Na Muhidin Amri, Tunduru

WAKULIMA wa zao la korosho wanahudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu Ltd),wamejipatia Sh.bilioni 40.8 baada ya kuuza tani 20,200 za korosho ghafi katika minada mitano iliyofanyika kwa mfumo wa stakabadhi gharani.

Hayo yalisemwa jana na meneja mkuu wa Chama hicho Iman Kalembo,wakati akitoa taarifa ya mauzo ya korosho za wakulima tangu mnada wa kwanza ulipofunguliwa tarehe 2 Novemba mwaka huu katika kijiji cha Nakapanya wilayani humo.

Alisema,katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 malengo ya Chama hicho ni kuzalisha tani 25,000 lakini hadi sasa wamefanikiwa kukusanya na kuuza jumla ya tani 20,200 kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) ambapo wastani wa bei ni Sh.1,750 kwa kilo moja.

Kalembo alisema,wana matumaini makubwa ya kuvuka lengo la uzalishaji kwa kuwa baadhi ya wakulima bado wako mashambani wanaendelea na kuokota na kukusanya korosho kabla ya kuzipeleka kwenye maghala ya vyama vya msingi kwa ajili ya kuuza.

Aidha alisema,katika msimu uliopita 2021/2022 wakulima walizalisha kiasi cha tani 15,000 tu ambazo ni kidogo ikilinganisha na mwaka huu,hata hivyo bei ya korosho katika msimu huo ilikuwa ya kuridhisha ambayo ni Sh.2,000 ikiwa ni tofauti ya Sh. 300.

Kalembo,amewapongeza wakulima wananaohudumiwa na Tamcu kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam yaliyosaidia kuongeza uzalishaji na kupata korosho zenye ubora mkubwa ambapo tangu mnada wa kwanza ulipofunguliwa korosho zote zilizouzwa ni za daraja kwanza.

Hata hivyo,Kalembo amewaomba wafanyabiashara kuongeza bei ya kununulia korosho ili wakulima waweze kunufaika na zao hilo kwa kuwa gharama za uzalishaji ni kubwa na itawahamasisha wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao.

Ameishauri bodi ya leseni za maghala hapa nchini, kutoa leseni chache kwa ajili ya wasimamizi wa maghala,badala ya kutoa leseni nyingi ili kudhibiti ubora wa korosho zinazopelekwa kwa wamiliki na waendesha maghala wasiokuwa waaminifu.

Mmoja wa wakulima wa korosho wilayani humo Issa Lada,ameipongeza serikali kutoa pembejeo za ruzuku zilizohamasisha watu wengi kujikita katika shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji wa zao hilo katika msimu 2022/2023.

Hata hivyo,ameiomba kutafuta na kusimamia suala la soko la korosho ili wakulima wapate bei nzuri zitakazolingana na gharama za uzalishaji.

Mwenyekiti wa chama cha wachukuzi Bakari Hassan,ameitaka serikali kuhakikisha inapeleka pembejeo kwa wakulima kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha ili wakulima waweze kujiandaa na msimu mpya wa kilimo 2023/2024.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu Ltd) Iman Kalembo, akitoa taarifa ya mauzo ya zao la korosho za wakulima wanaohudumiwa na chama hicho kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)ofisini kwake mjini Tunduru.
 

Baadhi ya malori yakisubiri kubeba shehena za korosho zinazozalishwa na wakulima wanaohudumiwa na Chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...