Mkoa wa Singida umezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo wa Saratani la mlango wa uzazi kwa wasichana mwenye umri kati ya miaka Tisa hadi 14 ambapo Wasichana 178, 114 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo mkoani humo.

Akizindua zoezi la utoaji wa Chanjo hiyo katika Kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida, Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego (leo 22-Apr-2024 ) amewaagiza Maafisa Afya wahakikishe maeneo yote yaliyoandaliwa kutolewa huduma hiyo ya chanjo yanafanya hivyo kwa viwango vya juu ili kuwalinda watoto wa kike na saratani hiyo hatari.

Halima Dendego amesisitiza kuwa chanjo hiyo pia ni lazima iwafikie wanafunzi wanaosoma kwenye shule binafsi na watoto wa kike ambao wanaishi mitaani nao wapate fursa ya kupata chanjo hiyo ili kuwakinga na saratari na mlango wa uzazi.

“Tunapoenda kuwalinda watoto wa kike kwa kuwachanja chanjo hiyo maana yake tunawaepusha na madhara ugonjwa wa saratani ili wasije wakaambuzi wavulana”Ameeleza Halima Dendego.

Amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni muhimu kwa wasichana na inatolewa bure kwa sababu Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo imegharamia chanjo hiyo, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ili kuwaepusha na madhara yanayoweza kutokea.

Naye, Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Victorina Ludovick amesema kwa Tanzania chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ilianza majaribio mwaka 2014 mkoani Kilimanjaro na kupata mafanikio makubwa kwa kuwakinga wasichana wasipate ugonjwa huo.

Dkt Victorina Ludovick ameeleza mtu yeyote anaweza kuambukizwa saratani hiyo katika umri wowote ule hasa wakati wa tendo la ndoa na inaweza kusababisha magonjwa mengine ikiwemo saratani ya koo na magonjwa mengine ya via vya uzazi kwa wanamke na wanaume.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt Fatuma Mganga amewataka Maafisa Afya wanatoa chanjo hiyo kuhakikisha wanafanikisha zoezi hilo kwa viwango ili mkoa wa Singida uwe wa kwanza katika utoaji wa chanjo hiyo kwa wasichana mwenye umri wa miaka Tisa hadi 14.

Amesema saratani hiyo inaua na ni ugonjwa hatari hivyo ni muhimu kwa watoto wote wenye umri wa kupata chanjo wapewe chanjo hiyo kutokana na umuhimu wake katika kulinda afya zao.

Nao, Mashuhuda waliopewa chanjo hiyo wakizungumza kwenye uzinduzi wa utoaji wa chanjo ya satarani la mlango wa uzazi katika kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida Lukuresia Andrea na Salisabila Athumani wote wakazi wa mkoa wa Singida wamesema tangu wapatiwe chanjo hiyo hawajapata madhara yeyote hivyo wameomba wazazi na walezi wasiwauzie watoto wao wa kike kwenda kupata chanjo hiyo kwa sababu inafaida kubwa katika maisha yao.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick akimchoma sindano ya chanjo mwanafunzi wa shule ya msingi Kisaki
 

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi
 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Victorina Ludovick akisoma taarifa ya utoaji wa chanjo katika mkoa wa Singida
 

Wanafunzi kutoka Shule mbalimbali waliohudhuria zoezi la utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi katika kijiji cha kisaki.
 

Wanawake waliopata chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi Mkoani Singida wakiwa na watoto wao

NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

MBUNGE wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mgawanyo wa fedha zinazotolewa na serikali katika tarafa mbalimbali ndani ya wilaya ya Rombo haufanywi kwa upendeleo bali kwa kuzingatia uhitaji katika kila eneo.

Pia amesema kwa kipindi Cha miaka 3 , serikali imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilayani hiyo ikilinganishwa na kipindi cha Miaka 10 iliyopita.

