Na Janeth Raphael - MichuziTv

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka kulinda maeneo ya wazi na ya taasisi za umma, akisema uzembe katika usimamizi wake unachangia kuibuka kwa migogoro ya ardhi na kuleta malalamiko kati ya wananchi na Serikali.

Mmuya ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua maeneo ya wazi jijini Dodoma, ambapo amebaini baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma yamevamiwa na kuendelezwa na watu binafsi. Amesema hali hiyo haiwezi kuachwa iendelee, huku akiwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kwa matumizi ya umma yanasimamiwa ipasavyo.

Amesema Jiji la Dodoma lina jumla ya maeneo 3,237 ya wazi, lakini ni 385 pekee yaliyopimwa na kuwa na hati, hali aliyosema inaongeza uwezekano wa maeneo hayo kuvamiwa na kuibua migogoro. Ameagiza maeneo yote ya wazi yapimwe, yapatiwe hati na yawekwe alama za kudumu pamoja na mabango yanayoonesha ukubwa wa eneo, matumizi yaliyopangwa na mmiliki.

“Wakurugenzi mna dhamana ya kusimamia maendeleo ya maeneo haya. Yapitieni yote na kubaini hali yake ili kuchukua hatua stahiki. Ni wajibu wa kila anayemiliki kuhakikisha yanapimwa na kupatiwa hati,” amesema Mmuya, huku pia akikemea ujenzi holela unaofanywa bila kufuata taratibu za mipango na ujenzi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Fungo, amesema Halmashauri imepokea maelekezo hayo na imeanza kufuatilia maeneo yote yaliyovamiwa na kuendelezwa kinyume na matumizi yaliyopangwa. Mmuya katika ziara hiyo alikagua maeneo ya wazi yakiwamo Medeli, Ndachi na eneo la Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, akisisitiza umuhimu wa kuyahifadhi kwa manufaa ya umma.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...