Ndugu zangu,

JUMATANO hii ya leo kuna kusanyiko kubwa la watu kule Ifakara. Ni WaTanzania wanaoshiriki kumsindikiza kwenye safari yake ya mwisho, ndugu yetu mpendwa, Regia Estelatus Mtema.

Ni Jumatano hii ya leo, WaTanzania kwa mamilioni, nao, kwa kuelekeza fikra zao kwa Regia, wanashiriki kumsindikiza ndugu yetu Regia Mtema kwenye safari yake ya mwisho hapa duniani.

Katika maisha kuna visivyoshikika,visivyogusika, lakini vipo. Hisia, kwa mfano, zipo na zinaishi. Jumatatu usiku ya wiki hii nilifika nyumbani kwa wazazi wa Regia pale Tabata- Chang’ombe. Nilikwenda kutoa pole kwa wafiwa.

Regia alikuwa ni mmoja wa rafiki na dada zangu. Pale Tabata nilimwambia Remija, pacha wa Regia, kuwa niliongea kwa simu na Regia mara ya mwisho Jumapili iliyopita. Remija akanijibu;

” Nilikuwa nae wakati mkiongea!”

Ndio, mazungumzo yangu ya mwisho na Regia yalihusu ombi langu la yeye Regia, kwenye siku ya kutoa tuzo ya washindi wa mchakato wa kumtafuta mbunge bora kijana kwa mwaka 2011, mchakato ulioendeshwa na mtandao wangu wa kijamii wa Mjengwablog. com, atoe mada ya nusu saa juu ya nafasi ya mwanamke katika kushiriki uongozi na changamoto zake.

Kwamba mada hiyo ivuke mipaka ya siasa za vyama. Ilenge kwenye kuwajengea ari na moyo wa kujiamini wanawake vijana wa nchi hii. Regia alinikubalia ombi langu.

Ni Regia Mtema ambaye pia alipendekezwa na wadau wa mtandao wangu wa kijamii kushiriki na hatimaye kushika nafasi ya pili katika mchakato husika. Ni kwenye kundi la wanawake akiwa nyuma ya Halima Mdee. Nafasi ya tatu ilishikwa na Esther Bulaya.

Na hapa naungana na mwanasiasa kijana Nape Nnauye aliyesema; Regia Mtema alikuwa ni daraja kwa vijana bila kujali tofauti zao za kiitikadi.

Ni kweli, Regia alikuwa ni daraja. Katika dunia hii ni nadra sana kukutana na wanadamu wengi wenye urafiki na watu wawili walio kwenye uadui huku watu hao walio kwenye uadui wakilifahamu hilo na wakaendelea na urafiki wao na mtu huyo.

Nadharia iliyozoeleka ni ile ya ; rafiki wa adui yangu ni adui yangu. Kwa Regia Mtema nadharia hiyo haikufanya kazi. Regia ameweza kudhihirisha kinyume chake, kuwa adui yako anaweza kuwa rafiki wa Regia na wewe na Regia mkabaki kuwa marafiki. Ni watu wachache sana duniani waliojaliwa kuwa na sifa hizo.

Na kifo cha Regia kinathibitisha hilo. Kimewakusanya pamoja hata mahasimu. Kimewaleta pamoja hata wagombanao. Hakika, kumuenzi Regia kuliko na maana, ni kuendelea kuliimarisha daraja alilotujengea.

Tuache sasa siasa za ubaguzi. Wanadamu tunaweza kutofautiana katika hoja, lakini hatuna sababu za kuchukiana na kutakiana mabaya.

Na kuna wanaotaka kuutumia msiba wa Regia kujijenga kisiasa au kuwabomoa wenzao kisiasa. Naamini, Regia asingependa msiba wake utumike kwa kuendeleza ajenda za siasa za uhasama; kupandikiza chuki, kuleta migongano na hila nyingine.

Naam, katika maisha kuna visivyoshikika, visivyogusika, lakini vipo. Maana, jua laweza kuliangazia jiwe. Nalo jiwe likapata mwanga. Likapata joto pia. Lakini, jua laweza kuliangazia jicho lako, nalo likapata joto. Hata hivyo, kwa mwanadamu, kuna unachoweza kukifanya ambacho jiwe kamwe haliwezi kukifanya. Ndio, unaweza kulitazama jua kwa jicho lako. Jiwe huangaziwa mwanga wa jua, litapata joto, lakini jiwe haliwezi kulitazama jua.

