JK akiangalia mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi alipouzindua huko Ubungo, Dar. Pamoja naye ni meneja wa mradi huo, Ambakisye Mbangula

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UZINDUZI WA MTAMBO WA GESI KUZALISHA UMEME WA UBUNGO, DAR ES SALAAM, NOVEMBA 4, 2008

Mheshimiwa William Mganga Ngeleja (Mb),
Waziri wa Nishati na Madini;
Ndugu Peter Joram Ngumbullu, Mwenyekiti wa
Bodi, TANESCO;
Waheshimiwa Mabalozi;
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Warstila;
Waheshimiwa viongozi na watendaji mbalimbali;
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Waziri na uongozi wa Shirika letu la umeme (TANESCO), wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kwa kunialika katika tukio hili la kihistoria katika uhai wa Shirika letu la Umeme nchini. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii ya leo.
Nawapongeza pia waliofanikisha ujenzi wa mtambo huu. Mmefanya kazi kubwa na nzuri sana.
Mheshimiwa Waziri na Ndugu Wananchi;
Nimefurahishwa sana na sherehe hii ya leo kwani dhamira yangu na yetu sote imetimia. Mtakumbuka kuwa Serikali yetu ilipoanza moja ya mambo makubwa tuliyolazimika kuhangaika nayo mwaka 2006 ni upungufu mkubwa wa umeme nchini. Upungufu huo ulisababisha kuwepo kwa mgao mkubwa wa umeme ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.
Niliwaeleza wananchi wakati ule kuwa miongoni mwa mambo ambayo tumeamua kufanya katika mkakati wa kukabiliana na kumaliza tatizo la upungufu wa umeme nchini ni kuongeza matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme. Wakati ule tulikuwa na tatizo la uhaba wa umeme kwa sababu ya maji kupungua sana katika mabwawa yetu ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Mtera, Kihansi, Pangani, Hale na Nyumba ya Mungu. Bahati nzuri tunayo akiba ya kutosha ya gesi asilia tunayoweza kuitumia kuzalisha umeme na kusaidia kukabiliana na tatizo hili. Ndipo tukafanya uamuzi wa kuongeza umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia.
Wakati ule umeme unaotokana na gesi ulikuwa unazalishwa na kampuni ya Songas, kiasi cha megawati 190. Azma yetu ilikuwa kuongeza umeme huo kwa sababu hauathiriwi na mvua au jambo lingine lolote isipokuwa labda gesi asilia imalizike au mitambo iharibike kama ilivyotokea wiki chache zilizopita.
Tuliamua wakati ule kufanya mambo mawili. La kwanza tukodishe mitambo ya kuzalisha umeme, na la pili tujenge mitambo yetu wenyewe ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia. Yote mawili tuliyatekeleza. Kwa upande wa kuwa na mitambo yetu wenyewe tuliamua ifuatavyo:
Kujenga kituo cha kuzalisha megawati 200 pale Kinyerezi;
Kujenga kituo cha kuzalisha megawati 100 hapa Ubungo;
Kujenga kituo cha megawati 45 kule Tegeta;
Lingine ambalo halikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na tatizo la uhaba wa umeme bali kupunguza gharama kwa TANESCO ni kuigeuza mitambo ya IPTL inayotumia dizeli hivi sasa itumie gesi.
Nafurahi kuja kushuhudia mafanikio ya utekelezaji wa maamuzi yetu kwa uzinduzi wa leo wa kituo hiki. Azma yetu ya kujenga kituo cha kuzalisha megawati 100 hapa Ubungo imetimia. Nafurahi pia kusikia kwamba kituo cha Tegeta nacho kitakamilika mapema mwakani. Aidha, nafurahi kusikia kuwa mchakato wa ujenzi wa kituo cha Kinyerezi unaendelea.
