
MKUU wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Mhe. Mohamed Moyo amewataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kupanga bei mbili moja ya risiti na nyingine ya bila risiti jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mhe. Moyo amesema hayo leo tarehe 14.02.2025 ofisini kwake alipotembelewa na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika kujitambulisha kabla ya kuanza zoezi la kutoa elimu ya kodi mlango kwa mlango kwa wafanyabiashara wa Nachingwea mjini.
"Ninawasihi wafanyabiashara kuacha mara moja tabia ya kuuza bidhaa moja kwa bei mbili yaani anayedai risiti anauziwa kwa bei ya juu na asiyedai risiti anauziwa kwa bei ya chini, mtindo huu ni siyo mzuri na unashusha maendeleo ya nchi yetu."
Mhe. Moyo ameongeza kuwa, maendeleo yanayoonekana katika jamii kama vile barabara, ujenzi wa shule na miundo mbinu mbalimbali ni matokeo ya kodi inayolipwa na wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla na amesisitiza kwamba, hakuna taifa linaloweza kuendelea na kujitegemea bila ya wanachi wake kulipa kodi.
Bunge limepitisha nyongeza ya mapato na matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 945.7 kwa ajili ya kuongeza kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 kutoka shilingi trilioni 49.346 iliyoidhinishwa awali hadi shilingi trilioni 50.291.
Nyongeza hiyo imewasilishwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ambaye ameeleza kuwa fedha hizo zitakazotekeleza shughuli za sekta za elimu, afya utalii na program mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, zimepatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Alisema shilingi bilioni 325.9 zimetengewa Wizara ya Fedha, kwa ajili ya matumizi ya kitaifa, kugharamia malipo ya madeni ya watumishi, wakandarasi na wazabuni wa ndani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.
Mhe. Nchemba aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetengewa shilingi bilioni 131.4 kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya Mtaala mpya wa sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali, upatikanaji wa vifaa na walimu.
“Fedha hizo zitagharamia ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo vya VETA, ujenzi wa maktaba ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Nelson Mandela-Arusha, ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na ujenzi wa Jengo la Maktaba Mwanza”, alibainisha Mhe. Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa Wizara ya Afya imeongezewa shilingi bilioni 53.7 kwa ajili ya kugharamia dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeongezewa shilingi bilioni 173.7 kwa ajili ya sekta ya elimu, afya na kuiwezesha TARURA kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathirika na mvua za masika ili iweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema shilingi bilioni 260.7 zimetengwa kwa ajili ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili kugharamia uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Taasisi za Utalii za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA.)
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alisema mgawanyo huo umezingatia maono ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa kuhakikisha utekelezaji wa elimu ya amali ni unafanyika kwa vitendo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwasilisha bungeni nyongeza ya mapato na matumizi ya sh. bilioni 945.7 kwa ajili ya kuongeza Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025 kutoka shilingi trilioni 49.346 hadi sh. trilioni 50.291 iliyoidhinishwa awali na Bunge.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Fedha kutoka kushoto ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA, Leonard Mkude, Kamishna wa Idara ya Bajeti, Bw. Meshack Anyingisye na Kamishna wa Idara ya Sera Dkt. Johnson Nyella wakifuatilia wasilisho la Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), kuhusu nyongeza ya mapato na matumizi ya sh. bilioni 945.7 kwa ajili ya kuongeza Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025 kutoka shilingi trilioni 49.346 hadi sh. trilioni 50.291 iliyoidhinishwa awali na Bunge.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF- Dodoma)
Na Jane Edward, Arusha
Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wametakiwa kusimamia kikamilifu suala la lishe katika maeneo yao ili kuwa na Taifa lenye watu wenye afya bora pamoja na utimamu wa akili.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Dadi Kolimba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda katika kikao cha tathmini ya lishe Mkoa wa Arusha.
Kolimba amesema kuwa agenda ya Mheshiwa Rais ni kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na afya njema ili kuweza kusaidia kuwa na Taifa lenye watu waliosalama kiafya .
"Mheshiwa Rais ameingia mkataba na wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambapo imeenda mpaka kwa watendaji wa kata kwasababu ya usalama wa nchi yetu kuanzia usalama wa mama na mtoto kabla na baada ya kuzaliwa"Alisema
Aidha amewaeleza wadau hao wa lishe kuangalia afua za lishe kila wilaya kuona kama zinatekelezwa ili kuwa na tija.
Kwa upande wake Afisa lishe Mkoa Dotto Mirembe anasema kuwa taarifa ya utekelezaji ya viashiria vinavyosimamiwa na mkataba kwa kipindi cha July hadi Desemba 2024 hadi 2025 ambapo mkoa umeweza kutenga bajeti ya afua za lishe ambapo Mkoa umetenga kiasi cha shilingi Milioni 947 ambapo ni sawa na shilingi 2490.4 kwa kila mtoto.
