Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Patrick Rutabanzibwa.
Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, yuko matatani baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi, kumhukumu ama kulipa faini au kwenda jela kwa kitendo cha kuidharau amri halali ya mahakama hiyo.

Jaji Nchimbi wa Mahakama ya Ardhi alitoa hukumu hiyo Ijumaa dhidi ya Rutabanzibwa ama kulipa faini ya sh. 500,000 katika kipindi cha siku tano (hadi Alhamisi wiki hii), au kutumikia adhabu ya miezi sita kwenye gereza la Ukonga, endapo atashindwa kulipa faini hiyo.

Mbali na hukumu hiyo, Jaji Nchimbi pia aliwahukumu Kaimu Kamishna wa Ardhi, Bramsden Sichone na Mkurugenzi Mipango Miji, Albina Bura, kutumikia adhabu hiyo kutokana na kutenda kosa hilo la kudharau amri halali ya mahakama hiyo.

"Mahakama ina uwezo wa kutoa uamuzi wake dhidi ya wadaiwa watatu chini ya sheria ya mahakama," alisema Jaji Nchimbi alipokuwa akitoa uamuzi wake dhidi ya Rutabanzibwa na wenzake.

Baada ya kusoma hukumu hiyo, baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakamani hapo kusikiliza hukumu, walionesha kufurahi na wengine kushangilia, pengine kutokana na hivi karibuni katika kikao cha Bunge la Bajeti, baadhi ya wabunge kumshambulia Rutabanzibwa wakitaka aondolewe kwa madai ya ubadhirifu na urasimu, vitu vinavyotia doa utawala wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Mmoja wa mawakili waliobobea ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alidokeza kuwa kutokana na kosa hilo la jinai, endapo Rutabanzibwa na wenzake watalipa faini au kwenda jela, watapoteza haki zao zote za mafao kazini na hawatatakiwa kuendelea kuwepo ofisini, labda wakate rufani na kushinda.

Wakili huyo alidai vikao 12 vya Serikali vilifanyika ili kupata suluhu ya suala hilo na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewahi kumwandikia barua Rutabanzibwa mara kadhaa akimtaka kusaini hati za viwanja walivyokaidi, na hata akatishia kumchukulia hatua za kinidhamu, lakini Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amekuwa akikaidi.

Jaji Nchimbi alibainisha kuwa amri hiyo ilitolewa na mahakama hiyo kutokana na muafaka uliofikiwa baina ya kampuni za Oysterbay Properties Ltd, Kahama Minning Corporation Ltd, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamishna wa Ardhi kuhusiana na viwanja No 1272 na 1273 vilivyoko Msasani Peninsula, Dar es Salaam.

"Makubaliano yaliyofikiwa na pande zote mbili yaliifanya mahakama hiyo itoe tuzo kwa wadai kukamilishiwa viwanja hivyo na wadaiwa wote kwa pamoja," alidokeza na kuongeza tuzo hiyo ilikuwa ni amri halali kwa wadaiwa kuitekeleza bila ubishi wowote.

Jaji Nchimbi alisisitiza kuwa ni wajibu wa vigogo hao wa wizara hiyo kutii amri hiyo kwa kuwapatia hatimiliki ya viwanja hivyo wadai hao wawili, na pia wameagizwa kutoa hatimiliki hizo ndani ya siku tano.

"Wadaiwa hawana mamlaka ya kukataa amri halali ya mahakama," alisisitiza Jaji Nchimbi.

Aliongeza kuwa haikuwa sahihi kwa wadaiwa kukaidi amri hiyo kwa kisingizio cha utawala bora, vinginevyo walitakiwa kupeleka kiapo mahakamani kuonesha ni eneo la wazi.

Jaji Nchimbi alihitimisha hukumu yake kwa kuwatoza faini ya fedha hizo kila mmoja na wakishindwa kulipa ndani ya siku tano, waende jela kwa miezi sita kila mmoja.

Pia aliagiza vigogo hao wa Wizara ya Ardhi wawe wamesaini hatimiliki ya viwanja hivyo na kuwapatia wadai hati hiyo ndani ya siku tano.

Jaji Nchimbi alitoa hukumu hiyo mbele ya Wakili Mwandamizi wa Serikali (SSA), Obadia Kameya, wakili wa wadai, Aliko Mwananenge na Ofisa Uhusiano wa Kahama Minning Corporation, Francis Endeni.

Rutabanzibwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Mkurugenzi wa Kampuni ya kigeni ya Tangold Limited, amekuwa akishutumiwa kwa ufisadi.

Awali, aliwahi kujitetea kuwa wanaomtuhumu kwa ufisadi ni wale ambao yeye amewaripoti kwa DCI kutokana na tuhuma za uporaji wa viwanja vya mashirika ya umma na kuviuza kwa watu hewa ambao nao huviuza kwa wawekezaji binafsi au wafanyabiashara wakubwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Iam with Katibu Mkuu 100% huwezi kubatilisha matumizi ya ardhi mahakamni, cha msingi wao ni kukata rufaa. Halafu hawa Kahama mining wanatakaje umiliki wa ardhi wakati wao ni kampuni ya Kigeni. Jamani hivi vitu vitakuja kuumbua watu ukweli wake ukijulikana?

    ReplyDelete
  2. Hili suala liangaliwe kwa umakini zaidi. Sio rahisi kwa kiongozi wa Kitanzania (kadri niwajuavyo) kubishana na mkuu wake na mahakama. Aidha kanyimwa mgao au ni kweli ameona kuna kasoro katika matumizi ya ardhi ambayo anaizuia. Umakini ufanyike katika kuliamua hili ili mtu yeyote asionewe. Pia nakubaliana na mdau hapo juu, inakuwaje Kahama mining wamilikishwe ardhi??? Na mahakama inalibariki hili jamani???
    Na hiyo Kahama mining ibadilishwe jina, wasitumie "Kahama" ndani yake, wanaidhalilisha Kahama yetu kwa skendo zao zisizokwisha na zinazolindwa na wakuu kwa nguvu zote.

    ReplyDelete
  3. Wote wanaomchafua huyu Katibu mkuu, ndio wezi wakubwa wa ardhi na ndio wanaleta matatizo makubwa sana ya kubadulisha maeneo ya wazi kuwa viwanja na kuwadhulumu wanyonge haki yao.. ipo siku watu watachoka kitu ambacho sio kizuri kabisa..... Wapenda haki tumpe support Katibu Mkuu.. azidi kuwakalia kooni wezi hawa hata kama wana fedha nyingi. Tukiamua tunaweza.Wanajaribu kumnyamazisha lakini hawataweza . Mungu akutangulie Katibu Mkuu usichoke.

    ReplyDelete
  4. Ndugu Michuzi, watanzania wanatarajia uendelee kuwajuza kuhusu mwendelezo wa hili suala. Kama mwanahabari maarufu tungetegemea uwe unajua kipi kilichofuatia baada ya hukumu ya Jaji Nchimbi. Mbona hujatueleza kuhusu hatua ya Jaji Mkuu kuhusu hiyo hukumu? Unasubiri nini?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...