Kwa kuwepo kituo hiki uwezo wetu wa kukabiliana na tatizo la kupungukiwa umeme kwa sababu ya mabwawa kukosa maji ya kutosha sasa umeongezeka. Haya ni mafanikio makubwa kwa kupata mtambo huu. Bado tutaendelea na juhudi hizo za kuongeza kiwango cha umeme unaozalishwa kwa gesi asilia.
Kuhusu kuigeuza mitambo ya IPTL kutumia gesi asilia badala ya kutumia dizeli, kasi yake si ya kuridhisha kwa sababu ya kukosa ushirikiano wa kuridhisha kutoka kwa wawekezaji. Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wawekezaji hao kuwa watoe ushirikiano wa kutosha ili kasi iongezeke katika zoezi hilo.
Kadhalika, ile Kamati ya Serikali ya kushughulikia uwezekano wa kuinunua mitambo ya IPTL nayo iongeze kasi ya kufuatilia na kutekeleza ununuzi huo. Tukifanikiwa kuinunua mitambo hiyo tutakuwa tumepunguza mzigo mkubwa wa gharama kwa TANESCO.
Napenda pia kuitumia nafasi hii kuihimiza Wizara ya Nishati na Madini na Kamati ya Serikali ya Majadiliano na Kampuni ya Artumas ya kule Mtwara kukamilisha mazungumzo yanayoendelea kuhusu ushirikiano baina ya TANESCO na Kampuni hiyo. Mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu mno. Makubaliano na kampuni hiyo yatafungua njia ya uwekezaji katika kuzalisha umeme mwingi zaidi kwa matumizi ya mikoa ya Lindi na Mtwara na kuiingiza katika gridi ya Taifa. Pia itaharakisha kazi ya usambazaji umeme katika wilaya za mikoa hiyo miwili.
Mheshimiwa Waziri;
Natambua na kuipongeza Wizara yako na TANESCO kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kuendelea kuongeza uzalishaji umeme, kutandaza gridi ya taifa ya umeme na kuyapatia umeme maeneo ya vijijini hapa nchini. Nawaomba muendelee na juhudi hizo. Kadhalika naiomba Wizara ya Fedha iendelee kuwapa ushirikiano wa karibu katika upatikanaji wa fedha za kutekeleza kazi hiyo kubwa na muhimu kwa maendeleo ya taifa letu. Pale mtakapohitaji msaada wangu tafadhali msisite kuniambia.
Mheshimiwa Waziri;
Nafurahi kwamba Wakala wa Umeme Vijijini umeshaanzishwa na umeanza kazi. Nimefurahi zaidi kusikia kuwa katika hatua za awali za kutekeleza mpango wa usambazaji wa umeme vijijini, mitambo 17 ya dizeli yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 31 imenunuliwa ili ifungwe kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa. Maeneo hayo ni Loliondo, Kigoma, Kasulu, Kibondo na Sumbawanga.
Napenda kuwaahidi kuwa tutaendelea kuongeza fedha kwa Wakala wa Umeme Vijijini ili tuhakikishe kuwa kila Makao Makuu ya Wilaya nchini ina umeme kama tulivyoahidi. Pia kwa nia ya kuwapatia umeme wananchi wengi vijijini.
Mheshimiwa Waziri;
Miradi ya umeme ina gharama kubwa hivyo tuendelee kushirikiana na wabia wetu wa maendeleo. Nitumie fursa hii kuwatambua na kuwashukuru marafiki zetu na wabia wetu wa maendeleo wanaotusaidia katika kuendeleza sekta ya umeme nchini. Napenda, kwa ajili hii kuitambua Serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Millennium Challenge Corporation ambao wamekubali kutusaidia kujenga kituo cha uzalishaji umeme wa megawati 8 kwa kutumia maji katika mto Malagarasi. Umeme huo utainufaisha Kigoma na Kasulu.
