"UTALII"
Showing posts with label UTALII. Show all posts


Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKURUGENZI wa Mauzo wa Turaco Collection Tanzania, Florenso Kirambata, amesema kuwa maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kimataifa, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya utalii inayokua kwa kasi duniani.

Akizungumza wakati akiwasilisha hoteli za Turaco Collection katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Arusha, Florenso alisema tukio hilo linawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, ukarimu, safari na uwekezaji kutoka Tanzania na mataifa mengine duniani.

Maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 yanafanyika kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026 katika Viwanja vya Magereza, Arusha.

Florenso alisema Turaco Collection imeendelea kuimarisha uwepo wake nchini kupitia hoteli zake katika maeneo mbalimbali. Dar es Salaam kuna Element by Westin Dar es Salaam na Delta Hotels by Marriott Dar es Salaam, huku Kaskazini mwa Tanzania kukiwa na Turaco Ngorongoro Valley Lodge, Tribute Portfolio na Turaco Manyara View Lodge, Tribute Portfolio. Zanzibar, kampuni inamiliki Turaco Nungwi Resort, Tribute Portfolio, Turaco Spice Tree Stone Town, Tribute Portfolio pamoja na Beyt Al Salaam by Turaco.

Alieleza kuwa hoteli zote za Turaco Collection zinazobeba chapa za kimataifa zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya Marriott International, jambo linalochangia kuimarisha ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia za kisasa na utoaji wa uzoefu wa kiwango cha kimataifa kwa wageni wanaotembelea Tanzania.

Akizungumzia matumizi ya Akili Bandia (AI) katika sekta ya ukarimu, Florenso alisema Marriott International inaamini teknolojia hiyo inapaswa kuboresha uzoefu wa wageni kwa kuufanya kuwa wa kibinafsi zaidi, wenye ufanisi mkubwa na rahisi, huku ikidumisha misingi ya ukarimu unaozingatia mahusiano ya kibinadamu.

Alisema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika teknolojia za AI ili kuboresha mifumo ya uwekaji nafasi za malazi, shughuli za uendeshaji wa hoteli, programu za uaminifu kwa wateja na huduma mbalimbali za wageni.

“Teknolojia haitachukua nafasi ya ukarimu wa kibinadamu, bali itaongeza uwezo wa wafanyakazi wetu kutoa huduma bora zaidi. Mwelekeo wa Marriott International ni kutumia AI kuifanya safari ya mgeni, kuanzia kupanga safari, kuweka nafasi, kuwasili hotelini hadi kuondoka, kuwa rahisi, ya haraka na yenye uzoefu wa kipekee,” alisema Florenso.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano wake na Marriott International, Turaco Collection inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya teknolojia katika sekta ya ukarimu ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kisasa vya kimataifa.








Farida Mangube Morogoro
KATIKA hatua mpya ya kuimarisha sekta ya utalii nchini, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Hamis, amebainisha mkakati wa kipekee wa kuendelea kuwavutia watalii wanaotembelea Zanzibar kuongeza safari zao kwa kutembelea vivutio vya Tanzania Bara, hususan Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kutokana na upekee wake

Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo iliyopo mkoani Morogoro, Mhe. Hamida alisema ipo haja ya kutumia fursa ya wingi wa watalii wanaoendelea kumimina Zanzibar kama daraja la kuutangaza utalii wa Bara ikiwemo hifadhi za taifa kama Mikumi.

“Zanzibar ni lango kubwa la utalii, lakini tunataka wageni hawa wasiishie visiwani pekee bali wavuke na kuja kuona hazina ya vivutio tulivyonavyo Bara,” alisema.

Katika kile alichokiita uzoefu wa kipekee, Mhe. Hamida alieleza kufurahishwa na tukio la kuona simba ndani ya muda mfupi mara tu baada ya kuingia hifadhini hapo, Tena wakiwa chini ya Ndege zilizoegeshwa ndani ya hifadhi zinazotumika kuleta wageni Mikumi kutokea Zanzibar akisema hali hiyo inaonesha ubora wa vivutio vya Tanzania.

