Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuzindua ofisi ya ardhi
mkoa wa Geita jana. Wa tatu kulia ni Mbunge wa jimbo la Bukombe mkoa wa
Geita ambaye ni Waziri wa Madini Doto Biteko na wa pili kushoto ni Mkuu
wa wilaya ya Geita Josephat Maganga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akionesha hati ya ardhi ya kwanza
kutolewa katika mkoa wa Geita mwaka 1976 ambayo tayari imehamishiwa
ofisi ya ardhi ya mkoa wa Geita wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi katika
mkoa huo jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia moja ya majalada ya ardhi
katika ofisi ya masijala ya ardhi mkoa wa Geita alipokwenda kuzindua
ofisi ya ardhi mkoa wa Geita jana. Kushoto ni Mbunge wa jimbo la Bukombe
na Waziri wa Madini Doto Biteko na wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Geita Josephat Maganga na kulia ni Msajili wa Hati Msaidizi ofisi ya
ardhi Mkoa Revina Kayanda.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza mmoja wa wananchi wa
mkoa wa Geita aliyewasilisha kero ya ardhi kwake wakati wa uzinduzi
ofisi ya ardhi katika mkoa wa Geita jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi hati ya ardhi Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Geita Mji Mhandisi Modest Apolinary wakati wa uzinduzi
ofisi ya ardhi katika mkoa wa Geita jana. Lukuvi aliagiza wakurugenzi
wa halmashauri zote nchini kupima na kumilikishwa maeneo yao ili kuepuka
migogoro ya ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akielekea kuzindua ofisi ya ardhi
mkoa wa Geita jana huku akiangalia vifaa vya upimaji wakati wa mfululizo
wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
……………………………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM GEITA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi katika ofisi za ardhi za mikoa
nchini kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wasioendeleza viwanja vyao
tangu kumilikishwa hawahuishi miliki zao za miaka 33 ili kupatiwa za
miaka 99.
Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Geita wakati akizindua
ofisi ya ardhi mkoa wa Geita ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi
hizo nchini. Uzinduzi wa ofisi ya ardhi Geita umeenda sambamba na ule wa
mkoani Kagera uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula.
Alisema, kuna wamiliki wa ardhi katika maeneo mbalimbali
katika mikoa wameshindwa kuchukua hati za viwanja na wengi viwanja vyao
ni vya miaka 33 na kutolea mfano wa mkoa wa Geita wenye zaidi ya
wamiliki 30,000 huku baadhi yake wakishindwa maendelezo yoyote jambo
alilolieleza limeikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
” Nawaagiza Makamishna Wasaidizi wa ardhi wa mikoa
kuhakikisha wamiliki woteb wa ardhi wasioendeleza maeneo yao
wasihuishwe hati zao, kama kwa muda wa miaka 33 umeshindwa kuweka hata
tofali huwezi kujenga tena, hatukutoa ardhi kwa mtu kama land bank”
alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wananchi walioendeleza viwanja
vyao Makamishna wa mikoa wanatakiwa kuhakikisha hati zao za miaka 33
zinahuishwa na kupatiwa zile za miaka 99 ili waweze kuzitumia kwa
shughuli za kiuchumi kama kuchukua mikopo ya muda mrefu benki.
Sambamba na hatua hiyo, Waziri Lukuvi aliwataka Makamishna
Wasaidizi wa ardhi katika ofisi za ardhi za mikoa kumpatia gharama
halisi za upimaji kufuatia usambazaji vifaa vya upimaji uliofanywa na
wizara yake kwenye ofisi hizo.
Alisema, kwa sasa gharama za upimaji katika halmashauri
mbalimbali za wilaya hazina uhakika kutokana na kila eneo unapofanyika
upimaji kuwa na kiwango chake alichokieleza kuwa kinawaumiza sana
wananchi hasa wale wanyonge.
” haiwezekani serikali inunue vifaa vya zaidi ya bilioni 3
halafu mwananchi anaumizwa, yaani vifaa vya upimaji vinakodishwa na
halmashauri kwa makampuni kwa gharama ya shilingi laki mbili na nusu
kwa siku na gharama hizo anazibeba mwananchi ni lazima gharama zishuke
sasa” alisema Lukuvi.
Aidha, Waziri wa ardhi alisema, kuanzia mwakani wizara yake
itaanza mradi mkubwa wa kupima kila kipande cha ardhi na hati kutolewa
kwa mfumo wa kidijitali unaowezesha mwananchi kumilikishwa hati ya
kielektroniki ya kurasa moja.
Akizungumzia suala la urasimishaji makazi katika maeneo
mbalimbali nchini, Waziri Lukuvi aliagiza wananchi wote waliojenga
maeneo hatarishi kama vile mabondeni wasirasimishiwe na badala yake
maafisa mipango miji waangalie upya ramani zake ili wazirekebishe.
” aliyejenga eneo hatarishi asipewe hati na wapanga miji
mrudi kutoa ramani, mvua zimeshusha hadhi yenu na kuonesha mafuriko,
futeni katika mpango wenu maeneo yaliyoathirika msiyapange na walio
mabondeni wasirasimishiwe” alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga
aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alisema
kupitia uzinduzi wa ofisi ya ardhi, mkoa huo sasa utafaidi kwa
kusogezewa huduma za sekta ya ardhi karibu ambapo awali zilikuwa
zilikuwa zikipatikana ofisi ya kanda uliyokuwemo mkoa wa Mwanza na
kutolea mfano upatikanaji hati ulilazimu mwananchi kusafiri hadi Mwanza
na kumuingizia gharama.
Mkuu huyo wa wilaya ya Geita alibainisha kuwa, kupatikana kwa
huduma zote za sekta ya ardhi katika mkoa wa Geita sasa miji katika mkoa
huo itapangika vizuri na maeneo yaliyoiva kimji itapangiliwa vizuri.
Naye Mbunge
wa Bukombe ambaye ni Waziri wa Madini Doto Biteko aliishukuru Wizara ya
ardhi kwa uamuzi wa kufungua ofisi za ardhi za mikoa pamoja na kutatua
migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo ni furaha
kwa wana Geita kwa kuwa hatakuwa wakisafiri tena umbali mrefu kufuata
huduma ya ardhi Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...