1. Ninamuomba manani, tuidumishe amani
Tusipate tafurani, kuipoteza amani
Utujarie imani, tusifanye yakihuni
Utuongoze manani tuidumishe amani

2.      Amani iwe motoni, tusiibebe kichwani
Tena ikae tumboni, wasiione jirani
Wao wanaitamani, kwao haipatikani
Utuongoze manani tuidumishe amani

3.       Mashekhe misikitini, Makasisi kanisani
Waumini waambieni, madhara yake ni nini
Amani haipatikani, ipoteapo nchini
Utuongoze manani tuidumishe amani

4.       Amani bidhaa gani, kwa pesa haipatikani
Dukani hata sokoni, dola za marekani
Yeni pia za Japani, Euro za Kijerumani
Utuongoze manani tuidumishe amani

5.       Tukipoteza amani, tutakuwa watu gani
Hatusomi kwa jirani, wanaishi ugenini
Nani atakuthamini kwenu hakujulikani
Utuongoze manani tusipoteze amani

6.       Unapoteza Amani, Kwa simu ya mkononi
Vocha atakupa nani, waonekana muhuni
Unaishi vichakani, roho iko mikononi
Utuongoze manani tusipoteze amani

7.       Tukumbuke majirani, wamejaa Marekani,
Kwao wanakutamani, lakini haiwezekani
Kuishi ukimbizini, upate faida gani
Utuongoze manani tusipoteze amani

8.       Kuikamata sukani, ndicho chenye thamani
Wakujue ni rubani, utakapokaa kitini
Ujulikane ni nani, umetua baharini
Utuongoze manani tusipoteze amani

9.       Maisha yetu zamani, kwetu hatuna kifani
Japo kuwa ni mgeni, hatumuweki pembeni
Utapewa biriani, tena katika sahani
Utuongoze manani tusipoteze amani

10.   Tunakuomba Rahamani, Zidisha yetu imani
Tukeshe misikitini, pamwe na makanisani
Utujazie imani, tuishi kama zamani
Utuongoze manani tusipoteze amani

11.   Kwaherini kwaheri, tukijaliwa mwakani
Yangu haya yashikeni, tusiwe kama manyani
Aingiapo shambani, hata huruma haoni
Utuongoze manani tusipoteze amani
  
Mimi Mpenda Amani
Bi. Tunguri Rajab Tambwe

Dar Es Salaam, Machi 2013.

Bi.Tunguri Rajabu Tambwe ni mtoto wa pili wa Mshairi wa zamani Enzi za akina Amri Abeid na Mzee Saadan Kandoro. Huwa anaandika mashairi ambayo yanatumika zaidi ndani ya familia. lakini hili hapa ni kwa watanzania wote. Bi Tunguri Rajab Tambwe alizaliwa tarehe 17 April 1945, mkoani Mbeya.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 14, 2013

    AMANI NCHINI TANZANIA:

    Ni wazi wapo waliopoma ya pazia wasioitakia mema nchi yetu, kwa visingizio mbalimbali ikiwemo Siasa na Itikadi za KiDini.

    HATUKUBALI KUCHEZEWA NA KUYUMBISHWA NA MAGENGE HAYA MACHACHE YA WATU WANAOHESABIKA YANAYOTAKA TUINGIE KTK MISUKO SUKO YA KIMAISHA NA MUSTAKABALI ILI WAO WAFIKIE MALENGO YAO MACHAFU!

    TUTAILINDA AMANI KWA GHARAMA YEYOTE ILE HATA KWA MTUTU WA BUNDUKI!!!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 14, 2013

    Nakushukuru mwanetu,Kutupa yako maoni
    Amani ni kila kitu, kwa ustawi makini
    Bora kula kidogo tu,na ulale kuvulini
    Nasisitiza kiutu, Amani ikumbatienie

    Namuunaga mkono kwa maoni ya kweli. Mimi niliwahi kuwahudumia wakimbizi wa nchi fulani miaka ya siombi hata siku moja kuwa mkimbizi. Ukikaa nao utaona ni jinsi gani wanaumia kwa hali walizonazo. Nina mengi ya kuongea kuhusu amani ila yanahitaji muda.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 14, 2013

    Unanikumbusha zamani sana wakati kabla ya simu za kiganjani na facebook.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 14, 2013

    Amani ni tunu ni vyemakuienzi
    Tuenzi majumbani ,nabarabarani pia
    Tuepuke ushabiki,Wa kuingizwa mitegoni
    Yarabi tunakuimidi,tupe upeo tuieshimu amani

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 14, 2013

    Bi Tunguri shikamoo, Asante kwa lako shairi
    Mimi pia niwapo, kuepusha hiyo shari
    Sote tujue tupo katika hali ya hari
    Mungu tujaliepo, Tanzania yetu shwari

    Hakika kweli wapo, wanaotamani ushari
    Bila kufikiri iwapo, Amani hii itaghairi
    Wao wale kiapo, tena wao waghairi
    Mungu tujaliepo, Tanzania yetu shwari

    Kama kuna kichapo, basi wapewe bahari
    Ndicho kiwatoshapo, kwa kutaka shari
    Wengine huko hatupo, hata kupewa dinari
    Mungu tujaliepo, Tanzania yetu shwari

    Tamati sasa nifikapo, salaamu zangu ni heri
    Niwasalimu na wapo, wa mbali kwa buheri
    Karibuni sote tupo, Tanzania yenye heri
    Mungu tujaliepo, Tanzania yetu shwari

    Selina


    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 14, 2013

    Potelea mbali!