Aliongeza kuwa miundombinu iliyopo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, usafiri wa anga na barabara pamoja na miundo mbinu mizuri ya ndani inayofikika kirahisi licha ya Mvua, imeifanya Mikumi kuwa miongoni mwa hifadhi bora zinazofikika kirahisi kwa watalii wa ndani na nje.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza Wazanzibari kubadili mtazamo na kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani, akisisitiza kuwa utalii si wa wageni pekee bali ni fursa kwa Watanzania wote.

“Ni wakati sasa kwa Watanzania kuwekeza katika kujitambua na kuthamini vivutio vyetu; utalii wa ndani ni msingi imara wa sekta hii,” alisisitiza.

Aidha akawahimiza watanzania kutokea Upande wa Bara kutembelea vivutio vya Utalii wa Zanzibar ikiwemo utalii wa fukwe, kuogelea na dolphins na matamasha mbalimbali likiwemo la Kizimkazi ili kufurahia upekee uliopo.

"Hata Rais wetu Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar Dkt Husein Ali Mwinyi, wanahimiza utalii wa Ndani, Rais Samia alifanya Kazi kubwa kutangaza Royal Tour, tuwaunge mkono kivitendo viongozi wetu"Alisisitiza.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Masesa, alifichua kuwa idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo wanatoka Zanzibar.

Alisema hali hiyo inaashiria mafanikio ya juhudi za kuitangaza Tanzania kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo Royal Tour, huku akibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa zaidi ya kuongeza idadi hiyo kupitia ushirikiano wa pande zote mbili.

Alisisitiza kuwa Mikumi inaendelea kuwa kivutio muhimu kinachochochea utalii wa ndani na wa kimataifa, huku akiwakaribisha Watanzania na wageni kufika kujionea vivutio hivyo kwa macho yao wenyewe hasa kutokana na miundo mbinu Rafiki na inayofikika kirahisi ikiwemo Reli ya SGR, Barabara na ndege ambazo kutoka Zanzibar ni dakika 40 tu kufika.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Paulina Mkama akizungumza, leo Aprili 11,2026 jijini Dar es Salaam wakati w kutangaza vipengele vya kuwania tuzo za utalii na usafirishaji duniani.

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imeendelea kung’ara katika anga la kimataifa baada ya kuingiza vipengele 41 katika Tuzo za Utalii na Usafirishaji Duniani (World Travel Awards), hatua inayoimarisha nafasi yake kama moja ya vinara wa utalii barani Afrika.

Akizungumza, Aprili 11,2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Paulina Mkama, amesema tuzo hizo zinahusisha jumla ya washindani 85 kutoka sekta za umma na binafsi, zikilenga kutambua na kusherehekea ubora wa huduma, kuhamasisha ushindani na kutoa fursa kwa wadau na watalii kupigia kura vivutio bora duniani.

Paulina ameeleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika tuzo hizo ni fursa adhimu ya kuitangaza nchi kimataifa na kuiweka katika ramani ya dunia kama kitovu cha utalii.

Ameongeza kuwa taasisi za serikali, ikiwemo TFS na TAWA, zimefanikiwa kuwasilisha vivutio vyake katika kinyang’anyiro hicho.

Kwenye kinyang’anyiro hicho , Tanzania imewania nafasi katika vipengele mbalimbali barani Afrika, huku vivutio vikubwa kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vikitajwa kuwania tuzo za juu. Aidha, katika baadhi ya vipengele, washindani saba kati ya 14 wanatoka Tanzania, hali inayoonesha uimara na ushindani wa sekta ya utalii nchini.

Amebainisha kuwa sekta ya utalii inachangia zaidi ya ajira milioni moja kila mwaka, na mafanikio katika tuzo hizi yataongeza fursa za uwekezaji, ajira pamoja na kukuza pato la taifa.

Kwa sasa, kampeni ya “Kura Moja, Tiketi Moja kwa Tanzania” inaendelea, huku Watanzania na wadau wa utalii wakihamasishwa kushiriki kikamilifu kupigia kura nchi ili kuongeza nafasi ya ushindi.

“Mbali na kuimarisha ushindani wa ubora wa huduma, tuzo hizo pia huchochea ukuaji wa sekta ya utalii kupitia ubunifu, uwekezaji na kuongeza mvuto wa vivutio katika soko la kimataifa,” amesema Paulina.

Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza, baadhi ya vivutio vinavyosimamiwa na taasisi za serikali kama TAWA na TFS ikiwemo Mpanga Kipengere, Aman Forest Reserve, Selous Game Reserve, Pugu Kazimzumbwi na Kilwa Kisiwani, vimeingia kwenye ushindani huo, jambo linaloashiria kukua kwa sekta ya utalii nchini.



Picha za matukio mbalimbali.





UN Tourism imeitaja Tanzania kushika nafasi ya 11 duniani na nafasi ya sita (6) kwa Afrika na Mashariki ya Kati na kuwa miongoni mwa nchi 20 katika nchi zilizofanya vizuri zaidi katika sekta ya Utalii duniani. 

Ripoti ya Januari 2026 iliyotolewa na UN Tourism  imeangalia ongezeko la watalii wa Kimataifa kati ya mwaka 2019 na 2025.


Dar es Salaam, Mei 16, 2025 – Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), wamefanya mahafali ya kwanza ya programu ya mafunzo ya ukarimu kwa vijana chini ya mpango wa SBL wa "Learning for Life", wenye lengo la kuwajengea vijana wa Kitanzania ujuzi wa vitendo katika sekta ya ukarimu na utalii.

Mahafali haya, yaliyofanyika katika kampasi ya NCT jijini Dar es Salaam, yalikutanisha wanafunzi 109 waliohitimu, wadau wa sekta ya ukarimu, pamoja na viongozi wa serikali. Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, huku Mgeni Maalum akiwa ni Mhe. Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mpango huu ulioanza Septemba mwaka jana ni sehemu ya mkakati mpana wa SBL wa Society 2030: Spirit of Progress, ukilenga kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya vitendo, masomo darasani na mafunzo kwa vitendo kazini ili wawe tayari kuajiriwa kwenye soko la ajira linalokua la utalii na ukarimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Pindi Chana alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kupitia utalii shirikishi:

“Utalii siyo tu kusafiri – ni injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira kwa vijana na kubadilishana tamaduni. Tanzania inalenga kufikia watalii milioni 5 kwa mwaka, na programu kama hizi zinahakikisha tunajenga rasilimali watu sahihi kufanikisha lengo hilo.”

Alibainisha kuwa serikali imeanzisha vifurushi vipya vya vivutio vya utalii, vikiwemo utalii wa chakula, ili kutangaza utajiri wa vyakula vya asili vya Tanzania:

“Watalii wa leo wanatafuta uzoefu wa kweli. Sasa tunawaletea vyakula vya asili vya Kitanzania – ‘vyakula vya asili’ – kama sehemu ya vivutio vya utalii. Kutoka kwenye chakula safi, kisicho na kemikali moja kwa moja kutoka shambani, hadi vyakula vya kipekee vya mikoa mbalimbali, utalii wa chakula utawawezesha watalii kujifunza utamaduni wetu huku pia tukikuza uchumi wa jamii zetu,” alisema Waziri.

Aidha, Dkt. Chana alisisitiza kuwa utalii ni lazima uwe endelevu, shirikishi, na wenye manufaa kwa jamii, huku akipongeza ushirikiano kati ya SBL na NCT:

“Ushirikiano huu ni mfano wa ubunifu tunaouhitaji – ambapo vijana wanapewa ujuzi siyo tu wa ajira, bali wa kujenga taaluma endelevu zinazoweka mbele maadili, utamaduni na huduma bora kwa watalii wetu.”

Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, naye aliipongeza programu hiyo kwa kuchangia katika jitihada za serikali kukuza sekta ya utalii “Sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha ajira na kuchochea maendeleo ya taifa. Programu kama hii siyo tu kwamba inawapatia vijana wetu ujuzi, bali pia inasaidia kutekeleza dira ya serikali ya kugeuza utalii kuwa nguzo ya maendeleo jumuishi na endelevu. Nawapongeza SBL na NCT kwa dhamira yao ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kwa vitendo.”

Programu hii iliwafundisha wanafunzi ujuzi katika mawasiliano, uongozi, uwasilishaji binafsi, usimamizi wa muda, upangaji wa bajeti na huduma kwa wateja. Kupitia Diageo Bar Academy, walipata pia mafunzo maalum ya uendeshaji wa baa, huduma kwa wateja, na sanaa ya mchanganyiko wa vinywaji (mixology). Ili kuhakikisha uendelevu, SBL ilianzisha pia programu ya kuwajengea uwezo wakufunzi wa NCT (Training of Trainers – ToT), ili waweze kufundisha programu hiyo kwa kujitegemea kwa awamu zijazo.

