa mzima wa Zhejiang, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupokea vikundi mbalimbali vya maonyesho ya Utamaduni lakini pia vikundi vya Tanzania vimefika Zhejiang kubadilishana uzoefu.

"Hata ujio wetu hapa kwa ajili ya Kongamano hili la Uwekezaji ni matokeo ya ushirikiano wa kihistoria uliopo lakini na ukuaji unaoendelea, tunapaswa kuutunza kupitia mabadilishano kama haya ya kiuchumi, watu na watu pamoja na kubadilishana uzoefu wa masuala la kisiasa."

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde ametumia nafasi hiyo kuelezea fursa mbalimbali zilizopo nchini na hasa akijikita kuzungumza kuhusu sekta ya uwekezaji ambapo amewaomba wawekezaji kutoka China kuwekeza katika kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema takwimu za sensa ya Watu na Makazi inaonesha Dar es Salaam kuwa na watu wengi na wataendelea kuongezeka hivyo wingi wa watu unapaswa kuwa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. 

Amefafanua Moja ya changamoto ni Makazi hivyo wakati umefika wa kujengwa kwa majengo makubwa kwa kubomoa baadhi ya nyumba zilizopo akitolea mfano baadhi ya nyumba za Kiwalani na Karakata.

"Idadi kubwa ya watu maana yake Makazi ya kuishi yanahitajika , hivyo changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kujengwa majengo makubwa marefu na kisha wananchi wakaishi na huenda ikasaidia kuondoa changamoto ya nyumba kumezwa na  mafuriko.

Pia amesema Dar es Salaam kumekuwa na takataka nyingi, hivyo ni vema kuwa na mfumo utakaowezesha kutabadilisha taka hizo kuwa bidhaa huku akifafanua tayari Kuna Wachina wameanzisha viwanda vidogo kwa ajili ya kubadilisha taka hizo kuwa bidhaa 

Chalamila amesema katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya barabara za mwendokasi kazi,amesema huko nako kuna fursa ambapo wawekezaji wanaweza kuingia ubia na Serikali ya Mkoa na kujenga barabara ambazo watumiaji watakuwa wakilipia na hivyo kuingiza fedha kwa pande zote mbili.










RAIS Samia Suluhu Hassan ameendelea kutajwa kupitia majukwaa mbalimbali kutokana na jitihada zake za kuboresha uchumi wa Taifa katika sekta mbalimbali na katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake amefanikiwa kuongeza fursa hasa za ushiriki wa sekta binafsi na kupanua wigo wa ukuaji wa uchumi nchini.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi nchini, Prof. Samwel Wangwe wakati wa mdahalo maalum ulioandaliwa na kampuni ya Mchambuzi Media kwa lengo la kutathmini miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.

Ameeleza kuwa, Rais Samia amejipambanua kama mlezi wa sekta binafsi na amekuwa na mikutano ya mara kwa mara na sekta hiyo ambayo inalenga kuwekana sana katika masuala ya kupanua wigo wa ukuaji wa uchumi na wanaoshiriki katika ukuaji huo.

"Pia Rais Samia amefanikiwa kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo, ameongeza mahusiano ya kiuchumi kuanzia nchi jirani hali iliyofanya wawekezaji kutoka nje kuongezeka na kusababisha uchumi kukua kwa kasi," amesema.

Pia amesema kati ya maeneo ambayo yalilega kiuchumi wakati Rais Samia anaingia madarakani ni pamoja na eneo la utalii ambalo alilitilia mkazo na kuongoza filamu ya Royal Tour iliyosaidia kuongezeka kwa watalii kutoka 700,000 hadi kufikia Milioni 1.8.

Kwa upande wake Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Kiuchumi, Kijamii, Kitaifa na Kimataifa, Dk. Denis Muchunguzi amesema katika kuangalia miaka hiyo mitatù ya uongozi wà Rais Samia ni muhimu kuundwa kwa tume au kuweka utaratibu ambao utawasaidia na kuwaongezea nguvu wakuu wa Mikoa ,Wilaya na Wakurugenzi kuwa na uwezo wa kutatua kero za wananchi.