Juzi usiku pale Tabata nilipokaa na kuzungumza na Remija, pacha wa Rejia, kuna mwanga niliouona. Nilimwona Remija akiinamisha kichwa na kufikicha macho yake yaliyokuwa yakilengwa na machozi.

Kisha nikamwuliza; wewe na Regia mlikuwa mkigombana utotoni? Na kwanini wewe hupendi siasa na mwenzako alipenda sana siasa?

Remija akanitazama kwa macho yake makubwa na yenye mvuto. Kisha akaangua kicheko. Hapo nikamwona Regia. Wamefanana sana.

Niliuona mwanga unaongazia jiwe, nalo jiwe likapata joto. Ni vile visivyoshikika, visivyogusika. Lakini, ni vyenye kuamsha hisia. Vyenye kuleta mwanga kunako giza. Vyenye kuleta matumaini katika hali ya kukata tamaa.

Regia amewapigania wengi. Amewaletea matumaini walo wengi. Ni wale walio katika hali ya kukata tamaa.

Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Marehem MtarajiwaJanuary 18, 2012

    Sasa hapo ulichotaka kutueleza ni nini? mbona story ndefu lakini haina kichwa wala mguu!? hapo mimi nilichokiona nikama tu umemtamani pacha wa marehem(Remija)unasababu gani ya kusifia macho yake kua niyenye mvuto wakati habari hapo niyakifo cha Regia?jamani kama hamna vyakuandika,msijaze nafasi za watu wanaoleta maada za maana.

    ReplyDelete
  2. AMEN! ila hiimakala imeandikwa na nani? hajajitaja

    ReplyDelete
  3. halafu alivyomuuliza kama yeye remija anapenda siasa hajatoa jibu alilomwambia hatakama alilia ilibidi atoe jibu

    ReplyDelete
  4. Hata mie nimeshangazwa na mtoa mada kuanza kusifia macho tena!

    ReplyDelete
  5. Utamu wa fasihi: Ni matumizi ya lugha tamu kufikisha ujumbe mzito.Lazima ujue fasihi kuuelewa ujumbe vinginevyo utaonekana 'unajaza ukurasa', patamu hapo. Hata hivyo, mwandishi uitambue hadhira unayoifikishia HABARI HIYO, vinginevyo hawatakuelewa akina 'marehemu mtarajiwa'.Pole.
    Kwa ufupi: Mwandishi hana maana ya hisia ya mapenzi ILA kwamba Remija, ambaye ni pacha wa Regia, anaweza kuja kuwa mwanasiasa wa mfano wa Regia kwa namna anavyo shabihiana sana na pacha wake wa mambo mengi. Yeye ni 'vile visivyo shikika, visivyogusika lakini ni vyenye kuamsha hisia. Vyenye kuleta mwanga kunako giza na kuleta matumaini katika hali ya kukata tamaa'.

    ReplyDelete
  6. michuzi onyesha mwandishi wa mada hii umesahau, ni mjengwa ameiweka na kwenye blog yake

    ReplyDelete
  7. Hii makala haina kichwa wala miguu so what mwandishi unataka kutueleza hatutaki porojo humu ndani ama!

    ReplyDelete
  8. Hii makala ni kama Mixed Grill.

    ReplyDelete
  9. Mimi sikuwahi kukutana na marehemu Mh. Regia Mtema. Nilikuwa nasikia sifa zake na nilikuwa na matumaini kuwa atafanya mengi na mema katika ujenzi wa taifa. Mungu kamchukua mapema mno kama alivyowachukua Amina Chifupa na Prof. Crispin Hauli.

    Mwenyezi mungu apumzishe roho ya Regia mahala pema mbinguni. Amen.

    ReplyDelete
  10. alikuwa anachukua mazoezi ya isha jamani

    ReplyDelete
  11. Pamoja na makosa yote yanayoonekana kiuandishi siachi kukubaliana na mwandishi wa makala hiyo kuwa msiba huu kweli umeleta watu wote pamoja na hiyo inadhihirisha maisha ya Regia yalivyokuwa na mguso mkali kwa jamii yetu.

    ReplyDelete
  12. Kuna jambo haliongelewi hapa. Marehemu alikuwa amekatwa mguu wa kulia. hebu jaribu kuendesha gari kwa kutumia mguu wa kushoto hata kama ni la automatic. Halafu safari yenyewe ilikuwa ndefu. Jamani sio tu kwamba alikuwa anahatarisha maisha yake bali hata ya watumiaji wengine wa barabara. Jamani ndugu zetu wenye ulemavu wa macho au miguu kuweni makini.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...