Na Janeth Raphael MichuziTv - Iringa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ameonyesha kutoridhishwa na baadhi ya hospitali nchini kuendelea kuwaagiza wananchi kununua dawa nje ya hospitali licha ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi katika sekta ya afya ili kuhakikisha hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na dawa za kutosha kwa ajili ya wananchi, huku taarifa za vitabu zikionyesha kuwa kiwango cha upatikanaji wa dawa kinafikia zaidi ya asilimia 90.

Hata hivyo, amesema bado wananchi wengi wanapofika hospitalini kupata matibabu huambiwa kwenda kununua dawa katika maduka binafsi jambo alilolitaja kuwa ni “mambo ya ajabu” yasiyopaswa kuendelea kuvumiliwa.

“Mtu anaambiwa dawa zipo kwa mujibu wa taarifa na kumbukumbu za hospitali, lakini mgonjwa akifika anatakiwa kwenda kununua dawa mtaani. Haya ni mambo ya ajabu kabisa na hayakubaliki,” amesema Dkt. Mwigulu.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu amesema tayari ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu pamoja na watendaji wa Mkoa wa Iringa kuhakikisha dawa zote zinazonunuliwa kwa fedha za Serikali zinawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa.

Amesisitiza kuwa viongozi na watendaji wa sekta ya afya wanapaswa kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wanapohitaji huduma za matibabu.

“Natoa maelekezo kwa Mganga Mkuu pamoja na watendaji wote kuhakikisha dawa zitakazotumika katika hospitali zote za Mkoa wa Iringa zinasimamiwa ipasavyo. Mimi mambo ya ajabu ajabu sina ustaarabu nayo. Ninachotaka ni wananchi wanufaike na dawa zinazotolewa na Serikali,” alisisitiza.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba pamoja na miundombinu ya hospitali ili wananchi wapate huduma bora karibu na maeneo yao.

Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya afya kufanya kazi kwa uadilifu na kuwahudumia wananchi kwa haki bila kuwapa usumbufu usio wa lazima, akisisitiza kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinapaswa kuonekana moja kwa moja katika huduma wanazopata wananchi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wilayani Kilolo, mkoani Iringa, alipokuwa akizungumza na wananchi katika moja ya ziara yake ya kikazi mkoani humo, ambapo alipokea na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimballina huduma za kijamii.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...