Na Mwandishi wetu,Tunduru
WAKULIMA wa zao la korosho wa mikoa ya Mbeya,Njombe na Ruvuma
wanaohudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma(Tamcu),wamevuka lengo la uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa
kilimo 2023/2024.
Ni baada ya kufanikiwa kuzalisha na kuuza jumla ya tani elfu 26.066
sawa na kilo milioni 26,066,333 zenye thamani ya Sh.bilioni
45,531,514,557 sawa na ongezeko la tani 1,000 ikilinganisha na msimu
uliopita ambapo walizalisha kiasi cha tani 25,000.
Kaimu meneja wa Tamcu Marcelino Mrope amesema hayo jana,wakati
akizungumza na wanachama wa chama cha msingi cha Ushirika
Ligunga(Ligunga Amcos) katika mnada wa nane na wa mwisho katika msimu wa
kilimo 2023/2024.
Mrope alisema,hayo ni mafanikio makubwa kwa wakulima na Chama hicho
katika uzalishaji wa korosho ambapo amewapongeza wakulima kwa kazi
nzuri waliyoifanya mashambani kwa mwaka 2023/2024.
Ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima, hali
iliyohamasisha wakulima wengi kurudi mashambani kwa ajili ya kufufua
mashamba yao.
“kwa mfano katika msimu huu wa kilimo 2024/2025 tumepewa pembejeo zenye
thamani ya Sh.bilioni 22.5 kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi
ipate Uhuru,tunaamini pembejeo hizi zitakwenda kuongeza sana uzalishaji
wa korosho katika wilaya yetu”alisema Mrope.
Amewashauri wakulima kutumia vizuri fedha walizopata kununua pembejeo
na kutumia mvua zilizoanza kunyesha kuanza maandalizi ya msimu mpya wa
kilimo 2024/2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAMCU Mussa Manjaule alisema,bei ya
korosho katika msimu wa mwaka huu haikuwa nzuri ikilinganisha na msimu
uliopita,hata hivyo amewataka wakulima kutokatishwa tamaa badala yake
waendelee kulima zao hilo ambalo ni nguzo kuu ya uchumi wao na wilaya
ya Tunduru.
Manjaule,ametoa ushauri wake kwa wakulima kuanza kulima mazao mengine ya
chakula na biashara ikiwemo zao maarufu la mbaazi ambalo lina soko la
uhakika na bei kubwa na halihitaji gharama kubwa katika uzalishaji
wake.
Naye afisa ushirika wa wilaya hiyo Georg Bissan,ameipongeza bodi ya
chama kikuu cha ushirika(Tamcu) kwa kusimamia vyema mauzo ya korosho kwa
mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewezesha wakulima kuwa na soko la
uhakika na kupata fedha zao kwa wakati.
Amewaasa wakulima kutumia fedha walizopata kufanya mambo ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa nyumba bora,kusomesha watoto na kuanzisha shughuli
nyingine zitakazowaingizia kipato badala ya kutumia fedha hizo kwenye
ulevi na uesharati.
Rashid Millanzi mkulima wa korosho,ameipongeza serikali kupitia chama
kikuu cha ushirika(Tamcu) kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani,hata
hivyo ameiomba kutafuta wafanyabiasha wengi watakaokwenda kununua
korosho kwa bei nzuri inayolingana na gharama za uzalishaji wake.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule akizungumza na wakulima wa korosho wa kijiji cha Ligunga(hawapo pichani) baada ya kukamilika kwa mnada wa 8 na wa mwisho wa ununuzi wa zao la korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu wa kilimo 2023/2024 ambapo jumla ya kilo milioni 26,066,333 za korosho zenye thamani ya Sh.bilioni 45 zimezalishwa na kuuzwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...