Profesa Mkenda alisema hayo wakati akifanya mkutano wa ndani na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya CCM kutoka katika Tarafa ya Mengwe kuelezea maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita wilayani Rombo kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia mgawanyo huo wa fedha zilizotolewa na serikali kupitia halmashauri kwa kipindi cha miaka 3 Profesa Mkenda amesema , Tarafa ya Mkuu ilipata kiasi Cha bilioni 3.8, Mengwe bilioni 3.558, Tarakea bilioni 2.3 , Useri bilioni 2.419 huku Mashati ikipata zaidi ya kiasi Cha shilingi milioni 903.



Na WAF - Mwanza

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema dozi Moja ya chanjo ya HPV inatosha kumkinga msichana kupata ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo hiyo.

Waziri Ummy amesema hayo leo Aprili 22, 2024 kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Dozi moja ya chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 iliyozinguliwa katika viwanja vya Furahisha Wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza.

“Wataalamu wetu ambao wanatoka kwenye Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) wametuhakikishia kuwa dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kumkinga msichana kupata Saratani ya Mlango wa Kizazi”. Amesema Waziri Ummy

Amesema, awali dozi zilizokuwa zinatolewa mbili, ya kwanza inatolewa leo na baada ya miezi Sita inatolewa nyingine hii ilikua inapelekea mabinti wengi kutorudi kupata dozi ya pili, Sasa hivi tumeamua kutoa dozi moja ya HPV kwa kuwa inatosha kuwakinga wasichana kuja kupata maambukizi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.

Aidha, Waziri Ummy amesema Saratani inayoongoza kuwatesa Watanzania ni Saratani ya Mlango wa Kizazi ambapo amesema katika kila wagonjwa 100 wanaougua Saratani, wagonjwa 23 ni wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi.

“Inafuata Saratani ya mfumo wa chakula asilimia 11, Saratani ya Matiti asilimia 10.4, Saratani ya tezi dume asilimia 8.9 kwa hiyo ukiaangalia hapo Saratani inayoongoza ni Saratani ya Mlango wa Kizazi”. Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy ametoa wito kwa wazazi na walezi wote nchini, kuhakikisha watoto wanapata chanjo zote wanazopaswa kupata kwa kuwa lengo kubwa la chanjo ni kuwakinga na magonjwa yakiwemo haya ya Saratani pamoja na kuwakinga na vifo vinavyoweza kuzuilika na chanjo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. Saidi Mtanda amesema watahakikisha watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka 9-14 wanapata chanjo hiyo ili kufikia malengo.

“Kwa mwaka 2022/23 Mkoa wa Mwanza ulifanikiwa kuchanja watoto zaidi ya laki Mbili sawa na asilimia 107 kati ya walengwa waliotarajiwa kuchanjwa ni laki 191,440 wenye umri chini ya Mwaka Mmoja, tumefikia malengo na kuyavuka”. Amesema Mhe. Makilagi

















*Jiji la DSM lafanya Hafla ya Maombi na Dua ya Kuliombea Taifa

KTIKA kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 22, Aprili 2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeandaa Maombi na Dua ya kuliombea Taifa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam yalioambatana na kauli mbiu isemayo “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa maendeleao ya Taifa Letu”.

Akiongoza hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “ tumeandaa Maombi na Dua ya kuliombea Taifa letu ikiwa ni sehemu ya Kumshukuru Mungu kwa kufikisha miaka 60 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa amani kwani kama Taifa tumeshikamana na tumeimarika kwa miaka 60 hivyo hatuna budi kufanya Maombi na Dua kwaajili ya kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu”.

Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameendelea kusema “katika maombi na Dua hizi tunaendelea kumuombea Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuendelea kuimarisha Muungano kwa amani pamoja na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kupata maendeleo bila kusahau kuombea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaoenda kufanyika Octoba 2024 ufanyike kwa Amani na tupate viongozi bora zaidi watakaoendelea kutuletea maendeleo.”