Pia kwa msaada wa Serikali ya Marekani mifumo ya usambazaji umeme katika mikoa sita ya Mwanza, Iringa, Mbeya, Morogoro, Tanga, Kigoma na Dodoma itapanuliwa na njia ya pili ya umeme wa chini ya bahari kwenda Zanzíbar itajengwa. Naishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika inayotusaidia kufadhili miradi ya umeme katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga (Bukombe) na Arusha.
Vile vile naishukuru Benki ya Dunia ambao wanafadhili mradi mkubwa wa kukarabati, kuongeza na kuimarisha uwezo wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro ii kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika zaidi.
Kwa namna ya kipekee nawashukuru marafiki zetu wa Sweden kwa kukubali kugharamia mradi wa kupeleka umeme wa gridi Mkoa wa Ruvuma ambao utanufaisha wilaya za Sondea, Ludewa na Mbinga. Naambiwa utekelezaji wa mradi huo unategemewa kuanza hivi karibuni.
Ndugu Wananchi,
Nimeamua kuelezea mipango yote hii kwa kirefu ili kukumbusha kwamba dhamira yetu ya kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inasambaa nchini bado ipo pale pale, na bado tunaifanyia kazi.
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyojua, Shirika la Umeme TANESCO ndicho chombo kikuu cha kuendeleza uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa umeme kwa watu wetu. Serikali inatambua wajibu wake kwa Shirika hili na ninaahidi tutaendelea kuutimiza. Tunafanya hivyo sasa na hatuaacha kufanya hivyo siku za usoni. Lakini upo pia wajibu wa Shirika hili ambalo nafurahi mnaendelea kuutekeleza vizuri. Pamoja na hayo upo wajibu wa wananchi.
Wajibu wa kwanza unawahusu watumiaji wa umeme. Hatuna budi kulipa bili zetu za matumizi ya umeme kwa wakati. Tukifanya hivyo tunalijengea shirika uwezo wa kutimiza wajibu wake kwetu. Jambo la pili ambalo wananchi hatuna budi kufanya ni kusaidia katika ulinzi wa miundombinu ya usafirishaji wa nguzo za kusafirishia umeme, wizi wa nyaya za umeme na mafuta ya transfoma.
Ni jambo la kusikitisha sana kuona baadhi ya wananchi wenzetu wanafanya vitendo hivyo viovu vinavyosababisha watu wengine kukosa umeme na kuitia hasara Shirika na Serikali inayogharamia miradi hiyo. Nawaomba Watanzania wenzangu tusaidie Shirika na Serikali kwa kuwafichua wahujumu hawa ili wachukuliwe hatua zipasazo. Naamini baadhi yetu tunawajua. Watajeni na Shirika na Serikali iko tayari kuwapa tuzo wale watakaosaidia kutoa habari zitakazosaidia kutiwa nguvuni wahalifu hao ambao ni maadui wakubwa wa maendeleo ya taifa letu na watu wake. Tuwe na mayo wa uzalendo.
Ndugu Wananchi,
Baada ya kusema hayo naomba kwa furaha kubwa nihitimishe kwa kutamka kuwa kituo hiki cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi cha Ubungo kimezinduliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.


Nafurahi kusema kuwa, tukiondoa matatizo ya hivi karibuni ya mitambo mitatu ya Songas, mtambo mmoja wa Aggreko na mtambo wetu wa TANESCO kuharibika na kusababisha mgao mdogo wa umeme, suala la mgao tuliishaanza kulisahau kabisa. Hata hivyo, nafurahi kuhakikishiwa na wataalam kwamba matengenezo yanaendelea vizuri na tatizo la kutopatikana kwa umeme litaendelea kupungua kama si kuisha kabisa katika mfupi ujao.
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu, nchi yetu imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa umeme unaotokana na nguvu ya maji. Umeme huu ni wa gharama nafuu. Lakini tatizo linakuwa pale mvua zinapokuwa chache na kushindwa kujaza mabwawa ilipo mitambo ya kuzalisha umeme. Tatizo hili limetokea mara kadhaa huko nyuma lakini hatukuwa wepesi kujifunza.
