Na Janeth Raphael - MichuziTv
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, amewataka wananchi kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane 2026 kama fursa ya kujifunza huduma na mipango mbalimbali ya Serikali inayolenga kuboresha maisha yao.
Nderiananga ametoa wito huo alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma, Agosti 6, 2026.
Akiwa katika banda hilo, aliwapongeza waandaaji kwa maandalizi mazuri na namna wanavyotoa huduma kwa wananchi kupitia elimu, ushauri na mwongozo unaowawezesha kupata suluhisho la changamoto mbalimbali pamoja na kuunganishwa na taasisi husika kwa haraka.
Amesema ushiriki wa taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maonesho hayo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, huku akiwakaribisha wakazi wa Dodoma na maeneo mengine nchini kutembelea banda hilo ili kujionea kazi zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Nderiananga pia aliwahamasisha wananchi kutembelea maonesho hayo kwa wingi ili kupata uelewa mpana kuhusu majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, sambamba na kujifunza fursa zinazopatikana katika sekta za kilimo na mifugo ambazo ni nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi.
Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane 2026 yanaendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050."




.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...