Marehemu Kamanda Lucas Ng'hoboko enzi za uhai wake

Na Dixon Busagaga,Moshi.

KAMANDA wa polisi mkoani Kilimanjaro,Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi (SACP),Lucas Ng’hoboko, amefariki dunia gafla baada ya kuanguka leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kaimu kamanda wa polisi mkoani humo,Yusuph Ilembo alisema kuwa kifo hicho kimetokea leo Majira ya saa 3 asubuhi katika zahanati ya polisi mjini hapa.

Alisema taarifa za awali zinaeleza kwamba kamanda huyo alifikishwa katika zahanati ya polisi kwa ajili ya kuangalia afya yake lakini kabla suala hilo halijatekelezwa alianguka gafla na kupoteza maisha.

Ilembo alisema Ng’hoboko ambaye alikuwa katika likizo ya kustaafu tangu Juni mosi mwaka huu,hakuwa anasumbuliwa na maradhi yoyote hadi kifo chake kilipotokea.

“Ni kweli kamanda Ng’hoboko amefariki dunia leo asubuhi…hii imetushtua sana,hakuna anayefahamu sababu za kifo chake,tunasubiri taarifa za kitaalamu kutoka kwa madaktari”alisema.

Kaimu kamanda alisema kwa sasa mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi na baadaye taratibu za mazishi kufanyika kwa maelekezo ya familia yake.

Marehemu Ng’hoboko alihamia mkoani Kilimanjaro mwaka 2006,baada ya mkuu wa jeshi la polisi nchini,Said Mwema kufanya mabadiliko ya kumhamisha aliyekuwa kamanda Venance Tossi ambaye naye alimpokea kamanda Mohamed Chico.

Marehemu Ng’hoboko alianza rasmi likizo ya kustaafu Juni mosi mwaka huu na kwamba kamanda wa polisi mkoani Pwani,Absolom Mwakyoma anatarajiwa kuhamia rasmi mkoani humo Julai mwaka huu.

Baadhi ya askari ambao hawakutaka kutajwa Majina yao,wamezungumzia maisha ya marehemu,Ng’hoboko kwamba alikuwa kiongozi aliyejali maslahi ya askari wake na kuwasikiliza wote bila kujali vyeo wala umri ikilinganishwa na viongozi wengine.

Walisema baadhi ya maafisa wa jeshi huvunja mahusiano na kutowajali askari waliopo chini yao ikiwa ni mara baada ya kupata nafasi za juu katika jeshi hilo jambo ambalo halikuwa likifanywa na marehemu Ng’hoboko.

Kwa upande wao wakazi wa mji wa Moshi,Abdalah Ali na John Mushi walisema wakati wa uongozi wa marehemu Ng’hoboko alijitahidi kudhibiti matukio ya ujambazi ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita.

“Siyo vizuri kufurahi jinsi polisi walivyokuwa wakifanya mauaji lakini kwa kiasi Fulani mauji yale yalipunguza matukio ya ujambazi mkoani Kilimanjaro…hii ilikuwa kazi nzuri ya kamanda Ng’hoboko,Mungu amlaze pema peponi”alisema Mushi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 17, 2011

    Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi Amin!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 17, 2011

    REST IN PEACE COMANDO L.NGHOBOKO...
    Posted by.J.J. KUNDI-Arusha

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 17, 2011

    POleni sana wafiwa, ila hiyo ni Heart attack. Na kwa sasa inaua watanzania wengi mno

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 17, 2011

    Poleni sana jamani nimeshtuka sana na kifo hiki, binadamu tunatakiwa kua tayari wakati wote mana hatujui siku wala saa tutakayorudi kwa Baba.Rest In Peace Ng'ohoboko

    Carol-Geneva

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...