Na Ashura Mohamed – Arusha

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka wasomi na watafiti nchini kuja na suluhisho la kudumu la kumaliza ugonjwa wa Malaria, kama ambavyo wasomi katika mataifa mengine wamefanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo.

Akizungumza Jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 33 wa Kisayansi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Waziri Mchengerwa alisema wataalamu ni lazima waje na tafiti mbalimbali zitakazosaidia jamii kuondokana na changamoto za kiafya.

“Ndugu zangu watafiti, ugonjwa wa Malaria ni lazima sasa ifike mwisho. Wapo wanaotumia dawa lakini haziwasaidii, lakini mazingira yao yapoje? Wapo wanaotumia vyandarua, lakini je watavitumia mpaka maeneo ya kutafuta biashara zao? Hilo si kweli. Au tutatumia njia gani na utaalam gani kumaliza mazalia ya mbu katika mazingira yao? Wajibu wa watafiti ni kuleta suluhisho. Au tukibuni suluhisho taasisi zetu zitakosa kipato? Tuambizane tu,” alisema Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa alisema haiwezekani changamoto ya Malaria ambayo imedumu kwa miaka zaidi ya mia moja bado iendelee kusumbua nchi zinazoendelea, wakati katika mataifa makubwa duniani ugonjwa huo umekwisha na kuwa historia licha ya kuanzia katika mataifa hayo.

“Ni vema tukakubaliana kuwa maamuzi magumu mtayatafiti katika kipindi hiki. Nikiwa Waziri, tutamshauri Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuyatekeleza ili ugonjwa wa Malaria utokomezwe kabisa. Haiwezekani kila siku tunalia Malaria wakati kuna mataifa Malaria kwao ni historia. Twende tukaokoe vifo vya mama na watoto wachanga chini ya miaka mitano kwa kutokomeza ugonjwa wa Malaria,” alisisitiza Waziri.

Pia alisema anaamini NIMR ikiwezeshwa itapiga hatua katika tafiti mbalimbali, kwa kuwa yapo maeneo yanayoweza kusubiri ila si tafiti.

Alibainisha kuwa mara nyingi fedha zinazotengwa kwa ajili ya tafiti haziwafikii kwa wakati, hali inayokwamisha maendele huku akisisitiza kuwa ili taifa lipige hatua, utafiti haukwepeki.

“Eneo la tafiti kwenye nchi yetu halikwepeki. Tukifanikiwa kwenye tafiti na wenzetu wa mipango wakitusaidia kutafsiri, nchi itapiga hatua kubwa sana, kwa kuwa changamoto zilizopo kwenye jamii zitapata majibu,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR), Profesa Aboud alisema taasisi hiyo imeendelea kufanya tafiti zinazotegemea ushahidi wa kisayansi na kusaidia uundaji wa sera bora za afya.

Alitaja tafiti zilizochangia mabadiliko ya sera ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kutoka dozi mbili hadi dozi moja, pamoja na tafiti za kifua kikuu zinazoonesha uwezekano wa kupunguza muda wa matibabu kutoka miezi sita hadi miezi minne kwa manufaa ya Serikali na wagonjwa.
Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watafiti katika Kongamano la 33 la Kisayansi lilioanza Leo Mkoani Arusha


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...