Kwa upande mwingine Mhe. Mpogolo amewahakikishia Wananchi wa Wilaya ya Ilala kutatua changamoto ya Athari za mvua kwani tayari ashawaelekeza wataalamu kutoka TARURA wakiambatana na Wahandisi kutoka Jiji la Dar es Salaam kutambua maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua ili pindi mvua zitakapopungua maeneo hayo yatafanyiwa marekebisho.

Aidha kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomary Satura ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini kuliombea Taifa letu huku akiwahakikishia kushirikiana na watendaji wake kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Ilala kama Mheshimiwa Rais anavyoelekeza.

Akitoa Shukrani zake kwa viongozi wa Dini walioshiriki kuliombea Taifa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto ameeleza kuwa “kupitia Maombi na Dua hizi za kuliombea taifa kufikisha miaka 60 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni Imani yangu maombi haya yatadumisha Amani na yatakuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu”.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Ilala Adam Mwinyipingu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuandaa siku ya Maombi na Dua ya kuliombea Taifa kwaajili ya muungano kwani maombi haya ni sehemu ya uzalendo pamoja na mshikamano kwa viongozi huku akiahidi kusimama na kuimarisha Muungano wa Tanzania kupitia Dua na Sala ili nchi iendelee kuwa na amani.
Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rose Rwakatale (aliyevaa nguo ya bluu) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba msaada wa tani tano za vyakula kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wa Jimbo la Mlimba mkoani.Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo Aprili 22,2024 kwenye ofisi za Mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Zahra Michuzi akiwa na wanafunzi wa shule ya St Mary’s mara baada ya kukabidhiwa msaada wa mchele kwa waathirika wa mafuriko Mlimba mkoani Morogoro leo Aprili 22,2024
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi  St. Marys Mlrogoro baada ya kupokea msaada huo wa chakula kwa ajili ya waathirika wa mafuriko jimbo la Mlimba leo Aprili 22,2024.
Wanafunzi wa St Mary’s Ifakara wakimkabidhi msaada wa tani tano za chakula Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba uliotolewa na Mwenyekiti wa CCM Wazazi Mkoa wa Morogo (Kulia) Dkt. Rose Rwakatare.
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rose Rwakatare ametoa msaada wa tani tano za mchele kwa waathirika wa mafuriko wa jimbo la Mlimba mkoani Morogoro.

Dkt. Rose amekabidhi msaada huo leo Aprili 22, 2024 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba katika hafla ambayo imefanyika ofisini kwake.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Dkt. Rose amesema amezaliwa Mlimba hivyo ameguswa sana kuona wananchi wenzake wanaishi maisha ya shida....“Mimi ni mzaliwa wa Mlimba, kwa hiyo hapa ni nyumbani kwangu ndiyo maana nimeamua kuja kulia na wanaolia, tufarijiane wakati huu mgumu, sijaja bure nimekuja na mifuko 1,000 ya mchele angalau wapate chakula,” amesema

Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ujumbe kupeleka msaada wa vitu mbalimbali na kuwaomba wadau mbalimbaali waendelee kupeleka msaada.

“Hata ukiwa na mfuko mmoja wa mchele, unga unakaaribishwa kuja kusaidia watanzania wenzako, sisi ni watanzania na tunajulikana dunia nzima kwa upendo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba amemshukuru Dkt. Rose Rwakatare kwa upendo aliouonyesha kwa wakazi wa Mlimba na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano huo na kwenda kutoa misaada.

Amesema msaada huo umekuja wakati mwafaka kwani wananchi wa maeneo yaliyoathirika na mafuriko wanahitaji faraja na kushikwa mkono wakati huu.

“Napenda kutoa wito kwa viongozi wengine na wafanyabiashara waige mfano wa Dkt. Rwakatare waje kusaidia wananchi ambao wako kwenye wakati mgumu wakati huu,” amesema

Naye, Mohamed Msuya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero amempongeza Dkt. Rose kwa msaada alioutoa kwa wananchi hao na kusema kuwa msaada huo ni wa kuigwa na wa mfano kwa wananchi wa wilaya ya Kilombero bila kujali itikadi za kisiasa.

