Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego (Kulia) akisisitiza jambo juu ya ngoma za asili wakati akizungumza na wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Jivunie Tanzania,Bi.Mariam Ismail na Agnes Kimwaga,Afisa Uhusiano wa BASATA.
Mdau kutoka Business Times,Humphrey Shayo akitaka kujua juu ya sanaa mbalimbali za asili zinazofanywa na kundi la la Sanaa la Jivunie Tanzania na nafasi yake kwa sasa.
Baadhi ya wasanii wazee wa Kundi la Sanaa la Jivunie Tanzania wakicheza Ngoma ya Manyanga na kutambika kabla ya wasanii wengine wa kundi hilo hawajaja Jukwaani kumwaga burudani kedekede za asili.
Wasanii wakiwajibika kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia burudani kutoka Kundi la Sanaa la Jivunie Tanzania.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kwamba,ngoma za asili bado zina hadhi na nafasi kubwa katika jamii zetu ingawa kwa maeneo ya mijini mwamko wa sanaa hiyo unaonekana kupungua tofauti na zamani.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,ngoma za asili zipo kama kawaida na zimekuwa na nafasi kubwa mikoani ambako zimekuwa zikivuta watu wengi.

“Kuna matamasha makubwa ya ngoma za asili kama yale ya Makuya, ya kale yanapokutana na ya sasa, Bujora na Chamwino.Matamasha haya yamekuwa yakivuta watu wengi sana hivyo,dhana kwamba ngoma za asili zimetoweka si sahihi” alisema Materego.

Aliongeza kwamba,kinachotokea kwa sasa ni athari za utandawazi kwenye ngoma za asili ambazo zimebadili upepo wa sanaa hiyo maeneo ya mijini lakini akasisitiza kwamba,bado hata maeneo ya mijini kuna vikundi vingi vya ngoma za asili vinavyofanya vizuri.

“Utandawazi kwa kiasi fulani umeathiri ngoma za asili hasa maeneo ya mijini lakini bado hata hivyo kuna vikundi vingi Baraza limevisajili na kuvisimamia mijini kama hiki kilichotuburudisha leo cha Jivunie Tanzania” Alisisitiza Materego.

Alitoa wito kwa wakuzaji sanaa kujikita kwenye kuandaa matamasha mbalimbali ya sanaa za asili ili kuzidi kuisambaza sanaa hiyo ambayo ni muhimu sana kwa utambulisho wa utamaduni wetu na kwa muda mrefu imelijengea heshima taifa letu.

“Ni kweli tuna matamasha mengi ya ngoma za asili lakini ni wazi juhudi nyingi zinahitajika ili kujenga mwamko zaidi katika sanaa hizi.Ni muhumu ikaeleweka kwamba,sanaa hizi zinabeba kila kitu ndani ya jamii” alimalizia Materego.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Jivunie Tanzania,Bi.Mariam Ismail alisema kwamba, watanzania wasiache kupenda ngoma za asili na kupapatikia vitu vya nje kwani kufanya hivyo ni kupuuza malezi na historia za jamii zao.

Jukwaa la Sanaa kila mwisho wa mwezi linapambwa na burudani mbalimbali na kwa mwezi huu Kundi la Sanaa la Jivunie Tanzania kutoka Temeke Dar es Salaam lilitoa burudani kedekede za asili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 29, 2011

    Jambo kubwa kama hili, haliwezi kupata majibu mepesi na yenye kujitia moyo kama haya ya Basata. Ni ukweli usiopingika kwamba utamaduni kwa ujumla umeathiriwa sana na mambo mbalimbali ikiwemo utandawazi, ukosefu wa sera madhubuti (au zipo lakini katika makabrasha) ukosefu wa meno au nguvu za kuzisimamia nk. Athari hiyo siyo kwa nchi yetu tu ni karibu kila sehemu duniani. labda ningemkumbusha Basata kuwa siyo ngoma za asili tu zinazoathirika, ni pamoja na Lugha, mambo ya kitamaduni, nyumba, chakula, mavazi nk. Siyo rahisi sana.

    Ni kweli kuna vikundi vya ngoma au utamaduni vinajaribu kuonyesha ngoma, Lakini kiukweli si ngoma asili ndizo huwa zinaonyeshwa, bali ni zilizochakachuliwa ili kufurahisha watazamaji. Inashangaza siku hizi hata baadhi ya ngoma za kisukuma wakinamama wanacheza kwa kukata kiuno. Uliona wapi. Wasukuma kinamama au kina baba hawakati viuno. kwa hiyo basi hiyo siyo ngoma ya kisukuma kwa uhalisia.

    Nini maoni yangu.
    1. Serikali ilitambue hili tatizo na kulitengenezea sera za makusudi.
    2. Kurudisha hata baadhi ya watawala wa kiasili (Kwa sababu ndiyo walikuwa custodians wa traditions and norms)
    3. Kwa kuwa tuna shule za kata na kwamba hakuna tena msukuma kwenda kusoma umakondeni, basi lugha asili sifundishwe mashuleni.Kuwepo na vitabu vilivyoandikwa kwa lugha asilia.
    4. Kuwepo na siku za utamaduni kitaifa, kikanda, na kimkoa,
    5. Maeneo yaliyotambulika kama niya asili kwa matambiko, yahifadhiwe na kuruhusu matambiko na mila na desturi kushamiri.
    6. Utemi au uchifu unaoendelea utambuliwe na kupewa ruzuku na serikali. Tupinge hii hali ya kutawazwa machifu kishabiki. Iwe ni kiukweli.
    7. Kuwepo na recognition kwa viongozi wa kimila waliopo na wasaidiwe na serikali.
    8. Katiba mpya iingize vipengele vyenye madhumuni mahsusi kulinda utamaduni wa Tanzania na si ngoma pekee. (Ngoma za asili ni sehemu nzima ya utamaduni) Kila ngoma ina maana yake: Harusi, mavuno, sungusungu, tambiko, janga, mwali, nk nk nk.

    Tuchangie.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...