KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tabora,amewaagiza waganga wakuu wa wilaya za Mkoa huo kuhakikisha kwamba wanaume wote watakaougua na kulazwa Hospitalini kwa ugonjwa wowote ule,wawaambie kuwa ugonjwa huo unatokana na uchafu unaotoka kwenye sehemu za siri za mwanaume huyo kutokana na kutofanyiwa tohara.

Katibu Tawala huyo,Dk.Thea Ntala alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na madiwani pamoja na watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga kwenye mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

“Nimewaagiza waganga wakuu wote wa wilaya kuwa mgonjwa yeyote mwanaume akiwepo Mheshimiwa diwani,akiwepo mheshimiwa mbunge wakilazwa pale Hospitali awe anaumwa jino,awe anaumwa sikio,awe anaumwa mkono mwambie hivi hili tatizo lako linatokana na uchafu unaotoka kwenye sehemu za siri kwa kutofanyiwa tohara”alisisitiza katibu tawala huyo.

Kwa mujibu wa Dk.Ntala haiwezekani katika Mkoa wa Tabora wakaendelea kukaa na wanaume ambao mpaka sasa bado hawajafanyiwa tohara kwani kuendelea kukaa na watu wa aina hiyo kunachangia kwa namna moja au nyingine ongezeko la maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

“Hatuwezi kukaa Tabora,hatuwezi kukaa na hicho kitu na ndiyo maana ugonjwa huu wa Ukimwi unaendelea kutokana na sababu za kuendelea kuwepo kwa watu wasiofanyiwa tohara,nimewaagiza MADMO,RMO hili nimewaagiza wote Tabora kuhakikisha wanawafanyia uchunguzi wanaume wote wanaolazwa iwapo wamefanyiwa tohara”alifafanua huku akiwaacha waliohudhuria mkutano huo wakiangua kicheko.

Hata hivyo Dk.Ntala alibainisha kwamba hivi sasa baadhi ya wanaume wamekuwa wakihudhuria kwenye semina kupatiwa elimu ya juu ya umuhimu wa kufanyiwa tohara huku wengine wakiamua kwenda kwa hiyari yao kufanyiwa tohara hiyo kwenye maeneo yanayotoa huduma hizo.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa mabusha,Dk.Ntala alitumia fursa hiyo kuwashauri wanawake kumeza dawa kwani dawa za ugonjwa huo zinatakiwa kumezwa na wanaume pamoja na wanawake na kuonya dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii ya kuamini kwamba ugonjwa wa mabusha hauwahusu wanawake bali unawahusu wanaume peke yao.

“Madiwani mnisaidie kwenye mikutano wanawake wanafikiri ukiongelea ugonjwa wa mabusha ni wanaume,aah mwanamke anapata mabusha kwenye matiti yaani badala ya kuwa na saizi ya kawaida kama ya RAS anakuwa na saizi kubwa kama tikitimaji fulani hivi…sijui kama kuna watu wanapenda magodoro makubwa”alibainisha katibu huyo tawala.



Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya igunga,mkoani tabora wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo

Mbunge wa jimbo la Manonga,wilayani Igunga,mkoani Tabora,Mhe.Hamisi Gullamali(wa kwanza kulia) wakiteta jambo na katibu wake wakati wa mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
Jengo la ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora, mahali kulikofanyikia mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani.
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora,Dk.Thea Ntala akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na madiwani,watendaji wa Halmashauri ya wilaya pamoja na viongozi wa chama na serikali waliohudhuria mkutano huo wa kawaida wa Baraza la madiwani uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...