Kwahiyo, baada ya kupata tatizo jingine kubwa mwaka 2005/2006, tukafanya uamuzi wa makusudi kabisa wa kuanza safari ya kupunguza utegemezi wa mvua katika upatikanaji wa umeme. Bahati nzuri sana, Mwenyezi Mungu ametujalia gesi asilia ya kutosha inayoweza kutumika kuzalisha umeme.
Tumeanza kupata mafanikio kwenye safari ya kwenda huko. Mwaka 2005, kiasi cha umeme wa unaozalishwa na gesi asilia uliongizwa kwenye gridi ya Taifa ulikuwa ni Megawati 283. Mwaka huu, hadi sasa, tumeongeza kiasi hicho na kufikia Megawati 431. Haya ni mafanikio makubwa, na bado tutaendelea na juhudi hizi za kuongeza kiwango cha umeme unaozalishwa kwa gesi asilia.
Hata hivyo, bado tunalo tatizo la gharama kwani mitambo kadhaa tunayoitumia sasa katika kuzalisha umeme kutokana na gesi asilia tumeikodisha (Songas, IPTL), tena kwa gharama kubwa. Maana yake ni kwamba tunanunua umeme, lakini vilevile tunalipa “capacity charges”. Tumefanya uamuzi kwamba na hili tatizo nalo tuondokane nalo kwani gesi ni ya kwetu, sio ya mtu mwingine. Hatuwezi kuzalisha umeme kwa gharama kubwa kana kwamba gesi nayo tunaagiza nje ya nchi.
Kwahiyo, kazi tunayoifanya leo hii, ya kuzindua mtambo wetu wenyewe wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ni hatua muhimu sana katika kupunguza gharama za kuzalisha umeme na kujitegemea kwa nishati hii muhimu. Katika mradi huu hakutakuwa na gharama za capacity charges kwasababu mtambo huu ni wetu wenyewe.
Ndugu Wananchi,
Tutaendelea na hatua za namna hii ikiwa ni pamoja kuangalia namna ya kununua mitambo iliyopo tayari ikiwa tutakubaliana bei na wenzetu hawa. Serikali pia itamiliki mradi wa megawati 45 unaoendelea kujengwa katika eneo la Tegeta, ambao tunaujenga kwa fedha zetu wenyewe na mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya Uholanzi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya nusu ya kwanza ya mwaka ujao 2009.
Vilevile, tutaendelea kufadhili miradi mbalimbali kadiri ya uwezo wa mapato ya serikali. Kwa kushirikiana na wadau wengine tutajenga njia ya msongo mkubwa wa umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga, Chalinze hadi Arusha, Kanda ya Kaskazini (North West Grid Extension) kutoka Bulyanhulu-Geita-Kibondo-Kigoma mpaka Mpanda-Sumbawanga hadi Mbeya.
Miradi mingine tunayoifanyia kazi ni ile ya ufuaji umeme ya Kinyerezi (Megawati 200), Mwanza (Megawati 60), Ruhudji (Megawati 358) na mingineyo. Vilevile, Serikali itaharakisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme kutokana na makaa ya mawe ya Kiwira na Mchuchuma. Aidha serikali itasaidia utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kujenga kituo cha umeme wa maji chenye uwezo mkubwa wa kuzalisha zaidi ya megawati 1200 cha Stiegler’s Gorge katika awamu mbalimbali.
Ndugu Wananchi,
Moja ya ahadi za CCM kwa wananchi ni kuhakikisha kwamba wananchi walio wengi zaidi wanapata huduma ya umeme. Serikali inakaribia kukamilisha lengo lake la kuhakikisha kuwa kila Makao Makuu ya Wilaya yanapata umeme. Hadi ifikapo mwisho wa mwaka ujao, tutakuwa tumebakiza Wilaya moja tu au mbili.