“Tumpongeze sana Dkt. Rose kwa kuwa na maono ya kuwasaidia wananchi wa Kilombero, kutoa ni moyo wala siyo utajiri kwasababu kuna watu wana vingi lakini hawana moyo wa kutoa,” amesema

“Nawaomba sana watanzania wote bila kujali itikadi kujitokeza kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mlimba waliopata shida ya mafuriko na tutampa ushirikiano wa kutosha yeyote atakayeleta msaada,” amesema

“Dkt Rose Rwakatare ni mfano wa kuigwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kilombero, huyu ana moyo wa kipekee kwasababu kila linapotokea tatizo amekuwa msaada mkubwa kwenye Wilaya ya Kilombero,” amesema Msuya

Amesema kuna watu wanataka kutoa msaada lakini wanaogopa kutokana na sababu za kisiasa hivyo amewatoa hofu kwamba wajitokeze kusaidia kwani CCM na Serikali zitawalinda kwa kuwa siasa ni mpaka 2025.

“Kwa sasa hakuna siasa hapa tunaamini tuna madiwani na wabunge lakini tuko kwenye utendaji hatuko kwenye siasa kwa hiyo Dkt. Rose najua una marafiki huko mjini, wewe ni Mwenyekiti wa Wazazi CCM mkoa wa Morogoro, unawadau wengi tunajua unauwezo wa kuhamasisha wananchi wakaja kuleta misaada,” ameongeza
Na. Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ambaye ni Mwenyekiti wa TNCM ameongoza Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Jengo la Tume ya Ushindani Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Aprili, 2024 na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalaum, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Medical Stores Department (MSD), Local Fund Agent (LFA), Sekretarieti ya TNCM, Asasi za Kiraia (Non State Actors - NSAs) na Wadau wa Maendeleo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiongoza Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026. Mkutano ulifanyika ukumbi wa Jengo la Tume ya Ushindani Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Aprili, 2024.Kushoto ni Mwenyekiti wa TNCM Bw. Kent Pius na wa kwanza kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TNCM Bw. Godlisten Moshi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (kulia) akiteta jambo na Katibu Mtendaji wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) Bw. Kent Pius wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM),ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) wakifuatilia mkutano huo ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026. Mkutano ulifanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Aprili, 2024.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akisalimiana na Mwenyekiti wa TNCM Bw. Kent Pius wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026. Mkutano ulifanyika ukumbi wa Jengo la Tume ya Ushindani Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Aprili, 2024.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akisalimiana na Afisa Mratibu Uzingatiaji na Taratibu katika Utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia unaolenga Kupambana na UKIMWI, KIFUA KIKUU, MALARIA na Uboreshaji wa Mifumo na Miundombinu ya Afya (RSSH) Tanzania Bw. Denis Eliasaph wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) Dar es Salaam
Mwakilishi wa Meneja Mpango wa NASHCOP Bw. Ambwene Mwakalobo akiwasilisha kuhusu Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya ngoni na Homa ya Ininwakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM).
Mkuu wa Dawati la Uimarishaji wa Mifumo ya Kutolea Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hussein Athumani akiwasilisha wasilisho la Resilient and Sustainable Systems for Health (RSSH) wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM).
Mwenyekiti wa TNCM Bw. Kent Pius akizyngumza wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.

Mkuu wa Program Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachime, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ulilenga kujadili mikakakati mbalimbali itakayoongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Programu za Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na John Mapepele

Serikali imesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na Simba, Nyati na Chui wengi katika bara la Afrika huku ikishirikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa yaTembo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 22, 2024 kwenye mkutano ambao Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ametangaza rasmi matokeo ya Sensa ya Wanyamapori na kuzindua taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023.

Sensa hiyo ya wanyamapori imefanywa na TAWIRI kwa kushirikiana na TANAPA, TAWA, NCAA, Idara ya Wanyamapori, na Frankfurt Zoological Society katika mifumo ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi,Saadani-Wamimbiki na Serengeti 

Mkutano huo uliwahusisha wadau wa uhifadhi na utalii, ambapo Mhe. Kairuki amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wanyamapori nchi nzima mapema hapo mwakani.

