Kada wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Maneno Mbegu, akitangaza nia yake ya kutaka kugombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe, katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa CCM, Mjini Kisarawe, mkoani Pwani. Kutoka kushoto ni Katibu wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Zena Mgaya na Haruna Meza ambaye ni Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa wilaya hiyo.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho wakisikiliza kwa makini wakati Maneno Mbegu akitangaza nia yake ya kutaka kuwania ubunge jomboni humo katika Uchaguzi Mkuu ujao. Katibu wa CCM,Wilaya ya Kisarawe, Zena Mgaya akitoa pongezi kwa Maneno Mbegu kwa kutanga nia yake hiyo, bila kuwakashifu viongozi waliopo madarakani. Katibu wa CCM,Wilaya ya Kisarawe, Zena Mgaya akitoa pongezi kwa Maneno Mbegu kwa kutangaza nia yake hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Vulu (kushoto) akisalimiana na Maneno Mbegu muda mfupi kabla ya Mbegu kutangaza nia yake.
UONGOZI WA Chama Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Kisarawe, umempongeza Kada wa chama hicho, Maneno Mbegu kwa kitendo chake cha kutangaza nia yake ya kutaka kugombea ubunge wa Jimbo hilo kwa kutowapaka matope viongozi waliopo madarakani.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Zena Mgaya mara baada ya Mbegu kumaliza kuwatangazia wanaCCM, nia yake ya kutaka kuwania nafasi hiyo, juzi katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa CCM Mjini Kisarawe.

"Nimefurahi umejieleza vizuri, bila kuwakashifu viongozi wengine,ndivyo
inavyotakiwa, na nakuomba hata huko mbele ya safari uwe unafanya hivyo," alisema Mgaya na kuwapa fursa wanachama kumuuliza maswali Mbegu.

Mgaya, aliwaasa viongozi wa CCM, kuacha tabia ya kwenda mitaani kuwapigia debe waliotangaza nia ya kugombea, akidai kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwaharibia wao sifa za uongozi pamoja na kuwawekea mazingira magumu wagombea hao watakaopewa fursa baadaye kujieleza kwa wanachama ambao watawapigia kura na mmoja wao kufanikiwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo hilo.

Awali kabla ya kuanza kujieleza, Mbegu ambaye hivi karibuni ameteuliwa na Mkuu wa Mkoa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa, iliyopo Jijijni Dar es Salaam,aliwashukuru viongozi na wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Mbegu, alisema kuwa elimu na uzoefu alioupata kwa kutembelea nchi mbalimbali duniani, atahakikisha anavitumia kuliendeleza Jimbo hilo kwa ushirikiano na wananchi.

"Nimezaliwa Kisarawe,nimesoma Kisarawe kwa kutumia kodi zenu, hivyo sina budi kurejea kuiendeleza Kisarawe,"alisema Mbegu na kuongeza, "Mimi ni miongoni mwa wanachama wanzilishi wa CCM, 1977,Nimeamua kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo hili, kwa vile najua kuwa ni haki yangu ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa," alisema Mbegu.

Alisema kuwa wakati utakapofika atafafanua zaidi ni namna gani atakavyoshirikiana na wazee, wadogo zake na wananchi kwa ujumla kuiendeleza Kisarawe. Mbunge wa Jimbo hilo kwa hivi sasa ni Mh. Athuman Janguo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 01, 2010

    Mimi ningependa viongozi mliopo madarakani na ambao mnataka kuingia madarakani kwa kupitia wilaya ya kisarawe jamani acheni siasa,mimi si raia wa huko bali nimefanya utafiti wangu katika wilaya hiyo,ni majonzi na huzuni kubwa sana kwa jamii ya kisarawe,watu hawana maji wanakunywa maji machafu kabisa na bado yanapatikana mbali kabisa.hebu waoneeni huruma hao watu jamani naaamini nusu mshahara wa mbunge anaweza kuwachimbia visima hata vitano katika wilaya nzima.acheni siasa na kujilimbikizia mali wakati watu wanaumia.
    mkereketwa.

    ReplyDelete
  2. Inasikitisha sana kwene wilaya hizi Kisarawe na Mkuranga watu wanataabika wabunge wao hawana huruma nao hata kidogo,huwezi amini mtu kijana kama Adam Malima pamoja na pesa yote aliorithi bado anashindwa kuwa na huruma kwa watu wake,kama alivosema mdau hapo juu kuhusu maji ni mfano mmoja tu huu.mengine ningependa Michuzi awe kama Mjengwa kutuwa picha za hali halisi ya vijijini badala ya party na harusi kila kukicha najuwa hutoituma hii kwani inamuhusu Malima.Unavomfikilia wewe ni tofauti alivo huyu mtu.mimi nilitegemea sana angeleta changa moto kutokana na ujana na kuwa hana njaa kumbe wapi ni kibri dharau kwa watu wake we acha tu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 01, 2010

    Mzee Janguo it is about time ung'atuke kama anavyosema Prof. Jay. Waache wengine wenye mtizamo mpya wafanye kazi.Nakushauri uisikilize nyimbo ya Prof. Jay kwa makini sana Mzee Janguo.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 01, 2010

    kweli kabsaa.wilaya hii hainaga maendeleo kabisaa.pia wananchi waache imani za uchawi watilie mkazo maendeleo jamani.imani za kishirikina zinarudisha maendeleo nyuma.vijiji vya Vigama,Mwanarumangu tumwamini YESU ushirikina umepitwa na wakati.kha!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...