Aidha, Serikali imedhamiria kuongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini. Katika kufanikisha azma hiyo, tumeanzisha Wakala wa Umeme Vijijini. Katika hatua za awali za kutekeleza mpango wa usambazaji wa umeme vijijini, Serikali imeamua kununua mashine 17 za dizeli zenye uwezo wa jumla ya megawati 31 ili zifungwe kwenye maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa. Maeneo hayo ni Loliondo, Kigoma, Kasulu, Kibondo na Sumbawanga. Mradi huu ukikamilika wananchi wa maeneo haya watajikomboa kiuchumi kwa kutumia nishati hii kuendeleza miradi mbalimbali ya kujitegemea.
Aidha, kupitia Mfuko wa Millenium Challenge Corporation unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, kituo cha uzalishaji umeme kwa njia ya maji cha Megawati 8 cha Malagarasi kitajengwa, mifumo ya usambazaji umeme mikoa sita ya Mwanza, Iringa, Mbeya, Morogoro, Tanga, Kigoma na Dodoma itapanuliwa na njia ya pili ya umeme ya chini ya bahari kwenda Zanzibar itajengwa. Vilevile, Benki ya Maendeleo Afrika nayo inasaidia kufadhili miradi ya umeme katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga (Bukombe) na Arusha.
Isitoshe, Benki ya Dunia tayari inafadhili mradi mkubwa wa kukarabati, kuongeza na kuimarisha uwezo wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika zaidi.
Pia mradi wa kupeleka umeme wa gridi maeneo ya Ludewa, Songea na Mbinga unategemewa kuanza kutekelezwa hivi karibuni kwa kushirikiana na serikali ya Sweden.
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyojua, Shirika la Umeme TANESCO ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa letu. Serikali imefanya juhudi kubwa za kuliimarisha shirika hili kimfumo, kifedha na uendeshaji ili liwe na tija, liboreshe na kukidhi mahitaji ya wateja wa nishati ya umeme. Hivyo, sisi wananchi wote kwa ujumla wetu, tuna wajibu wa kulisaidia Shirika letu kwa kuilinda miundombinu yake katika sehemu zetu tunazoishi ili tuweze kunufaika na huduma nzuri ya umeme. Suala hili linahitaji msukumo wa ndani wa kila mmoja wetu.
Ni jambo la kusikitisha sana kuona baadhi ya wananchi wanabomoa transfoma tulizonunua kwa gharama kubwa sana kwasababu tu ya kuiba mafuta ya transfoma. Au unasikia watu wanakata nyaya za umeme kwa ajili ya kuziyeyusha na kuuza kwa watu wa vyuma chakavu. Serikali haiwezi kuweka askari kwenye kila transfoma au nguzo ya umeme nchi nzima. Wananchi ni lazima tuwe wazalendo, tujali mali za umma
ambazo zina manufaa kwetu sote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hongera JK, hongera wizara ya nishati na madini, na hongereni sana Tanesco. Hiyo ni hatua kubwa hapo mlipofika, maana hakuna kitu kinachoumiza kama 'Capacity charge' ingawa ipo duniani kote kwenye umeme unaozalishwa na makampuni binafsi lakini inaumiza, wawekezaje wanabeba faida kubwa kupeleka kwao wakati wananchi wanabeba mzigo mkubwa na hata hao wafanyakazi wazawa hawadhaminiwi. Huo sasa ni ushindani kwa IPTL (kwanza waondoke, hawa ingekuwa enzi hizi wangeshafikishwa mahakamani lakini ndio hivyo walibebwa enzi iliyopita)na Songas (waache kunyanyasa na kufukuza wafanyakazi bila sababu).

    Maisha bora kwa kila mtanzania yanawezakana, play your part.

    ReplyDelete
  2. hivi kwanini hotuba zetu huwaga ndefu mnooooo!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...