Na Dotto Kahindi.
Nianze kwa kuwasalimu na kutoa shukran zangu kwa Blogu hii kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja yangu ambayo inalenga kuishirikisha jamii katika kupata suluhisho la ajali za barabarani ambazo zimekuwa ni janga kubwa la kitaifa.
Mara kadhaa niliwahi kusikia takwimu za vifo vinavyotokana na magonjwa mbalimbali yakiwemo UKIMWI, Malaria, Vifo vya mama wajawazito n.k, na vifo hivi vilitia uchungu sana kwa jamii kiasi kampeni kadhaa zilianzishwa ili kupunguza vifo hivyo au kuvikomesha kabisa.

Jamii kwa kutambua athari zilizokuwa zikisababishwa na majanga hayo kijamii,  kiuchumi na kitaifa waliunga mkono kampeni hizo kwakuwa wao pia walikuwa wahanga wakuu na walipaswa kushiriki katika kubadili tabia na mienendo ili kuelekea kwenye Tanzania iliyo salama.

Nasikitika kutangaza kuwa Tanzania sasa kuna ugonjwa mpya unaitwa AJALI, kila siku ajali zinapoteza maisha ya wapendwa wetu. 

Takwimu zilizotolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dr. Harrison Mwakyembe mwisho wa wiki iliyopita zinaonyesha watu 1,126 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani kwa kipindi cha miezi mitatu, huku majeruhi ni 3,827 katika ajali 3,338.

Idadi hii ya ajali na vifo siyo ya kawaida, inatisha na kusikitisha sana ni wakati huu tunatakiwa kupambanua na kupata dawa ya kukabiliana na janga hili la ajali.

Tunaanzaje? Nani tuanze kumbana anayechangia ajali hizi? Ni maswali tunatakiwa kuyajibu kwanza kabla ya kuanza kutoa lawama, ni lazima tujue akina nani wanaohusika kwenye sekta hii ili tupate pa kuanzia kama tunataka kuziba ufa kwelikweli.

Mwakyembe ameunda kamati maalumu ya kutafuta chanzo na dawa ya ajali hizo, nimeona ni vyema kuunga mkono jitihada hizo kwa kuanzisha kampeni ya #DerevaMakini ambayo inalenga kuishirikisha jamii katika kukabiliana na ajali hizo ambazo zimekuwa mwiba kwa taifa. 

Kwa maoni yangu wafuatao ni wadau wa moja kwa moja wa sekta ya usafiri ambao wakitekeleza sawasawa majukumu yao ajali zitapungua; Askari wa Usalama Barabarani, Madereva, Abiria, Wamiliki wa vyombo vya usafiri, TRA, Sumatra, Bima, Vyombo vya habari, Tanroads, Miundombinu , NIT na vyuo vya namna hiyo, TBS, Wauzaji wa magari, mafuta na vipuli vya magari. 

Kupitia forum hii naomba kupata ushiriki wako mdau ili tutajadili kwa pamoja, toa maoni yako, ushauri na mapendekezo ukizingatia wadau waliotajwa hapo juu, maoni yako tutayatumia kwenye mada ifuatayo ambayo itakwenda kuchambua majukumu ya mdau mmoja mmoja.

Hii ni Kampeni ya Usalama barabarani yenye lengo la kupunguza ajali za barabarani ikilenga hasa mabasi ya abiria na imewezeshwa na Michuzi Blog, Tabianchi Blog na Transevents Marketing Limited.

Makala haya yatakuwa yakikujia kila wiki, kwa taarifa zaidi tembelea ukurasa wetu wa facebook

