Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TANZANIA ikielekea kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza uchumi wa viwanda, teknolojia na usalama wa chakula, utafiti wa miaka zaidi ya 20 wa kutengeneza juisi ya ndizi kwa njia ya kisasa unaonekana kuwa miongoni mwa fursa zinazoweza kuongeza thamani ya mazao ya ndani, kuzalisha ajira na kupunguza utegemezi wa vinywaji vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Oscar Tibazohi, anasema msukumo wa kuanza utafiti huo ulitokana na namna ya jadi ya utengenezaji wa togwa na pombe ya ndizi inayofanyika katika maeneo ya Kagera, Kigoma, Rwanda, Burundi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Anaeleza kuwa katika baadhi ya maeneo, hususan Kagera, pombe maarufu ya Rubisi hutengenezwa kwa kutumia ndizi kali ambazo hukanyagwa na kukandwa kwa miguu au mikono kabla ya kuvundikwa.

“Niliona kuna changamoto kubwa ya usafi. Unapokanyaga ndizi kwa miguu, masuala ya usalama wa chakula yanakuwa magumu kuyadhibiti. Hapo ndipo nilipoanza kufikiria namna ya kuiboresha teknolojia hii na kuipeleka katika mfumo wa kisasa,” anasema.

Profesa Tibazohi anasema baada ya kumaliza shahada yake ya uzamili alitaka kuendeleza teknolojia hiyo lakini hakufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.
Baadaye alijiendeleza hadi shahada ya uzamivu na aliporejea akaanza tena safari ya utafiti.
Katika hatua za utafiti, alishirikiana na mtafiti kutoka Uganda aitwaye Mkyamwangire.

Wawili hao walitumia takribani miaka mitatu kufanya majaribio na tafiti za kina ili kufahamu siri ya utengenezaji wa juisi ya ndizi.

“Ndizi zinazotumika ni ndizi kali zenye utomvu mwingi. Tofauti na matoke, ndizi hizi hazichemshwi. Ukizichemsha zinapata rangi ya kahawia na ukakasi unaongezeka. Tulianza kujiuliza ukakasi huo unatokana na nini na unakaa sehemu gani ya ndizi,” anasema.

Kwa mujibu wake, uchunguzi huo uliwasaidia kubaini chanzo cha utomvu na namna ya kuondoa ukakasi bila kuharibu ubora wa juisi.

Matokeo yake yalifungua njia ya kutumia mashine kutengeneza juisi badala ya kutegemea mbinu za jadi.

Leo hii, anasema mashine ya kutengeneza juisi ya ndizi tayari ipo na inaweza kutumika kuzalisha juisi inayoweza kuuzwa madukani kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya soko.

Katika hatua za uzalishaji, juisi hupashwa joto kati ya nyuzi joto 85 hadi 90 za selsiasi ili kuua vijidudu na kuzuia ukuaji wa vimelea vinavyoweza kuharibu bidhaa.
Anasema baada ya hapo huongezwa tindikali ya asili ya citric acid inayotokana na matunda ili kusaidia kuhifadhi ubora wake.

Anasema juisi ikifungashwa vizuri wakati bado ina joto na kuhifadhiwa katika mazingira sahihi inaweza kudumu kwa miezi mitano hadi sita bila kuharibika.

Kwa wanaotaka kuzalisha pombe ya ndizi, hatua inayofuata ni kuongeza amira (yeast) ili kuanzisha mchakato wa uvundishaji.

“Teknolojia hii inaweza kutengeneza juisi, pombe na hata mvinyo wa ndizi. Hivyo thamani ya zao la ndizi inaweza kuongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi,” anasema.

Profesa Tibazohi anaeleza kuwa juisi ya ndizi ina kiwango kikubwa cha sukari asilia, hivyo hupunguzwa kwa kuongeza maji safi hadi kufikia kiwango kinachokubalika cha takribani asilimia 13.

Licha ya mafanikio ya kiteknolojia, anakiri kuwa changamoto kubwa inayowakabili watafiti wengi nchini ni kushindwa kupeleka bidhaa zao sokoni.

“Watafiti wengi hawawezi kuzungumzia vizuri bidhaa zao wala kuzitangaza. Ndiyo maana mara nyingi tafiti zinaonekana kubaki kwenye makaratasi badala ya kuwa biashara zinazowanufaisha wananchi,” anasema.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni gharama kubwa za kununua mitambo, kuanzisha viwanda, kuajiri wafanyakazi na kufanya matangazo ya bidhaa.

Kwa mujibu wake, mradi huo uliwahi kupata ufadhili wa shilingi milioni 100 kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), fedha zilizosaidia kufanikisha hatua mbalimbali za utafiti.

Hata hivyo, anasema bado kunahitajika uwekezaji zaidi ili teknolojia hiyo ifikishwe sokoni kwa kiwango kikubwa.

“Kwa sasa tunahitaji angalau milioni 100 nyingine ili kuanzisha uzalishaji wa kibiashara. Tunahitaji eneo la uzalishaji, mashine na wafanyakazi wa kuendesha shughuli hizo,” anasema.

Anasisitiza kuwa teknolojia hiyo inaweza kuzalisha maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuanzia kwa wakulima wa ndizi, waendesha mitambo, madereva, wasambazaji wa bidhaa hadi wauzaji.
Akihusisha utafiti huo na Dira ya Taifa 2050, Profesa Tibazohi anasema sekta ya vinywaji ni sehemu muhimu ya mnyororo wa chakula na maendeleo ya viwanda.

“Tanzania inaagiza sharubati na juisi nyingi kutoka nje. Kama tutatumia malighafi zetu kuzalisha bidhaa hizi, tutatengeneza ajira, kuongeza mapato ya wakulima na kuifanya fedha ibaki ndani ya nchi,” anasema.

Pia anasisitiza umuhimu wa elimu ya amali katika shule na vyuo ili kuwajengea vijana uwezo wa kubuni na kuendeleza teknolojia zinazotatua changamoto za jamii.

“Tunapaswa kuwa na viwanda vidogo vya mafunzo ya kuchakata matunda, kutengeneza mbolea na bidhaa nyingine. Hii itasaidia vijana kujifunza kwa vitendo na kuendeleza ubunifu wao,” anasema.

Baada ya zaidi ya miongo miwili ya utafiti, teknolojia ya juisi ya ndizi ya Profesa Tibazohi imeonyesha uwezekano wa kubadilisha zao la ndizi kutoka mazao ya kawaida ya chakula kuwa malighafi ya viwanda.

Kilichobaki sasa ni uwekezaji wa kutosha ili ubunifu huo uvuke mipaka ya maabara na kuingia katika soko, ambako unaweza kuzalisha ajira, kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuchangia safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2050.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...