“Tusisubiri mpaka aende Makonda kutatua kero, uwekwe utaratibu utakaowaongezea nguvu na uwezo kwa wakuu wetu wa mikoa,Wilaya na Wakurugenzi ili kuweza kusikiliza na kutatua kero za wananchi, " amesema Dk. Mchunguzi.

Aidha Mkurugenzi wa Kampuni ya Mchambuzi Media ambao ndio waandaaji wa mdahalo huo, Salehe Mohamed amesema mdahalo huo umelenga kuangalia maeneo ambayo Rais Samia amefanya vizuri na yale ambayo hajafanya vizuri na nini kifanyike kupiga hatua ili maisha ya watanzania yaendelee kuwa bora zaidi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia amefanikiwa kuinua sekta ya kilimo ambayo katika miaka ijayo itaifanya nchi kuwa na uchumi imara zaidi.

"Rais amefanikiwa pia katika sekta ya elimu tumesikia wakati anaingia madarakani udahili wa wanafunzi ulikuwa haujafika hata 10,000 ila sasa hivi umefikia 17,000, eneo jingine ni sekta afya yaani sasa hivi karibu kila wilaya kama siyo Zahanati basi kuna hospitali kuna na vifaa vya kisasa ambavyo vinawafanya watanzania kupata matibabu kwa kiwango cha hali ya juu," amesema Mohamed.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF,) Bakari Machumu akichangia mada wakati wa jukwaa hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam.


 

Matukio mbalimbali wakati wa jukwaa Hilo.

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WANAJUKWAA wasichana kutoka vyuoni (Young Feminist Forum) wameiomba Serikali kutilia mkazo kwenye vipaumbele mbalimbali katika mwaka wa fedha ujao ambavyo ni vilio kwa jamii kubwa ya watu nchini kwa kutenga bajeti na kufanya ufatiliaji ili fedha zinazotengwa kufanya kusudi maalumu iliyopangiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 27,2024 katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mabibo-Dar es Salaam Mwanaharakati wa masuala ya jinsia Bi.Anna Sombe amesema wamejadili mambo katika suala la pembejeo za kilimo,bima ya afya,Mikopo ya Elimu ya vyuo vikuu,pamoja na miundombinu ya nishati na maji.

Aidha Bi.Anna amesema kwa upande wapembejeo za kilimo ambapo kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu zinatakiwa kufika kwa wananchi kwa wakati na kuondokana na desturi ya ucheleweshwaji ambao huchangia kuzorotesha uzalishaji wa mazao jambo ambalo linaendeleza njaa.

Pamoja na hayo Bi.Anna ameeleza kuhusina na suala la bima ya afya kwa watu wote kupewa kipaumbele kulifanya kuwa hitaji la lazima kwa watu kwa lengo la kuboresha afya za watu wote bila kujari hali zao za maisha.

Vilevile Bi.Anna amesema miundombinu ya nishati na maji ni jambo la msingi na ni hitaji la kila siku hivyo serikali inatakiwa kutilia nguvu masuala hayo ili kuboresha maisha ya wananchi.

"Serikali iweke nguvu sio kutenga bajeti tu ufuatiliaji na utekelezaji pesa imeweka kwaajili ya ujenzi mabomba je yamewekwa unakuta watu wanafanya upigaji au wanazitumia pesa vinginevyo"Bi Anna amesema.

Kwa Upande wake Mdau wa semina za Jinsia Bi.Raiyan khatib ameiomba serikali kutoa kipaumbele Cha huduma bure kwa mama na mtoto pamoja na tiba bure ya saratani ya mlango wa kizazi.

"Unakuta mzazi amefika kipindi Cha kujifungua kama vile anamnunua mtoto Kuna huduma kule anatakiwa alipe,Kuna vifaa anaambiwa toka nenda kanunie vifaa kwenye duka la nje"Bi.Raiyana amesema.











Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Alhaji Mustafa Rajab Shaban kwenye picha na Watoto Yatima Shuraiya Ramadhan, Dhul-kaya Ramadhan pamoja na Ikramu Selemani wa Kituo cha Watoto Yatima cha Rahman kilichopo Chang’ombe Jijjini Dodoma mara baada ya kufuturu Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimpakulia Iftar mtoto Yatima Shuraiya Ramadhan (6) wa Kituo cha Watoto Yatima cha Rahman kilichopo Chang’ombe Jijjini Dodoma. Rais Samia aliwaandalia Iftar Viongozi pamoja na Wageni mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimpa Futari mtoto Yatima Shuraiya Ramadhan (6) wa Kituo cha Watoto Yatima cha Rahman kilichopo Chang’ombe Jijjini Dodoma. Rais Samia aliwaandalia Iftari Viongozi pamoja na Wageni mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Iftar aliyowaandalia Viongozi pamoja na Makundi mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amebeba Kombe la Ubingwa wakati wa picha ya pamoja na Vijana wa Ramadhan Brothers ambao waliibuka washindi wa shindano la America’s Got Talent (AGT) mara baada ya Iftar Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiitikia Dua mara baada ya kupata Iftar aliyowaandalia Viongozi pamoja na Makundi mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.



Baadhi ya viongozi wa Dini wakiwa kwenye viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma kwa ajili ya Futari iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 27 Machi, 2024
Wageni mbalimbali wakiwa kwenye Futari iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.

Mapacha wa Mtume Qaswida Hassan na Hussein wakitumbuiza wakati wa Iftar Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024. Mapacha wa Mtume Qaswida Hassan na Hussein wakitumbuiza wakati wa Iftar Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Machi, 2024.

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kukuza uchumi wa Sekta binafsi inayochangia makusanyo ya kodi ambazo zitawezesha ujenzi wa miundombinu ya barabara na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.

Bashungwa amezungumza hayo Machi 27, 2024 katika kikao kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Wilaya ya Karagwe pamoja na Taasisi za Serikali zinazowahudumia ambapo amesikiliza kero zao ikiwemo tozo kubwa za kodi, ushuru pamoja na kauli zisizoridhisha kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Bashungwa amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato unawezesha Serikali kufanikisha malengo yake ya kuhudumia nchi pamoja na wananchi wake kwa haraka kwa kuwa wajibu wa Serikali ni kujenga ustawi wa wafanyabiashara na sio kuwadumaza.

“Sijafurahishwa na madai ya kauli za Maafisa kwa wafanyabiashara ambazo sio sahihi,kwa kuwaaambia wakishindwa kulipa kodi, wafunge baishara, Lengo la Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kwa kutoa elimu, kuwashauri na kustawisha wafanyabiashara” amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kagera kusimamia miongozo pamoja na kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za kodi mara kwa mara kwa wafanyabiashara pamoja na Maafisa kuwa na kauli nzuri na wezeshi.

Bashungwa amelitaka Baraza la wafanyabiashara la Wilaya ya Karagwe kutimiza wajibu wao kwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na wafanyabiashara wote ili kukumbushana masuala tozo mbalimbali zilizopo na kutatua changamoto zao kwa kuzipatia suluhu ya haraka kabla mfanyabiashara hajafikia hatua ya kufunga biashara.

Kuhusu utekelezaji wa miundombinu, Bashungwa amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa barabara ya Bugene-Benaco (km 128.5) pamoja na kuanza utekelezaji wa barabara ya Omurushaka - Kyerwa (km 50) na Omugakorongo – Kigarama - Murongo (Km 111) kwa kiwango cha lami.

Naye, Mfanyabiasha wa Kampuni ya SANOA, Bw. Metisela Philipo, ameeleza kuwa kodi na faini wanazotozwa zimekuwa kubwa na haziendani na biashara wanazozifanya hivyo kupelekea baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Bw. Omary Kigoda amesema kuwa suala la lugha mbaya kwa walipa kodi sio msimamo wa Taasisi hivyo TRA itaendelea kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe, Paschal Rwamugata amesema kuwa moja ya majukumu ya Chama ni kusikiliza kero za wananchi na kuitaka Serikali kutatua kero hizo kama ambavyo imekuwa ikifanya.







Top News