Mkuu wa mkoa wa
Mwanza Mhe. John Mongella ameuagiza uongozi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha
linakabidhi kiwanja namba 28-A kilichopo katika eneo la Bugando ifikapo Aprili
25, 2016 kwa mmiliki halali wa kiwanja hicho bwana Justine Eminoga ambacho
amekuwa akikidai kutoka kwa mfanyabiashara wa Jijini humo kwa zaidi ya miaka
sita sasa.
Mhe. Mongella amefikia
hatua hiyo mara baada yakupokea malalamiko kutoka kwa bwana Justine ambaye
alifika katika Jiji la Mwanza kwa ajili kufatilia suala lake ambalo limedumu
kwa zaidi ya miaka sita sasa. Akitoa malalamiko yake mbele ya mkuu huyo wa mkoa,
bwana Justine alidai kuzulumiwa kiwanja hicho na mfanyabiashara aliye mtaja kwa
jina Shanif Mansour ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwimba.
Katika hatua
nyingine mkuu huyo wa mkoa ametoa siku saba kwa halmashauri za mkoa wa Mwanza
kuhakikisha wanakamilisha zoezi la kuhakiki
watumishi, ili kubaini endapo kuna watumishi hewa waliosalia katika zoezi
la awali, zoezi la sasa ambalo linasimamiwa na Ofisi ya katibu Tawala wa Mkoa
wa Mwanza kwa kamati maalumu zilizo undwa na mkuu wa Mkoa huo.
Akiwa katika ziara
hiyo mkuu huyo wa mkoa aliagiza kukamatwa kwa Afisa Utumishi msaidizi wa jiji
la Mwanza Henry Sedetale, ambaye alisaidia watumishi hewa watano kuchukua
mikopo ya zaidi ya Mil.90 kutoka katika benki tofauti tofauti, hata hivyo
taarifa kutoka Taasisi yakupambana na
kuzuia rushwa mkoani Mwanza iliyotolewa
wakati wa kikao hicho na mkuu wa Takukuru mkoani humo, ilisema mtuhumiwa huyo
tayari alikuwa ametiwa nguvuni na taasisi hiyo kwa mahojiano zaidi.
Mkuu wa mkoa wa
Mwanza yupo katika ziara kujitambulisha katika mkoa huo na hii ikiwa ni Wilaya
yake ya tatu mara baada yakutembelea wilaya za Misungwi na Magu hapo awali.
Imetolewa na
Atley
J. Kuni
AFISA HABARI NA MAHUSIANO –RS
MWANZA.
18 Aprili, 2016
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...