 Aidha, Mhe. Kairuki amesema matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kwenye usimamizi wa wanyamapori nchini na kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha  uhifadhi na  kutangaza  utalii duniani.

Mhe. Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali ambapo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) kuandaa mpango kazi kwa ajili ya sensa ijayo huku pia akielekeza watendaji wa wizara yake kuchambua kwa kina  matokeo ya sensa hii  ili yaweze kuleta tija.
.

Akitoa taarifa ya sensa hiyo amesema spishi zilizoonyesha idadi kubwa ni pamoja na Nyati (59,878), Tembo (20,006), Nyumbu (19,060), Kongoni (18,361), swalapala (14,031) na Ngiri (13,806), ambapo spishi zilizoonyesha idadi ndogo ni pamoja na Twiga (1,679), Tandala mkubwa/ kudu (1,414) na puku/sheshe (496). 

Amefafanua kuwa kwa upande wa Tembo, idadi imeongezeka kutoka 15,501 (2018) hadi 20,006 (2022) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa hadi 0.8% mwaka 2022 ikilinganishwa na 16% wakati wa sensa ya 2018. 

Akizungumzia kuhusu taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023 amesema Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia na umeendelea kuimarika baada kuathiriwa na mlipuko wa janga la UVIKO-19. Mwaka 2023 sekta ya utalii duniani imeimarika kwa kiwango cha asilimia 88 ikilinganishwa na kiwango cha juu kilichofikiwa mwaka 2019.

 “Hali hii ilitokana na ukuaji endelevu wa maendeleo ya teknolojia na juhudi za kukuza na kuendeleza maeneo mengine ya utalii duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa asilimia 34 hadi kufikia watalii bilioni 1.3 Mwaka 2023 kutoka milioni 960 Mwaka 2022”. Ameongeza

Amesema kwa Tanzania, utalii wa Kimataifa umeimarika kwa kiwango cha asilimia 118.4 Mwaka 2023 ikilinganishwa na kiwango cha juu kabla ya janga la UVIKO-19.  Aidha, idadi ya watalii wa Kimataifa iliongezeka kutoka watalii milioni 1.4 Mwaka 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.8 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 24.3. 

“Hatuna budi kutambua kazi kubwa aliyoifanya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeitangaza Tanzania kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour”. Amesisitiza  

Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii hapa Nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilifanya utafiti wa watalii wanaoondoka Nchini Mwaka 2023 kwa lengo la kupata taarifa zinazosaidia kutunga Sera na kuandaa mipango ya maendeleo ya utalii. Aidha, taarifa za utafiti huo zinasaidia serikali kuandaa akaunti za taifa (national accounts) na mizania ya malipo ya nje (Balance of Payments). 

Aidha amesema utafiti umebainisha kuwa mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 33.5 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani 2.5 bilioni zilizopatikana Mwaka 2022.  Aidha, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 250 Mwaka 2023 kutoka wastani wa Dola za Marekani 214 Mwaka 2022. 

Kwa upande wa Zanzibar, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku ulikuwa Dola za Marekani 257 Mwaka 2023 ikilinganishwa na watani wa Dola za Marekani 218 Mwaka 2022.
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

BENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. Mil. 120 kudhamini Mkutano Mkuu wa 38 wa Mwaka wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT Taifa), unaofunguliwa Jumanne Aprili 23 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ukiwakutanisha washiriki zaidi ya 600.

Kiasi hicho kinachodhamini mkutano wa mwaka huu unaofanyika chini ya kaulimbiu; ‘Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Jambo Letu; Shiriki kwa Maendeleo ya Taifa,’ kinafanya udhamini wa NMB kwa ALAT Taifa kufikia Sh. Bil. 1.2 katika kipindi cha miaka nane.

