Waafrika tuna tamaduni nyingi ambazo japo hatupendi watu watuambie ama watukumbushie kuwa tunazo zimesababisha udumavu wa maendeleo katika taswira nzima ya maisha jamii yetu. Utamaduni wa kutowajibika katika majukumu tunayojipa sisi wenyewe ama tunayopewa na watu wengine. Hatuna uchangamfu katika kazi yeyote ile tunaona kufanya kazi ni kupoteza muda ambao tungeutumia vizuri kupumzika huku tukinywa vinywaji tunavyopenda na tukiwa katika mazingira ya starehe.
Kuanzia muuza chipsi na mtengeneza kandambili uswahilini mpaka mawaziri katika mawizara hali ndio hiyo hata kama mtabisha maana hili la ubishi sisi ni nambari moja. Tutabisha hata kama jambo liko wazi kama jua la mchana wa saa sita. Tunafanya kazi bila ya umakinifu yakinifu bila ya shauku ya kuboresha tulilofanya jana tutalirejea leo kama ilivyokuwa jana. Tunafanya kazi kama mashine (robot) hatutumii fikra zetu kuboresha huduma ila tuna ubunifu mkuu wa kupindisha miongozo ili tupate njia ya kutoza rushwa kwa huduma tunazotoa.
Uswahilini mpaka maofisini na viwandani na hasa serikalini tuna utamaduni wa kuleana na kuogopana. Wengi wenu mnaona makosa yanayofanyika katika sehemu zenu za kazi lakini ulezi umewazidi na mnaona kwamba mkisema juu ya kosa hilo basi mtakosana na mkosaji na kwasababu hakuna mazingira ya  kuadabishwa basi bora tu mgawane makosa. Hii huzaa woga kwamba wewe una siri ya Yule na Yule ana siri yako kwa hiyo wote  mnakaa kimya na kulindana kwasababu ya woga wa kuvuja kwa siri mlizowekeana.
Hii huleta kushuka kwa ufanisi kazini na pia uvunjaji mkubwa wa sheria za kazi na watu kujifanya miungu watu. Unakwenda kupata huduma ambayo unalipia lakini unajikuta kama vile ile huduma umepewa bure kutokana na dharau na usumbufu utakaopata. Ukienda mahospitalini makarani hujifanya ndio madokta kwa maana bila ya kuwapa kitu kidogo huwezi kumuona dokta. Mara utaambiwa faili lako limepotea wakati ulilifungua dakika kumi zilizopita. Una ugonjwa wa kufa utaambiwa daktari hayupo lakini ukitoa kidogo kama miujiza daktari anatokea.
Hata ukienda madukani kununua bidhaa wauzaji wanakupa dharau kama vile hizo bidhaa unanunua kwa bei ya bure na wao wanakufanyia hisani kukuuzia.
Ukienda wizara ya mambo ya ndani huko ndio usitoe pua kabisa kuomba passport imekuwa ni mradi unaojenga mahekalu mbezi na kwengineko. Utaambiwa wewe si mtanzania hapo ndipo utakapo koma, unaweza kuhisi wewe ni mkimbizi kwenye nchi yako wakati wachina wanakupita na mikoba ya baba Kambarage.
 Alama za vidole huchukuliwa wahalifu ili wapate kutambulika kirahisi wanaporudia makosa.Kuomba pasi ya kusafiria imekuwa kosa ama wewe ni mhalifu mtarajiwa na utajiuliza sasa haya madole mnayochukua ni ya faida gani wakati mijambazi kibao na mijizi iliyojaa mtaani hamujawahi kuikamata kwa kutumia alama za midole hii wajameni...hii ni kutokana na utamaduni wetu wa kuogopana tunaogopa kuwaambia wamarekani na ndugu zake kuwa hatuwezi kuuza alama za wananchi wetu kwa bei ya dola moja.
Tunaoneana haya kiasi watu wamekuwa wakitovuka adabu kupita mifano kwasababu wanajua na wewe unajua kuwa huwezi kumfanya kitu.hii ni kama maigizo ya Simba kumuogopa Swala..ni hivi hivi nchi inazama tunaoneana haya kuambizana kwamba ili mashua yetu iende mbele inabidi tupige makasia. Wakubwa wanakula marushwa halafu wanawekeana viporo mara kimya kama ubaridi wa asubuhi unapopiga usoni na ukaendelea kuvuta shuka.
Kwa utamaduni huu maendeleo hayaji n’go kama mvua jangwa la sahara tutaendelea kuungua na jua mpaka dunia ibadili egemeo. Yangu ni macho ila utamaduni huu utatupeleka pabaya maana wanaofaidi ni wachache na wengi tunaumia.  Wengi tunaingia makanisani na misikitini ili tuonekane tuna dini lakini ukweli ni kwamba hatuna imani wala dini..Dini yetu ni Ubinafsi na Mungu wetu ni Fedha..Tushauza roho zetu kwa shetani ili tupate Fedha, tunaua wenzetu ili tupate Fedha, tunadhulumu  wenzetu ili tupate Fedha.. hatujali mwengine zaidi yetu na yote haya kwasababu ya KULEANA na KUOGOPANA..
ndimi Saidi Ally Saidi aka Mwanafunzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 22, 2011

