Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na
Mwenyekiti wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari (hayupo pichani) pindi
ujumbe kutoka Taasisi hiyo ulipomtembelea Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani
jijini Dar es Salaam.
Maafisa kutoka MISATAN-Tanzania, (kushoto), Mwenyekiti, Bi. Salome
Kitomari na Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema Kasabuliro kwa
pamoja wakinukuu masuala yaliyokuwa yakitolewa na Mhe. Jaji Mkuu.
Mwenyekiti wa MISATAN-Tanzania, Bi. Salome Kitomari akizungumza jambo na Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani).
Mhe. Jaji Mkuu akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo. Wa pili
kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya
Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa kwanza kushoto ni Katibu wa Mhe. Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Adrian Kilimi, kulia ni Maafisa kutoka MISATAN na Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka MISATAN-Tanzania na baadhi ya Watumishi
wa Mahakama walioshiriki katika mazungumzo hayo, wa pili kushoto ni Mwenyekiti
wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari, wa pili kulia ni Mkuu wa Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa
kwanza kushoto ni Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema
Kasabuliro na wa kwanza kulia ni Salum Tawan, Mkutubi-Mahakama ya Tanzania.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISATAN) pamoja na vyombo
vya habari nchini kuitekeleza ipasavyo Sheria
namba 6 ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016.
Akizungumza na
Mwenyekiti wa MISATAN Tawi la Tanzania, Bi. Salome Kitomari, mapema Oktoba 08,
2019 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema Sheria hii
itumike ipasavyo kudai taarifa.
“Tumieni sheria
hii kudai taarifa, sheria inatoa shurti ya kutoa taarifa zinazotakiwa na umma,
hivyo suala la kutoa taarifa sio fadhila ni amri kwa hivyo ni vyema kuangalia
ni kwa namna gani tunatumia Sheria hii kushurutisha utoaji wa taarifa,”
alibainisha Mhe. Jaji Prof. Juma.
Mhe. Jaji Mkuu
aliongeza kuwa ili kutekeleza sheria hii ipasavyo ni wajibu wa kila mmoja
kutimiza wajibu wake, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza takwa la kikatiba
na kisheria.
Kwa upande
mwingine, Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia pia suala la Vyombo vya habari nchini
kuandika Habari za uchunguzi ‘Investigative Journalism’badala ya kutegemea
habari zitokanazo matukio mbalimbali.
“Ni muhimu pia
kufanya habari za uchunguzi kwa kuchagua mada maalum ‘agenda setting’
itakayokuongoza kufanya utafiti, kwa kufanya hivi itasaidia kupunguza
malalamiko na vilevile itasaidia kuwa na habari zenye usahihi zaidi ‘accurate’,
alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa MISATAN-Tanzania, Bi. Salome Kitomari alimueleza Mhe. Jaji Mkuu
kuwa Taasisi yake imekuwa na uhusiano mzuri na Mahakama katika maeneo
mbalimbali.“MISATAN kwa
kushirikiana na Mahakama tumefanikiwa kutoa mafunzo ya Huduma kwa Mteja
‘Customer Care’ kwa zaidi ya Watumishi 350 wa Mahakama,” alieleza Bi. Kitomari.
Hata hivyo;
Mwenyekiti huyo alishauri mafunzo haya ni vizuri kutolewa pia kwa Watumishi wa
Mahakama wa ngazi za juu wakiwemo Majaji na Mahakimu.
Aidha; Bi.
Salome aliongeza kwa kupendekeza kufanyika kwa Mkutano kati ya Mahakama,
MISATAN na Taasisi nyingine za Habari lengo likiwa ni kujenga imani na
uwajibikaji kwa taasisi zote.Ujumbe huo wa
MISATAN umemtembelea Mhe. Jaji Mkuu kwa lengo la kuitambulisha rasmi Taasisi
hiyo, kuishukuru Mahakama kwa kufanya kazi kwa karibu na MISA Tanzania ikiwa ni
pamoja na kujadili maeneo ya uhusiano baina ya Taasisi hizi kwa miaka ijayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...