Mkutano Mkuu wa ALAT, unaowapa fursa viongozi wa Serikali Kuu kutoa Maelekezo na Miongozo ya Kisera kwa Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wakiwemo Mameya wa Majiji na Manispaa, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmshauri 184 (za Tanzania Bara), utafungwa Aprili 25 na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa miaka nane sasa, NMB na ALAT zimekuwa na ushirikiano endelevu katika masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Halmashauri zote nchini, ikiwemo kudhamini na kufanikisha vikao na Mikutano Mikuu ya Mwaka ya ALAT, ambayo kimsingi ndio chachu ya utendaji bora kwa Halmashauri hizo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, iliyofanyika Golden Tulip Zanzibar Airport Hotel, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema wanajivunia kuwa wabia wakubwa wa ALAT, na kwamba wanathamini heshima ya kipekee wanayopewa na uongozi wa jumuiya hiyo.

“NMB tunajivunia ubia baina ya benki yetu na Jumuiya hii, lakini pia tunathamini sana heshima ya kipekee ambayo tumekuwa tukipewa na Uongozi wa ALAT Taifa ya kujumuika pamoja nao katika Mkutano Mkuu huu muhimu kwa maendeleo ya Halmashauri zetu nchini.

“Kwa siku zote za Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa, tutakuwa na banda letu nje ya ukumbi wa mkutano, ili kuhakikisha wajumbe wa kikao pamoja na wadau wengine watakaokuwa katika maeneo ya Golden Tulip Hotel, wanapata huduma za kifedha wakati wote wa kikao.

“Nitumie nafasi hii pia kuwaalika wote katika banda la NMB kupata Huduma Jumuishi za Kifedha muwapo katika mkutano huo, na niwakikishie tu kwamba wafanyakazi wetu watakuwepo kutoa huduma na ushauri kwa wajumbe kwa wakati wote,” alisema Bi. Zaipuna.

Aidha, sambamba na udhamini huo, Bi. Zaipuna alibainisha kuwa, NMB imeandaa mchapalo kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa, ambako aliwakaribisha kushiriki chakula cha jioni, pamoja na kujadiliana machache baina ya Wajumbe ALAT na wafanyakazi wa NMB.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Bw. Sima Constantine Sima, aliishukuru NMB kwa ubia endelevu unaowawezesha kufanikisha vikao na Mikutano Mikuu ya kila mwaka kwa kipindi cha miaka nane sasa ya udhamini wao.

“Shukrani za Jumuiya yangu ziifikie Benki ya NMB kwa hiki inachofanya katika kufanikisha Mikutano Mikuu ya ALAT Taifa kwa miaka nane sasa na hii ndio tafsiri sahihi ya mahusiano mema na ya muda mrefu, ambayo sisi ALAT ndio wanufaika wakuu.

“NMB sio tu wadau wetu kibiashara, bali wao wamekuwa moja ya sehemu kuu za sisi kutolea huduma zetu. Mambo mengi yanayoendelea kufanyika katika Halmashauri zetu yanapitia kwao na ndio ushuhuda wa hili na mahusiano haya ndio tafsiri sahihi ya tunayoyaona kwa miaka nane ya udhamini wao.

Nichukue nafasi hii kuishukuru NMB kwa kutafsiri kwa vitendo juu ya mahusiano mema, ambapo leo pia imedhamini uzinduzi wa kimapinduzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar (ZALGA), ambayo ni mamlaka sawa na ALAT kwa huku visiwani Zanzibar,” alisema Sima.

Aidha, aliishukuru NMB kwa kuandaa hafla ya chaklula cha usiku baina ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa na Wafanyakazi wa NMB, na kwamba anaamini mchapalo huo utakuwa fursa nzuri sio tu ya kubadilishana Mawazo, bali kufurahi pamoja baada ya kazi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 120, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Sima Constantine Sima (katikati) kwa ajili ya udhamini wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa utakaofanyika kuanzia leo jijini Zanzibar. Kushoto ni Afisa Mkuu Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao, Kulia ni Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (kulia) na Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT Taifa, Mohammed Maje (wa pili kulia). (Na Mpiga Picha Wetu).






Top News