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Mawazo yako ni.mazuri sana na ninayaunga ILI KAMA TAIFA tupate suluhisho la kudumu.
    Najua kila mtu ananamna yake yakuchangia mada na NAOMBA SANA kila mtu achangae kipingele anachoweza kuchangia. Kama ni zaidi ya kimoja basi ni vizuri zaidi.
    Washiriki tukinuia kusaidiana hilitutafanikiwa. Lengo langu.mwanzilishaji mada ni kuchangia tu.
    Naona rather than kuanzia wapi tushike point na tuendelee kwa maana mada zote zinategemeana.
    Dereva apate elimu ya kuendesha na katika mtihani kuwe na maswali ya ethics na pia kuwe na namna ya kupima accountability ya dereva. Hili ni wazo la kufikiria maana hadi sasa dereva akiua si tatizo.
    Dereva awe na road test kila baada ya miaka miwili na kama ameshafanya ajali basi ifuatiliwe na penalty ya point kuondola kwenye lesseni.
    Kila kampuni itafute jinsi gani watajali na kuhamasisha dreva wake. Wanaweza kuwa zawadia hela au kuchangia mfuko wa kusomesha watoto wao au kuchangia kwenye shida au swala linalo mgusa dreva pengine inaweza kuwa shughuli za ujasirimali wa familia wa dereva. Nacho sema hapa kumsaidia asitafute hela za kuiba au rauti za kuongeza iliapeleke ziada anakopeleka. Kwa maana kwamba akipewa benefits fulani ataijali kazi yake zaidi.
    Dereva nae ni mtu akipewa training yaani mafunzo ya shirikiana na muajiri kujenga uhusiano mzuri na wateja kila mtu atanufaika. Biashara itakuwepo, hadhi ya dereva na kampuni itaongezeka na pia wateja wataendelea kufurahia kusafiri na kampuni kama haya.
    Natarajia kuna mengi yata zungumziwa na wadau wengi tu, yangu haya ni machache tu kuhusu ya dereva.
    Wengine muongezee kuhusu dereva na pia mnaweza zungumzia ya SUMATRA, waajiri, sheria za usalaama barabarani pamoja na Traffic polisi, miundo mbinu na mengineo.

    ReplyDelete
  2. Bila kiongozi wa ngazi ya juu kujiuzulu kwa ajili ya hizi ajali hakuna kitakachofanyika kwani watu wengi wameshaongea kuhusu hili lakini hakuna linalotekelezwa. Nina uhakika wakiona kuna kupoteza kazi kila kitu kitaenda sawa. Njia za kutoa leseni hazifai wahusika watolewe mara moja ni bora kuwa watu wachache wanaosimami udereva wa magari ya abiria, wawe watu makini.
    Mimi Degelavita, Bergen, Norway

    ReplyDelete
  3. Binafsi nampogeza mwaandishi wa Mjadala huu,nawaponeza wadhamini wa wa Mjadala huu, na kikubwa zaidi nahisi ni jambo muhimu sana kuchambua vipengele vilivyoanishwa na mwandishi huyu,na kisha nawasihi watu kutoa maoni yao katika jambo hili muhimu ambalo kitaifa ni janga lisilostahili kupuuziwa kama ambaye utasoma comment hii pasipo kuchangia lolote..

    ReplyDelete
  4. Degelavita na Mwenzetu ambaye hujataja jina, michago yenu safi sana, tunaweza kuziba ufa pale tunapoujua ufa wenyewe uko wapi, na ndio maana maoni yenu yananipa mwanga wa kuleta mjadala ujao kwa kuwachambua wadau wa usafiri, tuendelee kupambana kwa pamoja

    ReplyDelete
  5. Ikiwa ndiyo maandalizi ya wiki ya nenda kwa usalama,binafsi nafikiri hii wiki haina tija yoyote,zaidi ya kutulazimisha kununua sticker za wiki ya nenda kwa usalama,ukiuliza sticker ile ina kazi gani nadhani hata wanao ziuza hawawezi kueleza maana yake.Tubadilike tusifanye kazi kwa mazoea, unakuta askari barabarani anakukamata anakwambia huna stiker, anabandika kwenye gari yako kisha anakudai sh.10,000/=,sticker yenyewe ndogo na kwanza imebandikwa kwenye kioo mtu aliye mbele ndiyo anaisoma sasa sijui anawekewa dereva au askari aje aisome, na baada ya hapo nini hufuata baada ya wiki hii?maisha yale yale watu spidi mwanzo mwisho...tubadilike we are commiting genocide...

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...