Dotto amesema tathmini ya lishe kwenye ngazi ya kata Mkoa wa Arusha wanafanya vizuri kwa kuwa mpaka sasa wameweza kuvuka lengo la Taifa katika suala la lishe.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Charles Mkombachepa kwa niaba ya Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha Mussa Misaile amepongeza Afua za lishe kwa kuendelea kufanya vizuri na kuwataka kutobweteka na kuendelea kushika nafasi nzuri katika masuala ya lishe kimkoa.
Mwisho....
Na Jane Edward,Arusha
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya umishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ,ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao e-GA kuendelea kufanya tafiti ili kuleta bunifu kwa mifumo ya Tehama katika kuboresha utendaji kazi na kusaidia kuondoa kero ya upatikanaji wa huduma mbalimbali za serikali kwa wananchi.
Chawene ameyasema hayo wakati wa kufunga Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao e-ga kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa AICC jijini Arusha na kuhudhuriwa na wadau takribani 1500 wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA na watumiaji wengine wa mifumo ya TEHAMA kutoka katika Taasisi, Halmashauri na Mashirika mbalimbali ya Umma.
Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha na kuongeza matumizi TEHAMA ili kwenda sambamba na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa shughuli nyingi duniani ikiwemo za kiuchumi kwa sasa zinafanyika kwa kutumia TEHAMA.
Simbachawene amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA, hususani katika masuala ya utafiti na ubunifu, ili kuimarisha usalama wa Mtandao wa Mawasiliano na kuongeza watumiaji wa internet.
Alisema Wizara kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma kidijitali sambamba na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima, ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma kwa wakati na kwa gharama kupitia mifumo ya TEHAMA,
Waziri Simbachawene amezitaka taasisi za umma kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha zinatumia fursa ya ongezeko hili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kidijitali kupitia simu za mkononi.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu,Mulula Mahendeka amesema Vikao vinavyofanyika vimekuwa na manufaa makubwa katika kukuza na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao, kupitia mawazo mbalimbali yanayotolewa na washiriki wa vikao,
Mahandeka amesema Wizara, itasimamia utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa kwenye kikao hiki kwa wakati, ikiwa ni kwa Wizara yenyewe, e-GA au taasisi nyingine ya umma inayohusika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba aliwashukuru washiriki wote kwa umakini, utulivu na usikivu walioonyesha wakati wote wa kikao, hali ambayo imechangia kupata mawazö bora wakati wa majadiliano.
Alisema mawazo yaliyotolewa ni chachu katika maendeleo ya Serikali Mtandao, na Mamlaka itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa kwa kuwa na jitihada za Serikali Mtandao zenye tija zaidi.
Ndomba alisema mawazo jumuishi katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni chachu ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kidijitali, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu,
Mwisho
Serikali za
Tanzania na Algeria zimekubaliana kukuza diplomasia ya uchumi kwa
kutumia fursa muhimu za kiuchumi zinazopatikana katika nchi hizo mbili
ili kujenga ustawi wa watu wake.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo
(Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora
wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la
Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari,
2025 Addis Ababa, Ethiopia.
Viongozi hao wamejadili juu ya
umuhimu wa maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambapo mara ya mwisho
mkutano huo ulifanyika mwaka 2023 jijini Algiers, Algeria. Mkutano ujao
ulikubaliwa kufanyika mwaka 2025 nchini Tanzania hivyo, wamekubaliana
kuitisha mkutano mwingine mapema ili kuendana na makubaliano ya
kuanzishwa kwa tume hiyo yanaoelekeza kuitishwa kwa mkutano huo kila
baada ya miaka miwili ili kuruhusu ufuatiliaji wa utekelezaji katika
maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa.
Pia wamejadili kuimarisha
ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo, Mhe. Attaf ameahidi kuwa
Algeria itaendelea kutoa fursa za ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na
mfupi kwa lengo la kujenga uwezo na uzoefu katika masuala mbalimbali ya
kitaaluma na kitaalamu.
Vilevile wamesisitiza umuhimu wa kukuza
ushirikiano katika sekta ya biashara, nishati na kwenye masuala ya
ulinzi, usalama. Pia, uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea
itakayotosheleza mahitaji halisi ya wakulima nchini Tanzania na
kuwezesha kuyafikia malengo ya Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ya
kuongeza ajira kwa vijana na kufanya kilimo biashara.
Ushirikiano
katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ni miongoni mwa masuala
yaliyopewa msisitizo ili kuhakikisha nchi hizo mbili zinasimama imara
katika kuunga mkono masuala ya kimkakati na yenye maslahi kwa pande zote
katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.