Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha..

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).

Marburg ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu haki­julikani. Hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na ha­raka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

o   Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.    

o   Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.

o   Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu. 
Kitengo cha mawasiliano ya Serikali

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Nashindwa kuelewa, mbona haya magonjwa hatari sana yanatokea Uganda??? Chanzo chake huko Uganda ni nini na kwa nini kisidhibitiwe kwa ushirikiano na nchi mbali mbali, hasa nchi jirani???

    ReplyDelete
  2. washausambaza wazungu ungonjwa huu sehemu kibao ambazo wanataka kuzi tawala kiuchumi kwa husda ya kuona uchumi upo
    hajishangainga waifrika kila siku sisi na kila kibaya ni chetu chao ni kizuri toka lini mkasikai magonjwa haya jeulizeni?

    africa ni nchi tajiri kuliko zote duniani na wazungu na wenginewe wanakodolea macho uchumi wenu

    kalaba bao kaeni hivyo hivyo kujiharibu akilizenu kwa mipombe na mibangi na madawa ya kulevyaa wenzenu pia wanataka mharibikiwe ili watukawaleni daimi maishani

    poleni sana ugonjwa huu umeshafika tanzania chunguzeni mtaona kama nakudanganyeni

    ReplyDelete
  3. Lohhh kwa misongamano yetu Mijini hapa Afrika ya Mashariki ktk Masoko, kama Vivuko vya Feri kwenda Kigamboni rundo la watu, vyombo vya Usafiri kama mabasi makubwa ya Mchina njia za Mbagala, Gongo la Mboto na Tegeta, tutakiwisha sana dude hili likiingia Tanzania!

    MUNGU TUSAIDIE!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...