    Acha dunia ituelewe itakavyo tuelewa hatuna jinsi.

    Tumesha watambua (TUNA WAFAHAMU VIZURI TU) wanao hatarisha amani nchini, TUNAWEZA KUWACHINJIALIA MBALI HAO WATU WASIOZIDI 200,000(LAKI MBILI) ili tuweze kunusuru Taifa la watu 45 Mil.!

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 14, 2013

    Dunia imeshuhudia mahala popote penye Jitihada za Kupiga hatua hapa kosekani Wapinga maendeleo hata kama atakuwa mtu mmoja tu.

    ''MFANO HAI NI YOMBA YOMBA KTK SINEMA MOJA YA ZAMANI HAPA TANZANIA, WATU KIJIJINI WALIKUWA WANANIA YA KUFANYA KAZI ZA KULETA MAENDELEO LAKINI YEYE AKAWA MPINGAJI MKUWA''

    Nchi mbali mbali duniani zili hakikisha Dira inafikiwa Mifano:

    1.ITALIA:
    Iliuwa MAFASHISTI kadhaa waliokuwa wapinga maendeleo ili Dola isimame.

    2.UFARANSA:
    Ililazimika kuuwa MABEBERU wachache wapinga maendeleo ili wasonge mbele.

    3.UINGEREZA:
    Ilihakikisha MABWENYENYE wapinga maendeleo wanatokomea na kuacha Mabwenyenye wachache wenye faida ili wasonge mbele.

    4.JAPAN:
    Iliangamiza MADIKTETA wote ili isonge mbele.

    5.URUSI:
    Iliwaangamiza MAKABAILA wote ili isonge mbele.

    Hivyo safari ya kuelekea kwenye AMANI iliyodumu ina mabonde na milima ambayo pana hitajika maamuzi magumu KAMA MNAVYOONA KTK MIFANO HIYO HAPO MITANO (5) JUU, UKIWEPO MFANO WA KUBWA LAO HAPA HAPA TANZANIA YOMBAYOMBA NA UPINZANI WAKE KIJIJINI KWAO ili kufikia malengo kwa faida ya walio wengi!

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 14, 2013

    Amani yetu ni tunu, isiyokuwa kifani
    idumu na zetu mbinu, pasipo na tafurani

    Wachochezi kama kinu, hutwanga na kurubuni

    Vurugu kwao kicheko, amani kwao ni kero.

    Tuilinde amani yetu kwa mbinde na kwa upinde!

    ReplyDelete
  9. AMANI IDUMU (MKAZO)

    Shkamoo Bi Tunguri, mwanao kuniitika,
    Hongera shairi zuri, vina mizani pangika,
    Ujumbe ni 'santuri', sokoni umeuzika,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI tia mkazo, chonde isije toweka,
    Ikajazuka mizozo, na vilio hasikika,
    Kwetu kubwa yetu nguzo, nguvu zote meishika,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI tuidumishe, hilo sifanye dhihaka,
    Dua na sala tukeshe, tataqabali RABUKA,
    Mitafaruku iishe, popote ilipozuka,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI mithili jua, nuruye kote itaka,
    Sijegeuka mvua, jibanza hahangaika,
    Ama gharika ikawa, hajakosa pa kushika,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI ni malighafi, kuitunza inataka,
    Kiidumisha haifi, kuienzi ni baraka,
    Ndipo huwa mambo safi, ndani nje hasifika,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI tuombe Mungu, nchi yote kuzunguka,
    Itande mithili wingu, kama radi kusikika,
    Tuwe mbali na machungu, tafrani sijezuka,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    AMANI iwe kioo, jitazama tukicheka,
    Pasi waita njoo, wengi kwetu tafurika,
    Hapa na pale masoo, na mengi yatatwepuka,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.

    Namaliza wasalamu, kidoto hapa naweka,
    Sichoki omba RAHIMU, sifa zote lojitwika,
    AMANI daima dumu, ulimwengu kuzunguka,
    TUIDUMISHE AMANI, NCHI DUNIA ZUNGUKA.








    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 15, 2013

    asante binti Tambwe
    ukiweza kuniandikia email , nitafurahi
    mimi mu omani , nilizaliwa Urambo
    namjua mzee marehemu Rajabu tambwe
    saeedmarjiby@hotmail.com
    00968 99813400

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 16, 2013

    Amani

    Amani shika hatamu, vurugu kwetu haramu,
    Na sisi tuwe na hamu, kuishi kwa ufahamu,
    Amani na ukarimu, isiwe ni ya msimu,
    Asante bi Tunguri, kwa hilo lako shairi

    Twaomba tunga lingine, elimu na izagae
    Hakuna nchi nyingine, hapana tutapakae
    Amani na si jingine, fujo na isisambae
    Asante bi Tunguri, kwa hilo lako shairi

    Asante Bwana Michuzi, kwa huo wako uwanja
    Malenga wana ujuzi, fujo haina mjanja
    Likivunda ni la juzi, si la udi wala ganja
    Asante bi Tunguri, kwa hilo lako shairi

    Tanzania ndipo kwetu, katu hatuna kwingine
    Tuiliinde nchi yetu, na wala si vingine
    Wachochezi si wenzetu, maadui pande nne
    Asante bi Tunguri, kwa hilo lako shairi

    Dar Es Salaam, 16th June 2013. A.P.M

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...