Na Janeth Raphael MichuziTv – Dodoma
Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeendelea kuimarisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR, huku idadi ya watumiaji wa huduma hiyo ikiendelea kuongezeka kwa kasi.
Akizungumza leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa amesema huduma za usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimeendelea kuimarika na kuvutia wananchi wengi zaidi kutumia reli hiyo.
Profesa Mbarawa amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa kupitia reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma, ikilinganishwa na abiria milioni 2.05 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 22.40, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wananchi katika huduma za usafiri wa reli ya kisasa nchini.
Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kutekeleza ahadi yake ya kuanza usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR, ambapo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, TRC ilisafirisha jumla ya tani 102,452 za mizigo.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha sekta ya uchukuzi nchini kwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia miundombinu ya kisasa ya reli.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...