JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na
mvutano baina menejimenti kwa upande mmoja na wafanyakazi na wanafunzi kwa
upande mwingine wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala katika Chuo Kikuu
Kishiriki cha Dar es salaam ama, kinavyojulikana kwa wengi, KIU. Mvutano huu ulisababisha
baadhi ya waalimu kusitisha kufundisha na pia baadhi ya wanafunzi kujikuta
katika mgomo hadi mvutano uliojitokeza utakapopatiwa ufumbuzi.
Mvutano huu
hatimaye ulisababisha Tume ya VyuoVikuu Tanzania kuingilia kati katika jitihada
za kuupatia ufumbuzi. Mnamo tarehe 14 Novemba 2012 Tume iliunda timu ya
wataalamu ambao walikwenda katika Chuo hicho na kufanya kazi kwa siku mbili
kabla ya kuuanda ripoti yao. Ripoti ilibainisha maeneo mbalimbali yenye
changamoto ambazo budi zipate majibu.
Ripoti hiyo ilijadiliwa katika kikao cha
Kamati ya Tume ya Ithibati na Chuo kupewa maelekezo katika maeneo mbalimbali na
pia kutakiwa kuleta majibu katika masuala yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa
majibu. Maelekezo haya yaliwasilishwa Chuoni kwa barua ya tarehe 4 Desemba 2012
yenye kumbukumbu na TCU/A.40/69/Vol.IV/15 na kutakiwa kuleta majibu Tume kabla
ya tarehe 30 Desemba 2012. Kabla majibu hayajawasilishwa mgogoro wa wafanyakazi
ulianza na kufuatiwa na mgomo wa wanafunzi na hivyo tarehe 11 Desemba 2012
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya
Juu walikwenda katika Chuo hicho ili kuonana hususan na wanafunzi pamoja na
menejimenti. Kimsingi, kikao kilihusisha menejimenti na wanafunzi kwa kuwa
suala la wafanyakazi lilikuwa limeshapatiwa muafaka wa jinsi ya kulitatua.
Kufuatia mawasiliano ya awali baina ya
menejimenti ya Chuo na viongozi wa wafanyakazi kuhusu mishahara ya wafanyakazi
ya mwezi wa Novemba 2012 pande zote zilikubaliana kwamba malipo hayo yawe
yamefanyika ifikapo tarehe 14 Desemba 2012.
Pia Chuo pamoja na waalimu
wameafiki kufidia kipindi cha masomo ambacho kilipotea wakati wafanyakazi
wanashughulikia mstakabali wa mishahara yao. Kufidia huko kutafanyika kati ya
tarehe 7 Januari na 11 Februari 2013 ili kutokuathiri mipango mengine ya
kimasomo ambayo tayari ilishapangwa kwa kipindi cha sasa hadi Januari 2013.
Makubaliano haya yamewasilishwa TCU kwa barua ya Mkuu wa Chuo ya tarehe 10
Desemba 2012 yenye kumbukumbu Na. KIU/PR/Vol.30/11/12. Tume imeelekeza
makubaliano haya yatekelezwe bila kukosa ifikapo tarehe 14 Desemba 2012. Ni
matumaini ya Tume kwamba hali hii haitajitokeza tena ili shughuli za
ufundishaji katika Chuo hicho ziende kulingana na ratiba ya kila semesta.
Kupata taarifa ya yaliyojiri katika
kikao baina na menejimenti, wanafunzi, Katibu Mtendaji wa Tume na Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu BOFYA HAPA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...