    Saidi nakubaliana nawe kuhusu viongozi wetu ni wabinafsi,wapo kwa ajili yao na familimia zao tu,ndio maana wanafanya wanavyotaka;they do not care at all, wamesahau kuwa walisomeshwa na serikali hii ambayo leo wanaiibia.
    Hivi bongo FBI hakuna?sababu sajawahi kusikia kiongozi kafikishwa mahakamani kwa uchunguzi uliofanywa na wapepelezi wa nchi kwa kutumia teknologia kama wire taping(kwenye nyumba zao),kuhakiki akaunti ktk benki,kuhakiki mali kama ni zako kupitia mshahara unaolipwa kazini au kama unafanya biashara.
    Maana nchi nyingine ukiwa na zaidi ya $10,000 ktk akaunti basi unaingizwa kwenye mtandao wa FBI na wanacheki kama hizo pesa ni halali kuzipata kwa kazi au biashara halali, kama hauna maelezo ,unapigwa muflisi period.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 22, 2011

    Wakati raia wa kawaida anahangaika na maisha ya kila siku ya kutokuwa na maji, umeme, madawati, madawa,nk, viongozi wanapewa gari bure,dereva bure,mafuta bure,chakula bure,matibabu bure na bado wanaiba mapesa kwa staili wanayoijua wao na kuwapachika watoto wao kwenye ofisi za serikali waendeleze wanachokifanya.
    Leo hii miongoni mwa kila mtoto wa kiongozi na yeye pia utasikia yupo serikalini, kwani hakuna kazi zingine zinazoendana na elimu zao? si lazima na wao wawe wanasiasa,they can do something else.
    Tujitume na tupende kazi zetu watanganyika, ili tuweze kuleta ufanisi wa taifa na familia zetu kwa ujumla.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 22, 2011

    Asnte saaaaaaana ndugu Said Ally. Umeongea mambo ambayo hasa ndiyo yanarudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Hapa mwanzo kuna wachangiaji wawili wamenyoosha vidole kwa viongozi. Sipingani na muono wao lakini matatizo aliyoongea Said yapo kwa jamii nzima ya kitanzania, yaani hata wasiokuwa viongozi. Ukichukua mikoa ya tanzania utaona kwamba kuna baadhi ya watu toka maeneo fulani ni wachapakazi kwelikweli lakini ni wazuri sana wa kutumia njia za mikato kama vile ujambazi, ufisadi, rushwa n.k. Hawa wapo zaidi mikoa iliyotawaliwa na wakoloni wa kizungu. Wakati ukienda kwenye mikoa mingine wengine ni waaminifu saaaana lakini hawapendi kufanya kazi. Hupenda kukaa na kuongea zaidi ikiwa ni pamoja na kuwa walalamishi kuwa eti wameonewa pale wanapoona maendeleo kwao hayapatikani. Hawa hupenda kusaidiwa zaidi kuliko kujisaidia. Hawa wako mikoa iliyotawaliwa na waarabu.

    Lakini Saidi pamoja na hoja yako nzuri hujapendekeza nini kifanyike. Pengine tungekaa siku moja tujute kuwa laiti tungefuata ushauri wa said tusingefika hapa tulipo. Samahani kama kuna niliowakwaza kwa kuwa muwazi zaidi wa fikra zangu.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 22, 2011

    Utakuta wengine jioni hasa uswahilini watu kibao wamekaa nje ya nyumba zao, hadi kutembea wakati unapita unajisikia vibaya, na ole wako usisalimie waliokaa kwenye vibaraza mtaa mzima utajua kuwa hujasalimia na umshaanza kuringa. Ukiwa msomi mtaani ndo balaa zaidi, kila mtu atakuona wewe ni msomi na atakuchukia wewe na familia yako. Nimekaa maeneo ya Mbezi Beach, kila mtu yuko kwenye nyumba yake, iwe na geti au bila geti lakini watu wanaheshimiana hawagombani kwa ajili ya wivu wa maendeleo ya mwingine. Wale wanaokaa uswahili wabadilike waache tabia ya kukaa vibarazani, wafanye kazi zaidi, kukaa kibarazani ni dalili ya uvivu na masengenyo kwa wengine. (Hizi ni tabia za uswahili, uvivu wa kitanzania-Pengine hii ni mikoa ilotawaliwa na Waarabu km Bwn Saidi alivyogusia). Itabidi tufanye kampeni nchi nzima kuwa Watanzania tuache uvivu, wivu usio na maana, tujifunze kufanya kazi. Duh sijui wazungu walitokatokaje kwenye huu umaskini wa mawazo na uvivu. Nchi za wenzetu ukipita mashambani wakulima wana nyumba nzuri, mashamba mazuri, mifugo mizuri, yaani mkulima ni mkulima haswa! Sasa kwetu mtu anayeitwa mkulima duh, ni AIBU! Ziwa Tanganyika lipo Kigoma, ila wananchi wa maeneo hayo ni maskini wa kutupwa, ziwa Nyasa kule Kyela-wananchi maeneo hayo ni maskini wa kutupwa, haya Victoria vile vile, Mara na Mwanza ni aibu tupu. Sasa nani aje kutukwamua kama sio sisi? Hebu serikali wakopesheni wakulima wanunue hata pampu za maji wamwagilie mashamba yao...maana Serikali imeshindwa kuzalisha umeme kutumia vyanzo hivi. Duh, hata sijui niongelee issue gani hapa hadi najikuta nawaza vitu vingi kichwani mwangu....matatizo matatizo matatizo matatizo matatizo.....ee Mola tunusuru!!