Dkt. Obinna Anyalebechi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, alisema:

“Mahafali haya siyo tu kusherehekea mafanikio ya kitaaluma – bali ni wakati wa mabadiliko. Tunajivunia sana wanafunzi hawa na tunashukuru kwa ushirikiano wa NCT. Kupitia ‘Learning for Life’, tunafungua milango ya ajira na kuwawezesha vijana kufanikisha ndoto zao katika sekta ya utalii na ukarimu inayokua kwa kasi hapa Tanzania.”

Dkt. Florian Mtey, Mkuu wa NCT, alisifu mpango huo:“Programu hii imefungua milango kwa wanafunzi wetu. Inawapeleka nje ya darasa na kuwapa uzoefu halisi wa kazi, kuwajengea kujiamini na kuwafanya kuwa tayari kwa soko la ajira la leo. Tunajivunia ushirikiano huu na tunatazamia kuupanua zaidi.”

Mahafali haya ni ushuhuda wa mafanikio yanayopatikana kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya umma na binafsi, na ni sehemu ya dhamira ya SBL katika kuendeleza jamii kupitia programu jumuishi na endelevu. Programu ya Learning for Life itaendelea kufikia vijana zaidi na kuimarisha msingi wa sekta ya ukarimu kote nchini.












 

 

Na John Mapepele 

Kwa mara ya kwanza  katika historia ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani ya mwaka huu  hapa nchini yanayofanyika katika viwanja vya Saba Saba Mjini Njombe  Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa maonesho maalum ya mnyororo wa thamani wa sekta ya misitu pamoja na Wanyamapori.

Kwa vipindi tofauti wakikagua maandalizi ya siku ya Misitu Duniani kwenye maonesho Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Pindi chana na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi wamefafanua kuwa Serikali imeamua kuwaleta Wanyamapori katika maonesho hayo ili kutoa hamasa kwa wananchi kupenda utalii wa ndani.

" Tanzania imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la misitu takribani asilimia 50 ambalo ni makazi ya Wanyamapori, hivyo tumeamua kuwaleta wanyama  wananchi waweze kupenda kutembelea hivyo kuliingizia taifa letu fedha." Amepongeza Mhe. waziri 

Naye Dkt. Abbasi amewaarika    wananchi  kutembelea maonesho ya Wanyamapori  hao na kwamba  Serikali imetoa fursa ya wanyama hao kuendelea kuwepo katika viwanja hivyo katika siku za mwisho wa juma hata baada ya kilele hapo kesho ili wananchi wengi wapate fursa ya kuwaona.

Mgeni rasmi hapo kesho ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli mbiu ya kitaifa ya mwaka huu ni ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa raslimali kwa kizazi hiki na kijacho.









Turaco Collection yashiriki Maonyesho Makubwa ya Utalii yanayofahamika kama ITB -Berlin yaliyofanyika nchini Ujerumani tarehe 4-6 March 2025.

Mkurugenzi wa Mauzo wa Turaco Collection Tanzania, Florenso Kirambata akiziwakilisha hotel zao katika maonesho hayo ya ITB- Berlin anasema kwamba, maonesho hayo ni eneo jema kabisa la kujitangaza kubadilishana uzoefu hasa katika dunia ambayo walaji (watumiaji wa huduma) wamekuwa wakibadilika kutokana na mazingira yanayotokea duniani.

Turaco Collection kwa upande wa Dar es Salaam wana Element By Westin Marriott na Delta By Marriott na kwa upande wa utalii wa kaskazini pamoja na bidhaa mbalimbali za utalii pia wana; Turaco Ngorongoro Valley Lodge Tribute portfolio under Marriott International na Turaco Manyara View Lodge  Tribute portfolio under Marriott International na kwa Zanzibar wana Turaco Nungwi Beach Reasort  Tribute portfolio under Marriott International na Turaco Spice Tree Stone  Town Tribute portfolio under Marriott International na Beyt Aly Salaam-By Turaco.





Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA, kupitia mradi wa Anwani za Makazi (NaPA) imefanikiwa kusajili anwani za makazi za vivutio vya utalii 187 na barabara zaidi ya 60 zinazopatikana ndani ya Hifadhi tatu zilizofanyiwa kazi.

Katika zoezi hilo lililoendeshwa katika Hifadhi za Taifa za Arusha, Ziwa Manyara na Tarangire, WHMTH imefanikiwa pia kusajili huduma 221 na kujenga uelewa wa Mfumo wa NaPA na umuhimu wake kwa Menejimenti zote za Hifadhi husika.

Hayo yamebainishwa tarehe 10 Septemba, 2024 na Mratibu wa kitaifa wa Mradi huo kutoka WHMTH, Mhandisi Jampyon Mbugi kwenye kikao cha majumuisho ya zoezi la usajili wa Vivutio vya Utalii katika Mfumo wa NaPA kwenye Hifadhi za Taifa.
Viongozi na Wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) na Wahifadhi na Viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA, wakiwa kwenye kikao cha majumuisho ya zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Anwani za Makazi lililofanyika awamu ya kwanza katika Hifadhi za Arusha, Ziwa Manyara na Tarangire tarehe 10 Septemba, 2024 mkoani Arusha.

Viongozi na Wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) na Wahifadhi na Viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA, wakifuatilia wasilisho kwenye kikao cha majumuisho ya zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Anwani za Makazi lililofanyika awamu ya kwanza katika Hifadhi za Arusha, Ziwa Manyara na Tarangire tarehe 10 Septemba, 2024 mkoani Arusha.

Viongozi na Wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) na Wahifadhi na Viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA, wakifuatilia wasilisho kwenye kikao cha majumuisho ya zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Anwani za Makazi lililofanyika awamu ya kwanza katika Hifadhi za Arusha, Ziwa Manyara na Tarangire tarehe 10 Septemba, 2024 mkoani Arusha.


Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wataalamu wa Mfumo wa NaPA, baadhi ya Wahifadhi, Viongozi wa TANAPA na Wawakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Mbugi amesema, ukamilishaji wa zoezi hilo utawezesha kuwa na taarifa nyingi za vivutio hivyo na kuzidi kuvitangaza ili kuwavutia watalii kufika na kuvitembelea.

Kuhusu uwekaji wa miundombinu katika maeneo ya Hifadhi, Mhandisi Mbugi amesema, kwa kuwa NaPA una sehemu mbili, yaani kidijitali (digital part) na miundombinu (Physical infrastructure), ni muhimu sehemu ya miundombinu ikafanyiwa kazi kwa kuweka kulingana na taarifa zilivyoingizwa kwenye Mfumo wa NaPA, kwani kwa sasa taarifa zimekusanywa kwenye mfumo wa kidigitali pekee.

Amesema, kuweka mfumo wa miundombinu kutamrahisishia mtalii au askari kutambua na kuona kwa urahisi eneo alilohitaji kulitembelea au kulifanyia kazi.

Aidha Mhandisi Mbugi amesema, ili kuhamasisha matumizi ya Mfumo wa NaPA kwa watalii, ni muhimu TANAPA ikashiriki kikamilifu kutangaza na kuhamasisha matumizi yake katika masuala ya utalii kuwezesha kufikiwa kwa malengo na kupata manufaa yanayokusudiwa.

Ameshauri picha za vivutio ziwekwe kwenye Mfumo wa NaPA ili kumvutia Mtalii anapotafuta taarifa za Hifadhi husika kama picha hizo zinavyowekwa kwenye Mitandao (Website) za Hifadhi, na kusisitiza kuwa, uwekaji wa Miundombinu ya Anwani za Makazi katika majengo ya Ofisi, mageti na hoteli, uzingatie Mwongozo wa Anwani za Makazi wa Mwaka 2016, isipokuwa kwa maeneo mengine, uzingatie Sheria, Kanuni na Miongozo ya uhifadhi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Bw, Ignace Gara ameipongeza Wizara kwa utekezaji wa zoezi hilo na kwamba siyo tu ni msaada katika kutangaza utalii bali pia una faida katika ulinzi na uhifadhi wa wanyama adimu.