Na Janeth Raphael MichuziTv
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, kupitia kwa Mwenyekiti wake Johanes Lukumay, ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubobezi, akisema hospitali hiyo imeendelea kuwa tegemeo muhimu kwa wananchi wanaohitaji matibabu ya kiwango cha juu nchini.
Lukumay ametoa pongezi hizo baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kufanya ziara katika hospitali hiyo jijini Dodoma, ambapo ilikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Matibabu ya Saratani, kutembelea wagonjwa pamoja na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na hospitali hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Lukumay amesema uongozi wa BMH chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Abel Makubi, umeonyesha mfano wa uongozi bora kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora wa hali ya juu.
“Hospitali hii ilianza kutoa huduma za upandikizaji wa uloto mwaka 2023. Hadi sasa watoto 30 tayari wamefanyiwa huduma hiyo kwa mafanikio, jambo ambalo linaonyesha uwezo mkubwa wa kitaalamu uliopo hapa,” alisema Lukumay.
Ameongeza kuwa kati ya watoto hao 30, watoto 20 walipatiwa gharama za matibabu kupitia msaada wa Samia Suluhu Hassan, hatua aliyosema imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya huduma hiyo muhimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ya matibabu.
“Tunapaswa kuipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kazi kubwa inayofanya katika kuokoa maisha ya Watanzania na kuendelea kupanua huduma za kibingwa na ubobezi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Florence Simizi, alimpongeza Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika hospitali hiyo, ambao umeiwezesha kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Amesema kuelekea maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, serikali imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya.
“Tumekuja kujionea maendeleo yaliyopo hapa. Hospitali hii kwa sasa inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 17 za ubobezi. Hili si jambo dogo kwa sababu huduma hizi zinahitaji wataalamu wa kada mbalimbali pamoja na miundombinu ya kisasa,” alisema Dkt. Simbazi.
Ameongeza kuwa utoaji wa huduma hizo unategemea uwepo wa miundombinu bora, vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, mambo ambayo yameendelea kupewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Makubi, amesema hospitali hiyo inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuifanya kuwa kituo kikuu cha matibabu nchini.
Amesema moja ya maono ya hospitali hiyo ni kuona BMH ikifikia hadhi ya Hospitali ya Taifa, huku maeneo ya wazi yanayozunguka hospitali yakitumika kuanzisha “Kijiji cha Matibabu” kitakachojumuisha huduma mbalimbali za afya na uwekezaji katika sekta ya tiba.
Profesa Makubi ameeleza kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo ya sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubobezi, pamoja na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za matibabu katika ukanda wa Afrika Mashariki.





.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...