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 22, 2011

    Ukienda hotelini nako hovyo hovyo, hasa hii migahawa ya watanzania wa kitanzania. hata maofisi mengine hasa ya umma, kama vile vyuoni, yaani ni kama unajipendekeza kwao wakati ndio kazi zao haswaaa. polisi yale yale. na ndio maana viongozi wetu wanaturudisha nyuma badala ya kutusogeza mbele au angalau kutubakisha pale pale walipotukuta. ni kwa sababu wametokana na mfumo huu huu kwa ujumla wake. viongozi wa dini wanauza mihandarati, vituo vya kulea watoto yatima navyo ni miradi binafsi, waandishi wa habari wananunulika, mahakamani nako unanunua haki, mwananchi anauza kura, n.k. yaani ni kero kweli kweli.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 22, 2011

    kaka saidi umesema ukweli mtupu. kweli hali yetu hapa bongo inasikitisha sana sana. Yaani kweli nasema kuna laana kubwa sana katika nchi yetu na mwisho wake sijui utakuwaje.

    Hayo uliyosema hata kwenye mashirika ya umma yanachangishwa na kutoa hela nyingi sana hasa kipindi cha uchaguzi na hili la umeme ni 40 yao tu na kusema ukweli mambo hayo yametendeka kwa wingi sana. Ubaguzi upo sana kwenye taasisi za serikali na mashirika ya umma na kweli nchi yetu imeoza kwa rushwa.Mungu akiingilia kati na watu wakakubali basi tutapona la sivyo hali ni mbaya sana kote kote

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 22, 2011

    Hata Ughaibuni hayo mambo inayoyasema yapo. Polisi wa mama ndio wanaongoza kwa hizo tabia, wanapokuwa hawaonyeshi hizo tabia ni inapokuwepo kamera au mtuhumiwa si mzungu mwingereza! Kuna nchi kweli hawana lakini kama utakaa nao sana utangundua hizo tabia wanazo. Wewe chukulia Rooney, amecheza mechi kadha bila ya kufunga bao, lakini babadov akikosa kufunga mechi chache tu wapenzi wote wa manu wanataka auzwe. Wengi wetu tunaangalia ligi ya uingereza, na kila mechi ya manu watapendelewa, mbona fa yao haichukua hatua?!!

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 22, 2011

    Kujali au kutojali hakutokei kwa siku moja. Hawa viongozi kuna siku walikua kama sisi tunaolalamika.

    CHANGAMOTO: Mpaka sasa umefanya nini au unafanya nini cha tofauti ili siku ukifikia kwenye uongozi uwe tofauti na hao tunaowanyoshea vidole?

    ANGALIZO:
    1. Acha kutunga safari ambazo sio za lazima ukiwa ofisini -
    2. Acha kugushi risiti
    3. Ishi maisha kulingana na kipato, achana na mashindano yasiyokua na tija - be authentic
    4. Pale NMB, CRDB au mahali popote kwenye foleni, usianze kutafuta wafanyakazi mnaofahamiana ili wakusaidie - be bold
    5. Acha kunywa kifungua kinywa cha elfu kumi wakati nyumbani umeacha elfu mbili kwa siku nzima
    6. Mjali jirani yako, hata kwa kumpa ushauri tuu
    7. Wajibika ufikapo kazini na sio kushindia kuchat na kucomment kwenye FB
    8. Acha kupita pembeni ya barabara wakati wa foleni, kwani hao unaowapita pia wana haraka kama wewe
    9. Kabla ya kufanya uamuzi, angalia madhara yake kwa waliokuzunguka na jamii kwa ujumla
    10. Ijali familia yako, utokapo baa rudi japo na nyama choma kwa ajili ya familia yako
    .
    .
    .
    .

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...